Geita. Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Doto Biteko amewataka askari wa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) kutambua uhai wa mtu ni wa thamani na kazi yao ni kuwakamata na kuwafikisha kwenye vyombo vya sheria wale wanaoingia msituni bila kibali, na sio kuwapiga, kuwasababisha ulemavu au kifo.
Pia amekemea tabia ya wananchi wanaoingia msituni wakiwa na silaha kama panga na mishale na kuwashambulia askari wanaolinda misitu, kuacha mara moja kwa kuwa askari hao wapo kwenye maeneo hayo kwa mujibu wa sheria na taratibu.
Dk Biteko ambaye pia ni Mbunge wa Bukombe ameyasema hayo jana Juni 6, 2024 wakati akizungumza na wananchi wa Kata ya Igulwa wilayani Bukombe, ambapo alimtaka Kamishna wa Uhifadhi wa TFS, Profesa Dos Santos Silayo kuwasimamia askari wake watambue uhai wa Mtanzania ni wa thamani na kuwa hawawezi kuua watu kirahisi.
“Kuna watu wameuawa, waambie watu wako uhai wa Mtanzania una thamani kubwa. Hawawezi kuua watu tena kirahisi, kazi yao kubwa pamoja na mambo mengine, ni kuwakamata hao watu na kuwapeleka kwenye vyombo vya dola. Acha watu wabaki na uhai wao wakashughulike mahakamani,” amesema Biteko.
“Na nyie wananchi, askari wetu wa TFS nao ni watu, mmekutana porini mna panga yeye ana bunduki, mnataka afanye nini kujihami, nawasihi msichokozane mnaoenda porini kwa mchongo, kuweni na subira na lazima tuilinde misitu,” amesema Biteko.
Akizungumzia Pori la Kigosi Moyowosi ambalo wananchi wa Bukombe wanaomba kuachiwa ili wafanye shughuli za kibinadamu ikiwemo ufugaji nyuki, amewataka kuwa na subira na kutoingia kinyemela wakati huu ambao Serikali inashughulikia maombi yao.
Biteko amesema pori la Kigosi Moyowosi lenye ukubwa wa kilomita za mraba 13,000 linalopakana na mikoa ya Shinyanga, Kigoma, Tabora na Geita lilikuwa hifadhi ya wanyamapori na badaye likapandishwa hadhi kuwa Hifadhi ya Taifa.
Kupandishwa hadhi kwa pori hilo kulisababisha wananchi waliokuwa wakitegemea kufuga nyuki kwenye eneo hilo kushindwa kuendelea na kazi hiyo na kusababisha malalamiko, jambo lililomfanya akamombe hifadhi hiyo irudi kuwa pori la akiba, ili maisha ya watu yaendelee.
Amesema kutokana na biashara ya asali Bukombe kuwa kubwa, pori hilo liliondolewa kwenye Hifadhi ya Taifa na kushushwa Hifadhi ya Msitu na kwamba tayari amemwelekeza Waziri wa Maliasili na Waziri wa Madini kwenda Bukombe kuwaeleza wananchi utaratibu unaofuta.
Amesema Serikali inatambua umuhimu wa watu kupata sehemu ya kufanyia shughuli na itakuja na utaratibu mzuri wa kuhakikisha pori hilo linaleta manufaa kwa watu.
Amewataka wafuga nyuki kuchukua vibali kwa utaratibu wa kawaida na kuendelea na shughuli zao huku wenye nia nyingine wakitakiwa kusubiri.
Wakizungumzia maagizo hayo baadhi ya wananchi wa Bukombe wamesema kwenye msitu huo mbali na kutegemea kufuga nyuki, pia eneo hilo lina madini na endapo watapewa kibali itasaidia wananchi kujipatia kipato na kuinua uchumi.
Shukrani Elias amesema kufunguliwa kwa pori hilo kutatoa ajira kwa wananchi hususan wachimbaji wadogo na kuiomba Serikali kuharakisha mchakato huo ili wananchi waweze kunufaika.
Aidha Mgogoro wa askari wa TFS na wananchi umekuwa ukisababisha madhara ambapo kwa mwaka 2022 askari sita wa TFS nchini walipoteza maisha katika mapambano dhidi ya raia.
Januari 6, 2024 askari wanne wa TFS wilayani Geita walikamatwa na Jeshi la Polisi mkoani Geita wakituhumiwa kumuua mwananchi kwa kumpiga risasi wakati akiokota kuni bila kibali katika msitu wa Samina uliopo wilayani Geita.