Tanga. Baadhi ya wavuvi wa samaki wanaofanya shughuli zao katika mwalo wa Deep Sea jijini Tanga, wameshindwa kuendelea na kazi ya uvuvi kwa saa 17 hadi muda kutokana na hali ya hewa kuchafuka baharini.
Mpaka muda huu, upepo mkali unavuma ukiambatana na mawimbi makubwa.
Wakizungumza na Mwananchi Digital leo Jumatano Mei 22, 2024 katika ufukwe wa bahari hiyo, wavuvi hao akiwamo Hamad Hamis amesema hawawezi uingiza vyombo baharini wakihofia madhara kwao na vyombo vyao.
“Wapo wenzetu wengine waliingia baharini jana mapema lakini hali ilipobadirika wamelazimika kurejesha vyombo pwani, hasa wale wenye vyombo vidogo kwa upepo huu ni rahisi kupata madhara,” amesema Hamis.
Amesema pia anga limetawaliwa na wingu kubwa linalokuja na kuondoka, hawajui kama mvua itanyesha ama laa.
“Lakini upepo na mawimbi baharini hii ni dalili ya mchafuko wa hali ya hewa, nawashauri wavuvi wenzangu wasiingize vyombo vya kuvulia baharini, lolote linaweza kutokea,” amesema Hamis ambaye pia ni nahodha wa chombo cha uvuvi.
Hata hivyo, anasema wamechukua tahadhari mapema kwa sababu tayari Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) ilishatabiri uwepo wa kimbunga Laly kinachosababisha mvua na upepo mkali kwa baadhi ya maeneo nchini, hasa pwani ya Bahari ya Hindi.
“Kama utakumbuka tangu kimbunga Hidaya bado hali haijakuwa sawa pwani ya bahari ya Hindi hasa maeneo tunayokwenda kuvua samaki, na tangu TMA itabiri uwepo wa kimbunga Laly, hali imeendelea kubadilika kila mara, hivyo kama unaingia kwenye maji lazima uwe na chombo (Jahazi au boti ya uvuvi) kikubwa na chenye uwezo,” amesema Hamis.
Ofisa Uvuvi wa Soko la Samaki Deep Sea jijini hapa, Neema John amesema baadhi ya wavuvi wamerudi kutoka baharini, wakieleza kuwa hali ya hewa si nzuri.
“Tuliwaambia mapema wachukue tahadhari na tunaendelea kutoa elimu kwa wavuvi kuhusiana na kuchukua tahadhari, wakiona dalili si nzuri wasiingie baharini,” amesema John.
Mwenyekiti wa mazingira wa mwalo wa Deep Sea, Hamisi Saidi ameonya wavuvi kutopuuza utabiri uliotolewa huku akisema hali ya hewa si rafiki kwa wale wanaofanya kazi za uvuvi.