Wanafunzi Hatarini Kuzama! Wakazi Waomba Daraja la Kudumu la Mto Fahhay, Babati – Video

Global Publishers
March 12, 2026
0 Comments

BABATI, MANYARA — Wakazi wa mitaa ya Mruki na Msasani katika Halmashauri ya Mji wa Babati wamesihi Serikali kuingilia kati kwa haraka na kujengea daraja la kudumu katika Mto Fahhay, ili kuondoa hatari kwa wanafunzi takribani 200 wa Shule ya Msingi Shikizi ya Mruki, ambao wanapaswa kuvuka mto huo kila siku kupitia daraja la mbao kwenda shuleni.

Mwenyekiti wa Bodi ya Shule hiyo, Bakari Said, amesema kwamba daraja hilo la mbao limekuwa msaada mkubwa kwa wanafunzi kwa zaidi ya miaka mitatu, lakini sasa limeanza kuharibika kutokana na mbao na miti iliyotumika kuanza kuoza, huku idadi ya watumiaji ikiongezeka.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Mruki, Abdilahi Rajabu, amesema daraja hilo ni kiungo muhimu kinachounganisha mitaa ya Sinai na Mruki, na asilimia kubwa ya watoto kutoka maeneo hayo wanasoma katika Shule ya Msingi Shikizi ya Mruki.

Wakazi wamesema kwamba wakati wa mvua kubwa, mto huo hujaa maji na wakati mwingine maiti kutoka maeneo ya juu husombwa na maji kupita katika mto huo, jambo linaloongeza hofu na hatari kwa wanafunzi na wananchi wanaovuka kila siku.

Kutokana na hali hiyo, wakazi hao wanaiomba Serikali kuingilia kati haraka kwa kujenga daraja la kudumu na salama, ili kulinda maisha ya wanafunzi na wananchi wanaotumia njia hiyo kila siku.