Iran imetuhumiwa kushambulia meli mbili kubwa za mafuta katika Ghuba ya Uajemi kwa kutumia boti zilizokuwa zimebeba vilipuzi, tukio lililosababisha milipuko mikubwa na moto mkali uliowalazimu wafanyakazi wa meli hizo kukimbilia kuokoa maisha yao.
Video ya tukio hilo inaonyesha moshi mzito mweusi ukipaa juu angani kutoka kwenye meli zilizokuwa zimebeba mafuta ya Iraq, huku moto mkubwa ukiendelea kuwaka chini yake baada ya shehena ya mafuta kulipuka.
Kwa mujibu wa mamlaka za Iraq, mfanyakazi mmoja alipoteza maisha wakati meli hizo ziliposhambuliwa, huku wengine wakikimbia kwa haraka kujiokoa wakati moto ulipokuwa ukisambaa.
Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni ya Bandari za Iraq, Farhan al-Fartousi, alisema kuwa meli mbili za kigeni zilizokuwa zimebeba mafuta ya Iraq zilishambuliwa zikiwa ndani ya maji ya Iraq.

“Meli mbili za kigeni zilizokuwa zimebeba mafuta ya Iraq zilishambuliwa na watu wasiojulikana ndani ya maji ya nchi, jambo lililosababisha moto mkubwa kuzuka,” alisema.
Baadaye alithibitisha kuwa mashambulizi hayo yalifanywa na boti zinazodaiwa kutoka Iran zilizokuwa zimejaa vilipuzi.
Maafisa wa Iraq walichukua hatua za haraka kuwaondoa wafanyakazi kutoka kwenye meli hizo huku vikosi vya uokoaji vikijaribu kudhibiti moto huo usienee zaidi. Jumla ya watu 38 waliokolewa salama kutoka kwenye meli hizo.
Saa chache baadaye, moto mwingine uliripotiwa kuzuka kwenye meli ya mizigo karibu na pwani ya United Arab Emirates baada ya chombo hicho kudaiwa kupigwa na kitu kisichojulikana.

Kufuatia mashambulizi hayo, mamlaka za Iraq zilitangaza kuwa bandari zote za mafuta zimeacha shughuli kwa muda, ingawa bandari nyingine za biashara zitaendelea kufanya kazi kama kawaida.
Wataalamu wa usafiri wa baharini wanasema matumizi ya drones na mashambulizi ya baharini dhidi ya meli za mafuta yanaonyesha tishio jipya kwa usalama wa meli zinazopita katika njia muhimu ya biashara ya kimataifa ya Strait of Hormuz.
Mashambulizi kama hayo yameripotiwa tangu vita kati ya Marekani, Israel na Iran vilipoanza. Mnamo Machi 1, meli ya mafuta ghafi ilishambuliwa karibu na pwani ya Oman baada ya kugongwa na chombo kisicho na rubani cha baharini, tukio lililosababisha mlipuko na moto kwenye chumba cha injini na kuua mfanyakazi mmoja.
Mvutano huo pia umeathiri usafirishaji wa mafuta duniani, huku meli nyingi zikiepuka kupita katika mlango huo muhimu wa bahari kutokana na hofu ya mashambulizi mapya.