Dar es Salaam. Dosari za kisheria katika hati ya kiapo cha rais wa chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), Boniface Mwabukusi, kimesababisha shauri la kikatiba lililofunguliwa dhidi ya Inspekta Jenerali wa Polisi (IGP), kutupwa na mahakama.
Uamuzi wa kutupa shauri hilo baada ya kubainika dosari hizo, umetolewa jana Jumatano, Machi 11, 2026 na jopo la majaji watatu wa Mahakama Kuu, Masjala ndogo ya Dar es Salaam ambao ni Immaculata Banzi, Fahamu Mtulya na Mwanabaraka Mnyukwa.
Kiini cha shauri hilo la Kikatiba namba 29366 la 2025 lililofunguliwa na TLS linahusiana na amri ya IGP ya watu kutotoka nje (curfew) kuanzia siku ya uchaguzi mkuu Oktoba 29, 2025 na siku zilizofuata kulikotokana na vurugu zilizojitokeza.
Katika vurugu hizo na siku zilizofuata, watu ambao idadi yao bado haijawekwa wazi na mamlaka na vyombo vya usalama, waliuawa na wengine kujeruhiwa huku mali za serikali na za watu binafsi yakiwamo majengo na magari yakiharibiwa.
Ni kutokana na yaliyojitokeza siku hizo tano, TLS walifungua shauri hilo la kikatiba wakiomba pamoja na amri nyingine, Mahakama itamke amri hiyo ya IGP iliyotolewa Oktoba 29, 2025 saa 11 jioni ilikiuka Katiba ya Tanzania ya mwaka 1977.
Kulingana na uchambuzi wa jopo hilo la majaji, TLS waliomba mahakama itamke amri hiyo ya IGP haikuwa na uhalali wa kisheria kwa kuwa haiungwi mkono na Katiba wala sheria yoyote, lakini pia inakiuka haki mbalimbali za watu.
Haki hizo ni pamoja na haki ya utu, haki ya kusikilizwa, haki ya mtu kutotendewa vitendo visivyo vya kibinadamu, haki ya kuishi, haki ya mtu kuwa huru kwenda popote, haki ya kuabudu dini yoyote na haki ya kikatiba ya kufanya kazi.
Mbali na maombi ya amri hizo, lakini TLS iliomba mahakama itamke mlalamikiwa wa tatu, Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora Tanzania (THBUB), haikutekeleza wajibu wake wa kikatiba wa kulinda haki za binadamu.
Amri nyingine ambayo TLS iliiomba, ni mahakama kuamuru ni kuundwa kwa Tume Huru ya watu saba ikimjumuisha Jaji mkuu mstaafu na wawakilishi kutoka TLS na kutoka Mahakama ya Afrika ya Haki za Binadamu na Watu (AfCHPR).
Wajumbe wengine watoke Chama cha Madaktari Tanzania na Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa (UN), ili kwa pamoja wafanye uchunguzi huru kuhusu vitendo vilivyofanywa na IGP Oktoba 29 na kutoa ripoti kwa korti.
Hata hivyo, shauri hilo lilikutana na mapingamizi ya kisheria kutoka kwa walalamikiwa ambao ni IGP mlalamikiwa wa kwanza, Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG) mlalamikiwa wa pili, na Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB).
Katika mapingamizi hayo mawili, walalamikiwa walisema mahakama hiyo ilikuwa haina mamlaka ya kutoa amri zinazoombwa na waleta shauri katika aya ya (e) na pia shauri hilo ni baya kisheria kwani kulikuwa na njia nyingine za kupata nafuu.
Mbali na Mahakama kuwataka mawakili wa pande zote mbili kuwasilisha mawasilisho yao juu ya mapingamizi hayo, lakini iliwataka kufanya mawasilisho juu ya uhalali wa kiapo cha mleta maombi kutaja amri ya IGP ilikuwa ni Desemba 29.
Katika usikilizwaji wa mapingamizi hayo, kuliibuka mabishano makali ya kisheria na ya hoja kutoka kwa mawakili wa pande mbili, lakini mwisho wa siku, hoja ya kukosewa tarehe ya amri ya IGP katika kiapo cha wakili Mwabukusi, kiliizamisha kesi hiyo.
Katika uamuzi wao, majaji walisema ni kutokana na amri hizo ambazo walalamikaji waliziomba, mawakili wa pande mbili walikuwa katika ubishani mkubwa wa hoja za kisheria na kama kulikuwa na nafuu kabla ya kutumia njia waliyoitumia.
Majaji hao walisema kulingana na walalamikiwa, walidai mahakama hiyo haikuwa mamlaka sahihi ya kushughulikia shauri hilo na kutoa sababu mbili, moja ni matumizi ya kifungu cha 8(2) cha Sheria ya Haki za Binadamu yaani Bardea.
“Sababu ya pili haiwezi kuchukua muda wa mahakama kwa kuwa ipo wazi. Lakini tatu walalamikiwa walidai ombi lililopo aya ya (e) iliyomo katika wito wa asili (originating summons) inapoka majukumu ya Rais ambaye ndiye mwenye mamlaka ya kuunda Tume kupitia kifungu cha 3(1) cha kuunda Tume
Majaji hao walisema yalikuwa ni maoni ya mlalamikiwa wa tatu ambaye ni THBUB kwamba maombi ya walalamikaji yanakiuka mamlaka ya mahakama, na kubadili nguvu ya mahakama (judicial powers) na kuwa Mamlaka ya Mhimili wa Serikali.
Hata hivyo, walisema wasilisho hilo la THBUB lilipingwa vikali na waleta shauri wakisema ni suala la kisheria zaidi ambapo majaji walisema wanafikiri hoja hiyo iliyoibuliwa ilikuwa ni ya kisheria kwa kuwa kuna nukuu za vifungu vya sheria.
Majaji hao walisema mahakama hiyo haikuwa na mamlaka ya kuunda Tume kama waleta shauri walivyoomba, kwani waombaji hao wanaomba mahakama kuanzisha utaratibu mpya ambao haujulikani na mhimili huo wala Jumuiya ya Madola.
“Ni kwa msingi huo pingamizi la pili lililowekwa na wajibu maombi linakubaliwa na mahakama kwa sababu mahakama hii haina mamlaka ya kuunda Tume ya Uchunguzi kama ilivyoombwa na waleta maombi katika aya (e)”.
Majaji hao walisema wamepitia shauri hilo na kubaini ni mchanganyiko wa maombi, baadhi yanaangukia katika taratibu zilizowekwa na Bardea na zingine zinaangukia katika taratibu zingine zilizowekwa , kama hiyo ya kuunda Tume.
Kuhusiana na hoja iliyoibuliwa na mahakama katika wito wa asili ulioungwa mkono na kiapo cha Rais wa TLS, walisema katika kiapo hicho katika aya ya 9, kinasema amri ya IGP ilitolewa Desemba 29,2025 na sio tena Oktoba 29.
“Kwa heshima zote hatuwezi kusema kile kilichosemwa katika aya hiyo ya 9 ilikuwa ni makosa ya uchapaji kama ambavyo wakili wa waleta shauri walieleza”
Majaji hao walisema japokuwa mawakili wa waleta maombi walisema kuna mfululizo (consistent) katika nyaraka hizo kuwa amri ilitolewa Oktoba 29,2025 lakini hiyo haiwezi kufanya kutajwa kwa tarehe 29 Desemba 2025 kupuuzwe.
Walisema hati hizo za asili za wito ziliandaliwa Novemba 12, 2025 na Rais wa TLS Mwabukusi akasaini hati ya kiapo siku hiyohiyo hivyo inakuwaje katika kiapo hichohicho kuna sehemu anasema amri ya IGP ilitolewa Desemba 29, 2025.
“Kwa kuwa alithibitisha kile alichokiandika katika aya zote kwamba ni za kweli, tunaweza kuhitimisha kwa kusema kuwa kile alichokisema katika aya ya 9 kilikuwa ni sentensi ya uongo na kiapo hakikuandikwa siku hiyo,”walisema.
“Ni msimamo wa sheria kuwa hati ya kiapo ambayo imejaa taarifa zisizo za ukweli ni kama vile hakuna kiapo cha kuzingatiwa katika maombi,”walisisitiza majaji.
Ni kwa msingi huo, majaji hao walisema ni utafiti wao kuwa shauri hilo halina miguu ya kisheria ya kusimama katika mahakama hiyo hivyo linatupiliwa mbali na kwa kuzingatia asili ya shauri hilo, kila upande utabeba gharama zake za kesi.