Wanawake jamii za wafugaji wanavyokabili mabadiliko ya tabianchi

Arusha/Manyara. Wanawake katika jamii za wafugaji, hususan Wamasai, hawahusishwi sana katika shughuli za uchumi za kujipatia kipato au kusaidia familia zao katika mahitaji ya kila siku.

Hata hivyo, wapo waliojikomboa katika hili na kuamua kuchakarika kutokana na uhalisia wa hali ya maisha, hasa ukame ulioathiri shughuli za ufugaji.

“Siku hizi ng’ombe siyo wengi na hawatoi maziwa mengi. Zamani ng’ombe wawili waliweza kulisha familia ya watu 10. Sasa hivi hawatoi maziwa hata ya watu wawili,” anasema Nalepo Saning’o.

Anaeleza kwa sasa hawategemei sana mifugo kwani hakuna malisho au yamepungua sana.

Wanawake katika kijiji cha Losirwa kata ya Esilalei wilaya ya Monduli wakiwa kwenye shamba la majani walilopanda wenyewe baada ya kupata elimu kutoka shirika la Baraza za Wanawake wa jamii za Kifugaji (PWC). Picha |Ombeni Danieli

Nalepo ni miongoni mwa wanawake 19 niliowakuta wamekusanyika kwenye mkutano wa pamoja katika Kijiji cha Oloswaki, wilayani Simanjiro. Wanawake hawa wanasema wanatoka Kijiji vya Terrat, Kitongoji cha Ololulung’a, Kijiji cha Engonongoi na baadhi kutoka Oloswaki.

“Huu ni mkutano wa kikundi chetu cha Kikoba, tunafanya hivi angalau mara moja kwa wiki,” anasema Nairukoki Tauta, kiongozi wa kikundi hicho.

Nairukoki anaeleza kutokana na hali ngumu ya maisha inayotokana na ukame unaoathiri ufugaji na kilimo, waliona umuhimu wa kuungana.

“Awali tulikuwa tunakaa nyumbani, tukitegemea tu waume zetu. Lakini hali ilivyozidi kuwa ngumu, tuliona haja ya kuchangia ustawi wa familia zetu. Hivyo, tuliungana na kuanzisha kikundi hiki cha Kikoba,” anasema.

“Tulianza kwa kila mmoja kuchangia Sh2,000 kwa wiki, kisha tunampa mtu mmoja, hivyo kila mtu alipata wastani wa Sh30,000. Tunatumia fedha hizi kufanya biashara ndogondogo kama kuuza sukari, vifaa vya shule, vitafunwa na zingine,” anasema.

Anaeleza biashara zao ziliathiriwa mwanzoni na mtaji mdogo, lakini baadaye uliongezeka baada ya kupata mkopo wa Sh1 milioni kutoka shirika lisilo la kiserikali la Mpango wa Uhifadhi na Uwezeshaji Jamii Tanzania (TACCEI) lililoko Terrat wilayani Simanjiro.

Mfano wa mbegu za majani zilizovunwa na wanawake kutoka kijiji cha Losirwa kata ya Esilalei wilaya ya Monduli mbegu hizo huvunwa na kuuzwa kwa vikundi vingine vya wafugaji kwa ajili ya kupanda majani . Picha |Ombeni Danieli

Anasema baada ya kuongeza mtaji, waliweza kukopeshana zaidi ya Sh100,000 kwa masharti nafuu.

Esupati Tajiri, mmoja wa wanakikundi hicho anasema anatumia fedha hizo kufanya biashara ya sukari na sabuni.

“Nilianza na kilo 10 za sukari na kilo tano za sabuni. Nauza kwa majirani zangu na maeneo ya kijijini kwetu, naweza kulipa mkopo,” anasema.

Mwanachama mwingine, Naitapuaki Lukas, mama wa watoto watano anasema: “Sasa naweza kununua madaftari na sare za shule kwa watoto wangu. Biashara ya sabuni na sukari imenisaidia sana.”

Kwenye Kijiji cha Oloswaki, wilayani Simanjiro, licha ya kukumbwa na ukame wa wastani unaoashiria ukosefu wa mvua, nyumba moja ilizungukwa na kijani kibichi cha majani na miti mbalimbali.

Hii ni nyumba ya Vaileth Kadogo. Kuna bustani ya takribani robo ekari iliyolimwa viazi, mboga mbalimbali, mihogo, na migomba iliyostawi.

Katika eneo hilo pia kulikuwa na matuta yaliyoashiria miche itapandwa hivi karibuni.

“Matuta haya yalikuwa ya mboga za majani, lakini sasa nataka kujiandaa kwa viazi,” anasema Vaileth mama wa watoto watano.

Anasema wanatumia matuta kupanda kwa sababu ya kuhifadhi maji.

“Tunachimba shimo la urefu wa futi mbili tunaweka majani, samadi na udongo kwa tabaka tofauti,” anasema.

Vaileth anasema bustani hiyo inasaidia familia yake kwani wakati wa ukame wanauza mboga na wanatumia baadhi nyumbani.

“Elimu tuliyopewa na wadau, hususan TACCEI kuhusu kutumia eneo dogo na maji machache, imekuwa na mafanikio. Nauza mboga na kupata kati ya Sh2,000 hadi Sh5,000 kwa siku. Nanunua madaftari kwa ajili ya watoto na pia namsaidia mume wangu,” anasema.

Mkurugenzi wa TACCEI, Justin Lukumay anasema:

“Tulilazimika kufikiria njia za kuwasaidia wanajamii wenzetu kwa sababu huku ndiko kwetu na sote tumekumbwa na mabadiliko ya tabianchi.”

Anasema waliwapatia wanawake hao elimu na msaada kwa sababu mara nyingi kundi hilo limeachwa nyuma.

Mwenyekiti wa Kijiji cha Terrat, Kone Medukenya anasema wanawake wanaathirika zaidi na ni rahisi kwa mwanamume kuacha familia kuliko mwanamke kufanya hivyo.

Anasema kuanzishwa kwa vikundi vya kukopeshana kumeonyesha umuhimu mkubwa kwa kundi hilo katika jamii.

Ofisa Mtendaji wa Kijiji cha Oloswaki, Lairorie Ormemei anasema:

“Tunashirikiana na taasisi zinazosaidia na kuunga mkono juhudi zetu kwa sababu kama serikali ya kijiji, tuna mipango ya kupanda angalau miti mitano kwa kila kaya kila mwaka. Elimu ya uhifadhi wa mazingira inapaswa kuendelea kwa sababu jamii zetu zimechelewa sana na zinaathiriwa.”

Hali si tofauti sana kwa wanawake katika Wilaya ya Monduli.

Katika Kijiji cha Losirwa, Kata ya Esilalei, nilikutana na kundi la wanawake kutoka jamii ya ufugaji wanaojishughulisha na mradi wa kilimo cha majani.

“Tulianza mradi huu mwishoni mwa mwaka jana baada ya kijiji kutupatia eneo,” anasema Grace Narumuta kiongozi wa kikundi cha watu 30 (wanawake 25 na wanaume watano).

Katika eneo la wazi lenye miti kadhaa ambalo upeo wa macho unaishia kuna sehemu ya tofauti iliyozungushiwa uzio wa miiba.

Hapa ndipo bustani ya ekari 14 ilipo. Majani ndani ya eneo la uzio ni marefu, yakifikia urefu wa magoti au zaidi ikilinganishwa na nje ya uzio.

Grace anasema bado wanatunza eneo hilo ambalo wataanza kuuza majani wakati wa kiangazi.

Wamekusanya mbegu kwa baadhi ya majani yaliyokomaa na kuuza.

“Tulivuna zaidi ya kilo nne za mbegu na kuuza kwa vikundi vingine kila kilo kwa Sh25,000 kwenye Siku ya Wanawake Duniani (Machi 8). Biashara hii imetuonyesha mwanga,” anasema.

Grace anasema mbali na mradi wa majani, kundi lao lina mradi wa Kikoba na hufanya biashara ndogondogo.

“Katika vikundi hivi tunasaidiana, mfano mwanakikundi ana mwanafunzi anahitaji fedha za shule, tunaweza kumpa msaada na asirudishe kwa sababu tuna mfuko wa jamii unaounga mkono baadhi ya mambo ya dharura,” anasema.

Katika baadhi ya nyumba za Esilalei, kuna uvunaji wa maji ya mvua, matangi kadhaa ya maji yamewekwa.

Dora Kilimbe anasema, “Tulikuwa tunapata shida wakati wa kiangazi, lakini tulipata elimu juu ya uvunaji wa maji ya mvua, na kwa matangi tuliyonayo, tunaweza kuhifadhi maji yanayoweza kudumu hadi miezi mitano kwa familia zetu na baadhi ya majirani.”

Wanawake hao walipata elimu juu ya uhifadhi wa maji, vikoba, na uvunaji wa maji ya mvua kutoka shirika la Baraza la Wanawake Jamii za Wafugaji (PWC).

Stella James, Meneja wa Miradi ya PWC, Wilaya ya Monduli anasema:

“Tulitafuta wataalamu kutoa elimu kwa vikundi hivi, lakini nasi pia tunachangia kuwapa elimu….”

Anasema kuna vikundi vinne vya kupanda majani wilayani humo, na zaidi ya ekari 44 zimepandwa na kuhifadhiwa.

Pia kuna vikundi 12 vyenye wanachama 30 kila kimoja wanaojishughulisha na shughuli za kuweka na kukopesha.

Mwenyekiti wa Kijiji cha Loswira, Yamat Laizer anasema:

“Kijiji kinaendelea kuunga mkono juhudi hizi, ndiyo maana tulitoa maeneo ya wazi kwa vikundi kulima majani. Bado kuna maeneo, tutaendelea kuyatoa kwa wengine ili kuhakikisha eneo letu linabaki salama.”

Katibu Tawala Mkoa wa Arusha (RAS), Missaile Musa anasema baada ya serikali kurejesha mgawo wa mkopo wa asilimia 10 kwa makundi maalumu, ambao utaanza mwaka ujao wa fedha, kila halmashauri imeunda mpango wa kuhamasisha vikundi hivyo kukopa.

“Kwa kushirikiana na idara za maendeleo, baraza za kata na madiwani katika kila halmashauri, tayari tumeanza kampeni ya uhamasishaji,” anasema.

Anasema lengo la kampeni ni kuwaandaa ili watakaopata fedha waweze kuziwekeza kwa ufanisi na manufaa yao.

Mkuu wa Wilaya ya Simanjiro, Faki Lulandala, anasema shughuli nyingi za kiuchumi, zaidi ya ufugaji zinafanyika zikiwamo uchimbaji madini, biashara, na uvuvi.

Anasema wameanza kuwaandaa wananchi, hususan wanawake, kuhusu vigezo vya kupata mikopo ya halmashauri na shughuli watakazozifanya.

“Tunasubiri mwaka wa fedha, na kwa sasa, kuna wale ambao tayari wameanza kuomba,” anasema.

Imeandaliwa kwa ufadhili wa Bill & Melinda Gates Foundation.

Related Posts