Samia agawa matrekta ya milioni 246 Namtumbo

Rais Samia Suluhu Hassan ametoa matrekta matatu yenye thamani ya Sh 246 milioni ambayo yana jembe la kulimia, jembe la haro pamoja na tela katika Wilaya ya Namtumbo ili kukuza kilimo katika wilaya hiyo. Anaripoti Mwandishi Wetu … (endelea).

Rais Samia ametoa matrekta hayo kupitia Wizara ya Kilimo ambapo Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Kanali Ahmed Abbas Ahmed amekabidhi matrekta hayo kwa uongozi wa Wilaya ya Namtumbo na kuagiza yapelekwe kwenye tarafa mbalimbali, maana huko ndiko wakulima wanatoka.

Amemwagiza Mkuu wa Wilaya ya Namtumbo, Ngollo Malenya ahakikishe matrekta hayo yanatunzwa na kuwafikia walengwa.

Mkuu huyo wa wilaya, Malenya, amemshukuru Rais Samia akisema mbali na matrekta hayo amewawezesha wakulima katika wilaya yake kupata mbolea za ruzuku ambazo zimesababisha uzalishaji Namtumbo kuongezeka.

Amesema hatua ya kuwapa matrekta ndio dhana halisi ya kuleta Mapinduzi ya Kilimo katika wilaya yake.

Rais Samia amefikia hatua hiyo baada ya Septemba mwaka jana Mkuu huyo wa Wilaya, Malenya kununua na kugawa bure majembe 500 kwa wakazi wa wilaya hiyo kwa lengo la kuwafanya wananchi washawishike kulima.

Mkuu huyo wa Wilaya pia alisema hiyo ni sehemu ya kuunga mkono jitihada za Rais Samia katika kuinua Sekta ya Kilimo nchini huku akikariri kibwagizo cha shairi maarufu kwamba: “Kama mnataka mali mtaipata shambani”.