Kilio cha barabara na maji chamgusa Dk Tulia

Mbeya. Diwani wa Kata ya Ilemi jijini Mbeya, Angelo Magoma amempokea Spika wa Bunge, Dk Tulia Akson kwa kilio cha barabara na maji akieleza kuwa wananchi wana manung’uniko mengi na wanatishia kuandamana kutokana na changamoto hiyo.

Magoma amesema hayo leo Juni 1 wakati Dk Tulia alipofika kata hiyo kusalimiana na wananchi na kukutana kero hiyo, akieleza kuwa kilio hicho kimekuwa cha muda mrefu na wananchi wanatishia kuandamana.

“Na hapa ni kwakuwa imekuwa dharura ila wananchi wangekuja kwa wingi lakini manung’uniko kuhusu huduma ya maji na barabara hadi wanatishia kuandamana ” amesema Magoma.

Akizungumzia kero hizo, Dk Tulia amesema Serikali ipo makini kufikisha huduma zote za jamii ikiwamo kituo cha afya Ilemi na kwamba barabara itajengwa yenye kilomita 3.8.

Mbunge huyo ameitaka kampuni inayosimamia barabara ya Maperere – Machinjioni  katika kata hiyo, kukamilisha mradi huo kwa wakati akieleza Juni 28 baada ya Bunge kuisha vikao vyake atarejea kuangalia hatua iliyofikiwa.

“Watu wa maji wataanza kuja leo na kuanzia wiki ijayo huduma itaanza kutoka katika maeneo ambayo hayatoki, japokuwa kipindi cha kiangazi huwa maji yanakuwa tatizo na kusababisha mgawo”

“Hii miradi iko chini ya Tactic, inasimamiwa na kampuni moja ya CICO sasa natarajia kumaliza bunge Juni 28, nitarudi hapa kujua mmefika wapi, Kama hamuwezi kumaliza kwa wakati tafuteni wa kusaidiana naye kazi iishe ndani ya muda” amesema.

Wakati huohuo, Dk Tulia amefungua wiki ya mazingira ambayo imefanyika jijini hapa kwa Kanda ya Nyanda za Juu, akiwataka vijana kuchangamkia fursa ya mazingira kujikwamua kiuchumi na kutengeneza ajira.

Dk Tulia amesema Serikali inatoa mikopo kwa makundi matatu ya vijana, wanawake na wenye ulemavu, hivyo kupitia kampeni ya mazingira inaweza kuwa fursa kiuchumi na ajira.

Mbunge huyo wa Mbeya mjini, ametumia fursa hiyo kutoa pongezi kwa Serikali mkoani Mbeya kufanikisha jiji hilo kuwa la pili kwa usafi kitaifa kati ya majiji sita nchini.

Related Posts