LICHA ya kukosa nafasi ya kucheza mara kwa mara chini ya Kocha Miguel Gamondi, kiraka wa Yanga, Faridi Mussa bado ataendelea kukipiga Jangwani hadi mwaka 2026.
Farid anayemudu kucheza kama kiungo mshambauliaji, winga na beki wa kushoto, aliyejiunga na Yanga Agosti, 2020 akitokea Tenerife ya Hispania ataendelea kukipiga kwa mabingwa hao wa Tanzania baada ya leo kuongeza mkataba wa miaka miwili.
Chanzo cha kuaminika kutoka ndani ya Yanga, kimeliambia Mwanaspoti Farid amesaini mkataba huo mpya baada ya makubaliano ya pande zote mbili kwenda vizuri na mchezaji kuridhia kubaki ndani ya timu hiyo na kumaliza utata uliokuwapo kwamba huenda akaondoka baada ya kumaliza mkataba aliokuwa nao.
Nyota huyo wa zamani wa Azam, amekuwa akihusishwa kurejea katika klabu hiyo iliyomlea, huku akitajwapia kuhitajiwa na Singida Black Stars (zamani Ihefu).
“Ni kweli leo kasaini miaka mingine miwili sasa kutokana na kutambua uwezo wake na amekuwa msaada mkubwa kwani anaweza kucheza beki wa pembeni, winga, na kiungo mshambuliaji hivyo ni hazina kuwa na mchezaji wa aina yake,” kilisema chanzo hicho kutoka Yanga na kuongeza;
“Farid amekuwa na msaada ndani ya Yanga, licha ya msimu huu kukosa nafasi lakini bado ni kipaji ambacho kimekubalika na ku[pendekezwa kuendelea kuwepo ndani ya Yanga.”
Tangu akipige Yanga, nyota huyo amefanikiwa kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu Bara mara tatu mfululizo sawa na Kombe la Shirikisho na Ngao ya Jamii mara mbili, mbali na kufika fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika msimu uliopita na kuweka rekodi ya kuwa miongoni mwa wachezaji waliiingia Yanga makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika baada ya kupita miaka 25 na kufika hadi robo fainali ikitolewa na Mamelodi Sundowns.