Dar es Salaam. Wakati Mwenyekiti mpya wa Chama cha Wananchi (CUF), Mirambo Yusuf akianza juhudi za kufanya maridhiano ya ndani, upande unaompinga umedai mchakato huo hautakuwa na maana iwapo hatajiuzulu.
Mirambo, aliyechaguliwa Februari 22, 2026 kuongoza chama hicho kwa kipindi cha miaka mitano ijayo, yupo katika ziara ya kujitambulisha kwa viongozi wa chama ngazi ya wilaya na wanachama, sambamba na juhudi za maridhiano.
Uchaguzi uliomweka madarakani ulizua mjadala baada ya kufanyika kufuatia maelekezo ya Msajili wa Vyama vya Siasa ya kutengua uchaguzi uliomweka madarakani mtangulizi wake, Ibrahim Lipumba pamoja na viongozi wenzake, uliokuwa umefanyika Desemba 18 na 19, 2024.
Msajili alifuta matokeo hayo akieleza washindi hawakupata zaidi ya nusu ya kura za wajumbe waliopiga kura, hivyo uchaguzi ulipaswa kurudiwa kwa mujibu wa Katiba ya chama ya mwaka 1992 na kanuni zake.
Uamuzi huo ulisababisha mgawanyiko ndani ya chama, ambapo baadhi ya wanachama waliunga mkono hatua ya Msajili huku wengine wakipinga na kuamua kwenda mahakamani.
Akizungumza na Mwananchi leo Alhamisi, Machi 12, 2026, Makamu Mwenyekiti Bara wa zamani wa chama hicho, Othman Dunga, amesema hawana tatizo na maridhiano, lakini hayawezi kuwa na maana kama kiongozi hajapatikana kwa uchaguzi halali wa wajumbe.
“Walimpigia kura si wanachama halali wa CUF. Hatuwezi kufanya maridhiano na mtu aliyepatikana kwa njia haramu,” amesema.
Dunga amesema baada ya kufanya utafiti wamebaini wajumbe 288 waliohudhuria mkutano wa kumchagua Mirambo hawakuwa halali, na ushahidi huo wameuwasilisha kwa Msajili wa Vyama vya Siasa.
“Mirambo hana sifa ya kutuita kufanya mazungumzo. Anatakiwa kujiuzulu kwa sababu hakuchaguliwa na wajumbe halali wa Mkutano Mkuu,” amesema.
Amesema suluhu ya kudumu ni kuitishwa mkutano mkuu mpya ili kila mwanachama apate fursa ya kushiriki kwa mujibu wa katiba ya chama.
Awali, Mirambo amesema yuko tayari kuzungumza na wanaopinga ushindi wake, iwe kupitia mahakama au kwa Msajili wa Vyama vya Siasa.
“Tutawawekea utaratibu ili tufanye maridhiano. Lazima tuweke msingi mzuri wa kumaliza tofauti zetu,” amesema.
Amesema anapanga kuzungumza moja kwa moja na viongozi wanaopinga uongozi wake ili kupata suluhu ya mgogoro huo.
“Nataka kuzungumza nao moja kwa moja kwa sababu sioni tatizo. Lengo ni kumaliza tofauti na kujenga chama,” amesema.
Katika hatua nyingine, akiwa mkoani Mwanza, Mirambo ameanza mazungumzo na makundi yanayopingana ndani ya chama hicho ikiwa ni sehemu ya juhudi za maridhiano.
Mkoani humo kulikuwa na mgogoro wa uongozi katika Wilaya ya Ilemela tangu mwaka 2025 uliosababisha kuwepo kwa makatibu wawili wa wilaya.
Katika mgogoro huo, Karim Moshi ameridhia kukabidhi ofisi kwa Ng’ongo Fereji ambaye sasa anahudumu kama Kaimu Katibu wa Wilaya ya Ilemela.
Mirambo amesema awali kulikuwa na mkanganyiko wa uongozi uliosababisha kila upande kuitisha vikao vyake, hali iliyochochea mgogoro.
Amesema baada ya mazungumzo na pande zote mbili wamekubaliana kumaliza mgogoro huo bila hata kuitisha kikao kilichokuwa kimepangwa kufanyika Jumapili.
“Katika kikao hicho tutathibitisha kwa wanachama kuwa tatizo limekwisha na sasa tuanze kufanya kazi ya kujenga chama,” amesema.
