Mshambuliaji wa Taifa Stars, Saimon Msuva amesema wachezaji wapo tayari kwa ajili ya kupambana ili kupata matokeo yatakayowaweka kwenye nafasi nzuri kufuzu kushiriki Kombe la Dunia.
Stars wataanza ugenini dhidi ya Zambia mchezo unaotarajiwa kuchezwa Juni 11 mwaka huu na wanaendelea kujiweka fiti tayari kwa mchezo huo.
Akizungumzia muda mchache kabla ya kuanza mazoezi alisema kwenye kundi lao timu watakazokutana nazo nyingi ni zile zile walizokutana nazo Afcon wanaamini kutokana na kikosi kilichopo ambacho kimejaa vijana wengi watafanya vizuri.
“Sio mashindano mepesi kwa sababu kila timu inahitaji hiyo nafasi hivyo sisi kama wachezaji tunajiandaa kwenda kushindana nina imani kubwa sisi wazoefu tukiungana na wachezaji wapya waliojumuika nasi tutafanya vizuri,” amesema na kuongeza;
“Damu changa zilizopo kwa asilimia kubwa wana hali na wana uchu wa mafanikio kama wakipewa nafasi ya kucheza watatupa matokeo mazuri,” amesema.
Msuva amesema wanatarajia mchezo mzuri na wa ushindani kutoka kwa wapinzani wao lakini wamejiandaa vyema kwenda kupata matokeo ugenini.