Singida Black Stars imemtambulisha kocha wa zamani wa Simba Patrick Aussems kuwa kocha wao mpya.
Taarifa iliyotolewa muda mfupi uliopita kutoka Ofisi ya Afisa Mtendaji Mkuu wa timu hiyo Jonathan Kasano,imesema Aussems atakuwa kocha mkuu wa timu hiyo kuanzia msimu ujao.
Aussems, ataanza kazi rasmi Julai Mosi ambapo Sasa ataendelea na majukumu ya kukijenga kikosi hicho kwenye eneo la usajili, akishirikiana na uongozi wa klabu hiyo.
Aussems raia wa Ubelgiji ataanza kazi na klabu hiyo ikiwa na jina jipya ikitoka kubadilishwa kutoka iliyokuwa Ihefu ya Mbarali kabla ya kuhamishiwa Singida.
Hata hivyo, taarifa hiyo haijaonyesha kocha huyo atakuwa na wasaidizi gani na hatma ya aliyekuwa kocha wao msimu uliopita Mecky Maxime.
Aussems ana leseni ya UEFA PRO na uzoefu wa kufundisha klabu kubwa barani Africa, Ulaya na Asia, zikiwemo timu za Al Hilal Omdurman (Sudan), Simba SC (Tanzania), AFC Leaopards (Kenya), Shenzhen Ruby (China), ETG (Evian Thonon Gaillard) FC & Angers SCO FC ya Ufaransa.
Pia amefundisha timu za taifa zikiwemo za Nepal na Benin. Kocha Aussems amewahi pia kuwa Mkurugenzi wa Ufundi wa Marbella FC ya Hispania.
Singida inakuwa klabu ya pili kwa Tanzania kumpa ajira Aussems ambaye kabla ya hapo aliifundisha Simba kwa mafanikio ikibeba ubingwa wa Ligi Kuu Bara mara mbili na kufikisha hatua ya Robo Fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika.