Muundo INEC waendelea kukosolewa na wadau

Dar es Salaam. Ukiwa umepita mwezi mmoja tangu Sheria ya Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi ianze kutumika, baadhi ya wadau wameendelea kuikosoa wakisema haijakidhi malalamiko ya wananchi kuhusu uendeshwaji wa uchaguzi nchini.

Sheria ya Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi Na.2 ya 2024 ni miongoni mwa sheria tatu zilizotiwa saini na Rais Samia Suluhu Hassan, zikiwamo Sheria ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani ya mwaka 2024 na Sheria ya Vyama vya Siasa ya mwaka 2024.

Tangu sheria hizo zilizosainiwa na kuanza kutumika, zimeendelea kukosolewa na wadau vikiwemo vya siasa vikisema hazikuzingatia maoni ya wananchi.

Akizungumza Mei 17, 2024 katika mkutano na waandishi wa habari ulioandaliwa na Baraza la Maaskofu wa Katoliki Tanzania (TEC) Dar es Salaam kuhusu utafiti wa chaguzi barani Afrika, Wakili Gloria Mafole amesema sheria hiyo haijajibu kilio cha wananchi kuhusu uchaguzi.

“Sheria za uchaguzi zilipotolewa lengo lilikuwa ni kujibu malalamiko ya wananchi baada ya uchaguzi wa 2019 na 2020, lakini je, zimejibu malalamiko ya wananchi?” amehoji na kuongeza:

“Ni kweli tumeiita Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, lakini bado tume haiko huru, kwanza watumishi wake watatokana na watumishi wa umma.

“Pili, bado inategemea bajeti yake haiko huru, inatoka kwenye wizara. Hata utoaji wa elimu ya uraia iko shakani kwani ni mpaka wapate bajeti.”

Ameendelea kusema kuwa bado Rais amepewa mamlaka makubwa yakiwamo ya kumteua Mwenyekiti na makamu wa tume hiyo, japo wajumbe wanapita kwenye mchakato wa usaili.

“Bado tunahitaji kufanya marekebisho, tunaamini watakubali marekebisho kama alivyosema rais kwamba anataka mabadiliko, ili kila mwananchi aone umuhimu wa kushiriki uchaguzi,” amesema.

Kwa upande wake Uzima Justine amesema sheria hiyo imeiiga ya  uchaguzi ya nchini Afrika Kusini, lakini kiutendaji ziko tofauti.

“Ile kamati ya usaili ya tume ya Afrika Kusini mwenyekiti wake ni rais wa Mahakama ya Uchaguzi ya nchi hiyo kama Tanzania tumechukua Jaji Mkuu kuwa mwenyekiti wa tume, halafu tumechukua wajumbe kutoka tume nyingine kama Tume ya haki za Binadamu na Utawala Bora.

“Lakini kwa wenzetu, mtu kuwa jaji kwanza anaomba anafanyiwa usaili na hiyo pia ipo hata Kenya. Kwa hiyo ukimleta mtu kama huyo kwenye kamati atazingatia weledi, lakini ukileta mtu aliyeteuliwa kama kwetu hatakuwa huru, atafanya yaleyale yaliyofanyika kwake.

“Tume yetu ina sura ya Afrika Kusini lakini haina moyo wa tume hiyo, Kenya wao wamechukua sura na moyo wa Afrika Kusini,” amesema.

Akifafanua utafiti huo, Uzima amesema barani Afrika kuna aina tatu za tume za uchaguzi ambazo ni inayosimamiwa na Serikali, tume isiyo na uhuru kamili na ya tatu ni tume yenye uhuru kamili.

“Kundi la kwanza la tume ni zile zilizopo katika nchi za Uganda, Zimbabwe, Rwanda, Sudan na Tanzania. Huko wajumbe wanateuliwa na Rais na tume inakiwa chini ya waziri ambaye huunda sekretarieti

“Kundi la pili zina uhuru kwa maeneo fulani, kama ya Malawi, Zambia, Msumbiji na kundi la tatu zipo katika nchi za Kenya, Afrika Kusini, Namibia na  Botswana,” amesema.

Amesema katika mambo waliyopendekeza katika ripoti yao ni uhuru wa tume katika eneo la kupiga kura.  “Pale kuna mawakala wanaoruhusiwa kuingia, waruhusiwe. Wakati fomu zinapotolewa za wagombea, tume wawe na jukumu la kuzikagua na kama iko sawa aruhusiwe na kama haiko sawa airudishe, sio kusubiri mgombea aenguliwe,” amesema.

Hata hivyo, Padre Chrisantus Ndaga amesema hatua Serikali kukubali kusikiliza maoni ya wananchi imeonyesha mwanga.

“Kwa mbali tunaona mwanga. Hata katika Biblia, Yesu aliuliza watu wananiona mimi ni nani? Ndivyo Serikali ilivyotoa nafasi ya kupokea maoni.
“Lakini tumeona mabadiliko bado, tume imebadilishwa jina tu, lakini tume sio huru,” amesema.
 

Related Posts