IMEELEZWA kuwa lengo la serikali kuwafikishia maji safi na salama asilimia 85 ya wananchi waishio vijijiji na asilimia 95 ya wananchi waishio mjini ifikapo mwaka 2025, linakaribia kutimia wilayani Kilombero mkoani Morogoro baada ya asilimia 77 ya wananchi wa wilaya hiyo kufikishiwa huduma hiyo. Anaripoti Victor Makinda, Morogoro … (endelea).
Hayo yamebainishwa na Meneja wa Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) wilaya ya Kilombero, Mhandisi Florence Mlelwa katika wa mkutano wa wadau wa maji uliofanyika mjini Ifakara wilayani Kilombero jana Ijumaa.
Akitoa taarifa ya utekelezaji wa miradi ya maji wilayani humo mbele ya madiwani, watendaji wa kata wadau wengine wa maji, Mlelwa amesema kwa mujibu wa Sensa ya watu na makazi ya mwaka 2022 Wilaya Kilombero inakadiriwa kuwa na watu 582,960, ikiwa watu 199,641 wapo katika eneo la Ifakara Mji ambao wanahudumiwa na Mamlaka ya Maji na Usafi wa Mazingira (IFAUWASA) huku RUWASA ikiwahudumia watu 383,319 waishio vijijini.
Amesema kati yao watu 297,838 sawa na asilimia 77.7 wanapata huduma ya maji safi na salama.
Akieleza mipango zaidi ya kusamabaza huduma ya safi na salama maji wilayani humo Mlelwa amesema kuwa RUWASA wilayani Kilombero imepanga kutumia jumla ya Sh 4.8 bilioni kutekeleza miradi ya maji katika mwaka mpya wa fedha unaotarajiwa kuanza Julai Mosi 2024-2025.
“RUWASA katika mwaka ujao wa fedha tunatarajia kutekeleza miradi 6 ya maji sambamba na kukamilisha ujenzi wa miradi ya maji ya Mbingu- Igima, na Mherule,’ amesema.
Ameitaja miradi mipya inayotarajiwa kutekelezwa na RUWASA kuwa ni mradi wa Mofu – Ihanga, Lugala, Nakaguru, Mgugwe – Chisano na Ngalimila sambamba na Uchimbaji wa visima 10.
Mlelwa amevitaja visima vinavyotarajiwa kuchimbwa kuwa ni kisima cha Ipinde, Lumumwe na Ngalimila. Vingine ni Ikwambi, Kalenga, Miyomboni, Msita Ibaku, Iduindembo na Kitete.
Akizungumza katika mkutano huo mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Kilombero, Mohamed Msuya, ameipongeza RUWASA kwa kufanya kazi kwa bidii na kwenda sambamba na matakwa ya Ilani ya CCM na mipango ya serikali.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Kilombero, Dunstun Kyobya, ameziagiza taasisi za serikali wilayani humo, zenye madeni sugu ya ankra za maji kulipa haraka madeni hayo wanayodaiwa na RUWASA ili wakala huo uweze kutekeleza malengo yake ya kuwahudumia wananchi kwa ufanisi.