2,500 kuliamsha kwa siku tatu Rombo Marathoni 2025

WAKATI wanariadha 2,500 wakitarajiwa kushiriki msimu wa nne wa mbio za Rombo Marathon, taarifa njema ni kwamba tofauti na misimu iliyopita safari hii mbio hizo zitafanyika kwa siku tatu mfululizo.

Tamasha la mbio hizo limepangwa kuanza Desemba 22, 2025 kwa washiriki kufanya utalii chini ya Mlima Kilimanjaro katika misitu ya Kinapa kupitia muongozo wa Wakala wa Misitu Tanzania (TFS).

Katibu Mkuu na mratibu wa mbio hizo, Similwa Mdumbwa aliliambia Mwanaspoti, Desemba 23 itakuwa ndiyo siku ya mbio zenyewe na washiriki watachuana katika umbali wa kilomita 5, 10 na kilomita 21 (nusu marathoni).

Mbio hizo itaanzia na kumalizikia kwenye viwanja vya Kilombero, Rongai Forest, wilayani Rombo, Kilimanjaro, huku zikishirikisha wakimbiaji zaidi ya 2500.

Akizungumza katika uzinduzi wa mbio hizo jana Dar es Salaam, Mdumbwa alisema Rombo Marathon yenye kauli mbiu ya ‘Mbio na Burudani’ itakwenda sanjari na tukio la Ndafu Festival.

“Itakuwa ni zaidi ya mbio, watu watapata fursa ya kula vyakula vya asili na kinywaji aina ya mbege mara baada ya mbio ndio sababu kauli mbiu yetu ni mbio na burudani,” alisema Mdumbwa na kuongeza, Desemba 24 itakuwa ni hitimisho la mbio hizo na wakimbiaji wote watashiriki kupanda miche ya miti 10,000 kwenye eneo la chini ya Mlima Kilimanjaro.

“Rombo Marathon na Ndafu Festival ni zaidi ya mbio, linakwenda kuwa jukwaa la kuimarisha umoja, kudumisha utamaduni wa eneo letu, kukuza vipaji na kutangaza vivutio vya utalii vya Tanzania,”  alisema Mdumbwa.

Alisema usajili wa washiriki unaendelea kwenye tovuti ya mbio hizo na katika baadhi ya vituo vya Dar es Salaam na nje ya Dar es Salaam ambako kuna matawi ya benki wadhamini wa mbio hiyo ikiwamo mdhamini mkuu, KCB na benki ya Mwanga Hakika.

“Gharama ya ushiriki ni Sh 40,000 kwa kila mshiriki kwa umbali wowote,” alisema Mdumbwa na kufafanua sababu za kufanyika kwa siku tatu mfululizo ikiwa mapendekzo yaliyotokana na maoni ya washiriki wa misimu iliyopita.

Mwakilishi wa Shirikisho la Riadha Tanzania (RT), Felix Chunga alisema mbio ya Rombo Marathon imekuwa chachu ya kuibua na kuendeleza vipaji vya riadha nchini.

“Imeendelea kufanya vizuri, ikitoa zawadi kwa washindi na kuwavutia wanariadha wengi kushiriki, kupima muda wao na washindi kuondoka na zawadi mbalimbali kutoka kwa waandaaji. Imekuwa moja ya mbio yenye mchango mkubwa katika ustawi wa wanariadha wetu, kama haitoshi imekuwa ikileta watalii, jambo linalozidi kuifanya kuwa kubwa,” alisema.

Gabriel Lekundayo, akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya KCB, Cosmas Kimario,  alisema mbio hizo zina manufaa makubwa kiafya na kiuchumi pia.