Unguja. Wakati ndugu wa mfanyakazi wa Hospitali ya Rufaa Mnazi Mmoja, Said Ali Shineni (49) wakiwatuhumu walinzi wa hospitali hiyo kutoka Jeshi la Kujenga Uchumi (JKU) kumuua mtumishi huyo, Polisi na uongozi wa hospitali wamesema wanachunguza tukio hilo.
Akizungumza na Mwananchi jana Jumanne Juni 4, 2024 ndugu wa marehemu huyo, Adil Suleiman Sheha amesema taarifa ya kifo walizipata siku hiyo na walipoenda eneo la tukio walibaini aliyefariki dunia ni ndugu yao.
Adil amesema taarifa walizonazo ni kwamba askari watano wanashikiliwa katika Kituo cha Polisi cha Malindi kutoka na tukio hilo.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mjini Magharibi, Richard Mchomvu licha ya kukiri kufahamu tukio hilo, hakuthibitisha waliohusika ni kina nani akisema bado wanachunguza.
“Taarifa hiyo bado hatuna uhakika nayo, tunaifuatilia,” amesema Kamanda Mchomvu.
Mkurugenzi Mtendaji wa hospitali hiyo, Dk Muhidin Abdi Mahmoud amekiri kupokea taarifa ya kifo cha mfanyakazi huyo.
“Mfanyakazi huyo inasadikiwa kauawa akiwa katika mikono ya askari wa JKU ambaye amefikishwa kwa Jeshi la Polisi,” amesema Dk Muhidin.
Amesema mwili umehifadhiwa hospitalini hapo kwa ajili ya uchunguzi ili kubaini kifo hicho kimetokana na shambulio au cha kawaida.
“Taarifa ya kifo hicho itatolewa baada ya kupatikana ripoti kamili ya chanzo cha kifo hicho kupitia mamlaka husika,” amesema Dk Muhidin.
Ametoa pole kwa wafiwa na kuwataka kuwa na subira katika kipindi hichi kigumu kwa ndugu na wafanyakazi wa hospitali hiyo.
Adil anadai askari wa JKU waliokuwapo lindo walimfunga ndugu yao kwenye mnazi na kumpiga wakidai alitaka kumpora mtu mkoba hospitali hapo.
Amedai hawajapatiwa mwili wa ndugu yao wameambiwa watapatiwa ripoti ndani ya saa 72 ndipo waende kuuzika.
Adil ameiomba Serikali kulishughulikia suala hilo akisema vikosi vya SMZ vinaonekana kuwa tishio kwa kuwapa maumivu wananchi na siyo tena kimbilio la wanyonge.
“Kuendelea kwa vitendo hivi ni kutokana na kuwa kesi za aina hii zinamalizika kienyeji na wala hazifikishwi katika sehemu husika ili kuwa funzo kwa wengine,” amedai Adil.
Amesema ndugu yao amefanya kazi katika hospitali hiyo kwa miaka 20 na hawakuwahi kupata sifa mbaya kutoka kwake.
“Jambo hili linasikitisha sana kwa sababu huyu ni mfanyakazi wa Serikali na jambo hili limetokea ndani ya mikono ya Serikali lazima hatua stahiki zichukuliwe,” amesema.
Amesema hata kama ndugu yao katenda kosa hakuna sheria inayosema mhalifu auawe badala yake apelekwe katika vyombo vya sheria.
Dada wa marehemu, Raifa Ali Shineni amesema ameacha mke na watoto watatu wadogo.
Amesema taarifa za awali walizopatiwa zilikuwa zikisema kuwa ndugu yao kaanguka na kufariki dunia ila baada ya kufika hospitali ndipo walipotambua kuwa hakuanguka bali alipigwa.
“Walisema alipigwa kwa sababu alitaka kuiba mkoba hatukatai ila zipo sheria wangezifuata na siyo kujichukulia sheria mkononi,” amesema.