KUNA uongo na uzushi katika jamii kuhusu wanaume, wanawake na watoto wenye matende na ngiri maji kwamba wamerogwa. Baadhi wanasumbuliwa na imani potofu kuhusu magonjwa hayo.
Fikra za kishirikina: Kuna jamaa mmoja aliambiwa utakapofika maeneo ya pwani kama Tanga, Bagamoyo, Dar es Salaam, Zanzibar, Pemba, Mtwara na sehemu kama Kilwa usinywe maji ya madafu na usile mafenesi utauguwa ngiri maji (busha) na utapata ugonjwa wa matende.
Fikra za kizinifu: Mwingine alipewa tahadhari nzuri na yenye maadili, kuwa akitembea na mke wa mtu, atapata ngiri maji. Watu wengine wanafikiri kuwa mwanamume akijamiiana na mama aliyeko kwenye hedhi (siku za damu zake za mwezi) atapata ngiri maji.
Kama kuna kitu kinachoweza kumpa mtu elimu ya kujuwa chimbuko la matende na ngiri maji linatokana na nini basi soma makala hii ya kisayansi ujue tiba na chimbuko la ngiri maji (mabusha) na matende. Kwa kifupi hakuna uchawi wala mazigahombwe yanayosababisha maradhi kama hayo katika jamii ya Watanzania na wengine walioko sehemu nyingine zenye joto, ambazo wengine huziita nchi za tropiki.
Chimbuko
Ugonjwa huu wa matende na ngiri maji kwa taaluma ya kitabibu/ kidaktari/ kisayansi huitwa “Lymphatic filariosis” ambao husababishwa na minyoo ambayo huwapata takriban watu zaidi ya milioni 90 ulimwenguni pote.
Minyoo hiyo, ambayo husababisha visa hivyo zaidi ya milioni 90 huitwa “Wuchereria bancrofti” na maambukizi yapo zaidi katika nchi za kiafrika zenye joto (nchi za tropiki), bara la Asia, nchi za Pacific, Amerika Kusini na nchi za Caribean kama Jamaica. Kuna aina ya minyoo ya matende katika bara la Asia huitwa “Brugia malayi” lakini hapa kwetu hatuna.
Minyoo ya kike huzalisha viluwiluwi vya awali ambavyo vinakuwa na utando ambavyo hujulikana kama viluwiluwi vidogo (microfilariae) ambavyo huenda kwenye damu na vina hulka ya kupatikana wakati wa usiku kwenye sehemu za damu zilizoko pembezoni kwenye mwili wa binadamu, kwenye vidole vya miguu na mikono.
Viluwiluwi hivi vidogo vinapofyonzwa kwenye damu, wakati wa usiku na mbu jike aina ya Culex na hata mbu hawa wanaoleta malaria Anopheles hapo sasa hubadilika katika hatua ambayo uwezekano upo wa mtu mwingine kung’atwa na mbu mahsusi ambaye atamsambazia vimelea hivyo na kuuguwa ugonjwa huo.
Madhila ya awali ya ugonjwa huu ni mtu kupata uvimbe na maumivu kwenye njia za mitoki mara kwa mara na kuvimba mitoki kwenye sehemu za chini/ kinenani. Mitoki, njia zake zinapoziba uvimbe mkubwa hujitokeza kwenye miguu, mikono, matiti kwa akina mama na kwenye hasua/ korodani.
Wanaume na wanawake wanaweza kupata uvimbe kwenye mashavu ya sehemu zao za ukeni (labia majora), akavimba mithili ya ngiri maji, kama mwanaume endapo uvimbe utaendelea. Ishara ya kuanza kwa nyonde nyonde hiyo ya kuvimba mitoki hujitokeza baada ya miezi 8 katika maambukizi ya awali yaliyosababishwa na mbu.
Mtu aliyeathirika atakuwa na homa za mara kwa mara, kichefuchefu, kuumwa kichwa kama vile mgonjwa wa malaria na huenda akapata harara (aina fulani ya kuwa na vipele kama vya joto) kwa majuma mawili.
Homa hii ya minyoo ya ugonjwa wa matende na ngiri maji inaweza kuendelea kwa muda mrefu hata zaidi ya miaka mitano na kuendelea endapo mhusika hata pata tiba stahili. Homa hizo za vipindi huenda zikaambatana na uvimbe kwenye njia za mitoki, korodani, matiti kwa mama na mashavu ya mama kule ukeni yakawa yanachonyota, na wakati mwingine muwasho mkubwa hutokea kwenye matiti. Baadhi ya watu walioathirika wakiwa watoto wanaweza wasioneshe dalili zozote zile.
Ugonjwa wa matende na ngiri maji katika jamii zote zile, iwe Tanzania au nje ya Tanzania, maambukizi hupita mkondo huo; hakuna uchawi wala kurogwa, hakuna madafu yaletayo matende, wala ulaji wa mafenesi, wala kujamiiana na mama akiwa katika siku zake. Lakini inashauriwa kwa wale waumini wa dini ya Kiislamu ni haramu kumuingilia mkeo akiwa katika siku zake.
Ugonjwa wa matende na ngiri maji upo katika mpango mkakati wa kitaifa wa kuutokomeza ugonjwa huo kwa kutoa dawa aina ya Ivermectin na Albendazole. Dawa hizo mbili hutolewa kwa kipimo maalum katika maeneo mengi niliyoyataja hapo juu.
Wananchi wasiogope kutumia dawa hizo ambazo ni salama. Baadhi ya watu waliozitumia wamerejesha nguvu zao za kiume zilizokuwa zimedorora. Baadhi ya akina mama wameshika mimba na kuzaa salama. Wanaume wengine wamefanyiwa upasuaji wa ngiri maji bila malipo katika maeneo husika.
Udhibiti wa malaria katika maeneo husika programu zao zikienda sambamba katika utumiaji wa vyandarua vilivyowekewa dawa husaidia kutokomeza minyoo ya ngiri maji na matende. Magonjwa kama hayo huitwa magonjwa yaliyosahaulika.
Sasa hufanyiwa mikakati maalum pamoja na ugonjwa wa usubi (Onchocerciasis), minyoo ya tumbo, kichocho, trakoma pamoja na malale (Sleeping sickness), kichaa cha mbwa na magonjwa mengneyo.
Mpango huo wa dawa huitwa Dawa za Kinga kwa wote “Mass Drug Administration” ambazo hutolewa na Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii kwa utaratibu uliowekwa kwa kushirikiana na wadau mbalimbali na jamii kuhusishwa, kushirikikishwa ili kufanikisha zoezi hilo.
Tukutane wiki ijayo panapo majaaliwa kwenye ulingo wetu wa uongo na uzushi katika tiba. Okoa uhai wako okoa maisha yako, pata taarifa na habari sahihi kutoka kwa watu sahihi.
Dk. Ali Mzige ni mtaalamu wa afya ya jamii na aliwahi kuwa Mkurugenzi wa Kinga, Wizara ya Afya kabla hajastaafu mwaka 2005. Sasa ni mkurugenzi wa Mshangai Polyclinic Korogwe. amzigetz@yahoo.com. 0754495998.