Tume yapendekeza mabadiliko ya sheria kukomesha matumizi mseto ya ardhi Ngorongoro

Dar es Salaam. Tume ya kutathmini matumizi ya ardhi katika Hifadhi ya Ngorongoro imependekeza Sheria ya Hifadhi ya Ngorongoro ifanyiwe marekebisho ili kuondoa utaratibu wa matumizi mseto ya ardhi.

Hayo yamebainishwa leo Machi 12, 2026 Ikulu ya Chamwino jijini Dodoma na Mwenyekiti wa Tume hiyo, Dk Gerald Ndika wakati akiwasilisha ripoti ya Tume hiyo kwa Rais Samia Suluhu Hassan.

Rais Samia aliunda Tume mbili kwa ajili ya kuchungua sakata la wananchi wanaoishi ndani ya Hifadhi ya Ngorongoro kupinga kuhamishwa kutoka ndani ya hifadhi hiyo na kupelekwa maeneo mengine yaliyotengwa na Serikali ikiwemo Msomera.

Mbali na Tume hiyo ya Dk Ndika, Tume nyingine iliyoundwa na Rais Samia ni ile iliyoangalia uhamaji wa hiari wa wakazi wa Ngorongoro. Tume hiyo iliongozwa na Mussa Iyombe.

Akiwasilisha ripoti ya Tume yake, Dk Ndika amesema Tume inatamani kuona jamii ya wenyeji inawekewa utaratibu wa kuwa na maisha bora kama ilivyo kwa Watanzania wote, hivyo katika maeneo yote matatu yaani Hifadhi ya Ngorongoro, pori la akiba la Pololeti na pori tengefu la Ziwa Natroni yaendelee kuwa na uhifadhi endelevu kutokana na umuhimu wake hasa katika kulinda mfumo wa ikolojia wa Serengeti – Mara.

Pia, amesisitiza kwamba maeneo hayo yaendelee kuwa na uhifadhi endelevu ili kulinda na kuendeleza vivutio vya watalii ili kulinda mapato ya utalii na uendelevu wa bioanuai kwa vizazi vya sasa na vizazi vijavyo.

Dk Ndika amesema baada ya tathmini ya kina na ili kushughulikia changamoto na malalamiko yaliyobainika kwa lengo la kuimarisha uhifadhi, shughuli za utalii na huduma za maendeleo ya jamii, wamependekeza mabadiliko ya sheria.

“Mfumo wa matumizi mseto wa ardhi ndani ya hifadhi ya Ngorongoro siyo endelevu, hivyo tunapendekezwa kuwa: mosi, Sheria ya Hifadhi ya Ngorongoro Sura ya 284, ifanyiwe mapitio na marekebisho kwa kuwashirikisha wadau wote muhimu ili iendane na wakati na mahitaji ya wakati wa sasa. Pili, shughuli zisizo za kiuhifadhi zitekelezwe nje ya hifadhi.

“Tatu, ili kuondoa uvamizi ndani ya Hifadhi ya Ngorongoro, NCAA (Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro) iwatambue na kuwaorodhesha wakazi wote wa ndani ya Hifadhi ya Ngorongoro, makazi yao, mifugo na kuwapa cheti kulingana na matakwa Sheria ya Hifadhi ya Ngorongoro,” amesema.

Dk Ndika ameongeza kuwa uhamaji katika Hifadhi ya Ngorongoro uwe endelevu na uwekeze msingi wa kisheria.

Tume ya Dk Ndika imebaini kwamba idadi ya watu imeongezeka ndani ya Hifadhi ya Ngorongoro kutoka watu 8,000 mwaka 1959 hadi kufikia watu 100,793 mwaka 2022.

Pia, inatarajiwa kwamba idadi ya watu katika eneo hilo inatarajiwa kufikia 272,671 ifikapo mwaka 2050 ikiwa ni ukuaji wa asilimia 3.6. amesema ongezeko hilo linakwenda sambamba na uhitaji wa rasilimali ardhi. Amesema jambo hilo limeongeza ushindani wa ardhi na kupungua kwa malisho ya mifugo na wanyamapori.

“Makazi ya watu, pia, yameongezeka kutoka 13,381 yaliyokuwepo mwaka 2019 hadi 17,784 mwaka 2025 sawa na ongezeko ya asilimia 28.8.

“Ongezeko la mifugo ndani ya hifadhi kutopka mifugo 261,723 mwaka 1960 hadi 715,466 mwaka 2022, ikijumuisha ng’ombe 274,943, mbuzi 201,938, kondoo 226,553 na punda 11,032,” amesema.

Dk Ndika ameongeza kuwa kwa mujibu wa tathmini ya Tume, inakadiriwa kwamba idadi ya ng’ombe pekee itaongezeka kutoka 274,943 hadi kufikia 418,913 ifikapo mwaka 2050, wastani wa ukuaji ukiwa asilimia 2.7 kwa mwaka, hivyo kuongeza mahitaji ya ardhi kwa malisho.

“Mwaka 2022, mifugo ilihitaji eneo la malisho la kilomita za mraba 4,579, sawa na asilimia 56.4 la eneo lote hifadhi la kilomita za mraba 8464.56 sawa na asilimia 104 ya eneo lote la hifadhi ifikapo mwaka 2050,” amesema.

Mwenyekiti huyo wa Tume amebainisha changamoto ya kupungua kwa baadhi ya wanyamapori kutoweka ndani ya hifadhi kama swala twiga pamoja na watu kuuawa au kujeruhiwa ndani ya hifadhi hiyo.

“Watu saba wamekuwa wakiuawa na wanyamapori kuanzia mwaka 2015 hadi mwaka jana, 2025, na kufanya jumla ya watu waliouawa kufikia 77. Pia, watu 274 wamejeruhiwa na mifugo 1,450 imeuawa na wanyamapori katika kipindi hicho,” amesema.