Aliyeanza na mtaji wa elfu mbili, apewa Sh5 milioni, kiti mwendo

Sengerema. Baada ya dhiki, faraja. Ndivyo ilivyokuwa kwa mkazi wa Sengerema aliyepata ulemavu wa kudumu baada ya kudondokewa na kifusi mgodini, lakini akaanza kujiajiri kwa kushona viatu kwa mtaji wa Sh2,000.

Mwananchi huyo alikuwa miongoni mwa walioudhuria mkutano wa hadhara wa Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Kenani Kihongosi uliofanyika wilayani Sengerema mkoani Mwanza, ambapo alijikuta akitoa machozi ya furaha baada ya kupewa mtaji wa Sh5 milioni, kitimwendo na ahadi ya kupatiwa eneo la biashara.

Akieleza changamoto yake, kijana huyo alisema alipata ulemavu baada ya kudondokewa na kifusi mgodini, hali iliyosababisha miguu yake kupooza.

“Miguu yangu ilipooza, lakini niliona mikono yangu ipo salama, hivyo nikaanza kushona viatu kwa mtaji wa Sh2,000. Naomba nisaidiwe kitimwendo ili iwe rahisi kufika kazini,” amesema.

Baada ya maelezo hayo, Kihongosi alimpa Sh5 milioni kwa ajili ya kukuza biashara yake na kuahidi kumnunulia kitimwendo, huku akimuagiza Mkurugenzi wa Halmashauri ya Buchosa, Benson Peter kumtafutia eneo la kufanyia biashara.

Hatua hiyo ilipokewa kwa shangwe na wananchi waliokuwa kwenye mkutano huo.

Mbali na hilo, Kihongosi ametoa motisha ya Sh500,000 kwa mzee Idu Cosmas aliyesema alipigania nchi wakati wa Vita ya Kagera lakini hajawahi kunufaika na chochote.

Wananchi wa Sengerema wakiwa kwenye mkutano wa hadhara wa Katibu wa NEC, Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Kenani Kihongosi

Kihongosi amesema Serikali inashughulikia suala la malipo ya wazee waliopigania nchi na kwamba mchakato unaendelea baada ya kuwataka kufungua akaunti za benki.

Katika mkutano huo pia aliibua wasiwasi kuhusu ujenzi wa madaraja katika vijiji vya Isenyi na Nyamadoke baada ya wananchi kudai ujenzi wake umesimama.

Amemuagiza Mkuu wa Wilaya kufanya ukaguzi na kutoa taarifa kabla ya kumaliza ziara yake mkoani Mwanza.

Wananchi pia wamelalamikia ubovu wa barabara ya Sengerema–Nyehunge inayosababisha ajali mara kwa mara, hasa kwa waendesha bodaboda.

Katibu wa NEC, Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Kenani Kihongosi, akikagua mradi wa ujenzi wa soko la Bukokwa, Sengerema.

Akilifafanua hilo, Meneja wa Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads), Makori Kisare amesema barabara hiyo tayari imeingia mkataba na mkandarasi na ujenzi wake utaanza wakati wowote.

Kihongosi amesema mkakati wa Serikali ni kuhakikisha kila kijiji na kitongoji kinapata umeme ifikapo mwaka 2030 kwa mujibu wa Ilani ya CCM.

Wananchi pia walitoa kero nyingine zikiwemo mikopo ya wajasiriamali, huduma za afya kwa wajawazito, ukosefu wa manesi katika zahanati ya Mahurukenda, pamoja na ukosefu wa wakalimani wa lugha ya alama kwa watu wenye ulemavu wa kusikia katika mikutano ya hadhara.

Kihongosi ameomba radhi kwa kutokuwepo kwa wakalimani wa lugha ya alama na kuahidi kufanyia kazi suala hilo.