Dk. Nchimbi ‘asepa’ na kigogo CUF Tanga, aonya wabadhirifu

KATIBU Mkuu wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Taifa Balozi Dk. Emanuel Nchimbi ameonya viongozi wa umma wenye tabia za wizi na ubadhirifu wa fedha za umma waache mara moja kwa sababu wanarudisha nyumba juhudi za Rais Samia Suluhu Hassan anayehangaika usiku na mchana kutafuta fedha za maendeleo. Anaripoti Oscar Assenga, Korogwe… (endelea).

Pia Katibu Mkuu huyo amempokea aliyekuwa Katibu wa Chama cha Wananchi (CUF) wilaya ya Korogwe Vijijini, Nurdin Abubakar ambaye ameamua kujiunga na CCM ili kuunga mkono jithada za Rais Samia kutokana na kazi nzuri anayofanya.

Dk. Nchimbi aliyasema hayo leo Jumamosi wakati wa mapokezi yake yaliyofanyika eneo la Mombo wilayani Korogwe akitokea mkoani Kilimanjaro ambapo alilakiwa na viongozi mbalimbali wa mkoa huo wakiongozwa na Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Tanga, Rajabu Abdurhaman.

Katika salamu zake kwa wananchi Balozi Dk. Nchimbi alisema Rais Samia Suluhu anahaingaika na kupigana usiku na mchana kuhakikisha watanzania wanapata maendeleo kwa kutafuta fedha nje ya nchi, lakini watu wachache wanataka kuiba jambo ambalo linaweza kukwamisha juhudi hizo.

“Kwanza nimefika hapa Mombo – Korogwe pokeeni salamu wa Rais wetu Dkt Samia Suluhu na tuendelee kumuombea maana kama tuliwahi kumpata rais ambaye anaipenda nchi yake anaitumika kwa uzaendo na anatafuta pesa mikopo na misaada na inafika nchini ni wakati huu”Alisema  na kuongeza;

“Mtu anatakiwa kuweka mifuko 10 ya saruji yeye anaweka miwili huko ni kuhujumu, tuwaombee watu wenye roho za wizi, roho za ubadhirifu ili waache na Tanzania iweze kukamilisha miradi yake kwa ufanisi.

Aidha, amesema kwamba wapo viongozi Afrika ambao wanakwenda kutafuta fedha halafu wanagawana wenyewe yeye na familia zao lakini sio kwa Rais Samia ambaye amejipambanua kuhakikisha nchi yetu inapiga hatua kubwa za kimaendeeo.

“Kuna viongozi wa Afrika ambao fedha za Serikali Kuu haziwahi kufika chini na kufanya kazi za maendeleo hivyo ni wajibu kumuombea Rais na wasaidizi wake wakiwemo watu wenye roho za ubadhirifu, wizi ili ziweze kutoka maana haiwezekani mtu anahaingaika kupigana usiku na mchana na kuna watu wanataka kuiba hii sio sawa” amesema.

Akizungumzia ombi la Mbunge wa jimbo la Korogwe Vijijini, Timotheo Mnzava aliyetaka mji wa Mombo upate hadhi ya halmashauri kamili, Balozi Nchimbi amesema atashirikiana na uongozi wa serikali uhakikisha mji huo unapata hadhi hiyo ili na yeye awe sehemu ya historia hiyo.

Awali akizungumza katika katika mkutano huo, Mzava amesema wakati anaingia madarakani bajeti ya Wakala wa Barabara Mijini na Vijijini (TARURA) ilikuwa ni Sh 690 milioni lakini sasa ni zaidi ya Sh 2.3 bilioni ambazo zimewezesha barabara kujengwa na kukarabatiwa kwa uhakika ikiwemo barabara ya Mombo.

Pia amesema pamejenga vituo vya afya vinne na zahanati zaidi ya 10 huku akieleza kwa upande wa elimu hawana changamoto ya madarasa watoto wanasoma.

“Katika suala la maji wakina Mama wametuliwa ndoo kichwani kwa miradi ya kutosha na Mombo Rais ametoa Sh bilioni 3 kwa ajili ya ukarabati na upanuzi wa wa mradi wa maji wa mji wa Mombo na jana mkandasi amekabidhiwa kazi kwamba changamoto chache azibebe ili chama izisukume,” amesema.

Awali akimkaribisha Katibu Mkuu huyo, mwenyekiti wa CCM  mkoa wa Tanga Rajab Abdallah alimhakikishia kiongozi huyo kwamba kutokana na kasi aliyofanya Rais ya kuwaletea maendeleo deni lao kubwa ni kuhakikisha, mkoa huo  umeahidi kuchukua vitongoji 572 vyote vilivyopo mkoani Tanga, mitaa yote 263 na vijiji 779.