Simulizi binti alivyochomwa moto kwa tuhuma za wizi

Mwanza. “Saa sita usiku wa kuamkia Jumapili, nilipokea simu nikaelezwa mdogo wako ana shida. Nikakodi pikipiki, nilipofika kwa bibi nikabaini ameunguzwa kwa moto.”

Ndivyo anavyoanza simulizi Joseph Semando, mkazi wa Kijiji cha Idetemiha, Kata ya Usagara akisimulia tukio la mfanyakazi wa ndani kumwagiwa mafuta ya taa na kuchomwa moto.

Tukio hilo alilotendewa Grace Joseph (17) lilitendeka Juni 4, 2024 katika kata na tarafa ya Usagara, wilayani Misungwi, mkoani Mwanza.

Binti huyo inadaiwa alitendewa kitendo hicho akituhumiwa kuiba Sh161,000 mali ya bosi wake Christina Shiriri (43), mfanyabiashara na mkazi wa Usagara anayeshikiliwa na Jeshi la Polisi.

Akizungumza na waandishi wa habari Juni 5, 2024, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Wilbroad Mutafungwa alisema Christina anadaiwa kutenda tukio hilo akimtuhumu binti huyo kuiba Sh161,000 alizokuwa amezihifadhi chumbani kwake.

Kamanda Mutafugwa alisema alipohojiwa polisi mtuhumiwa alidai binti alipoulizwa alikubali na kuzirejesha ndipo mtuhumiwa alipomwagia mafuta ya taa na kumchoma moto.

Semando amesema baada ya kumkuta binti akiwa katika hali mbaya alimpeleka Hospitali ya Nyanza iliyopo Usagara ambako walipewa rufaa ya kwenda Hospitali ya Wilaya ya Misungwi.

“Mashuhuda wanasema binti alikuwa akifanya kazi kwa mtu, akawa ametoka kuelekea kazini baada ya kurudi akakuta hamna fedha ndipo akaamua kumpiga na kumchoma moto baada ya kumwagia mafuta mwilini,” anadai Semando.

Shangazi wa binti huyo, Felista Simandu amesema hali ya binti bado ni mbaya kutokana na majeraha makubwa mikononi, mapajani, tumboni na kwenye matiti.

“Nilipigiwa simu na mtoto wa kaka yangu kwamba Grace amechomwa moto na bosi wake, nilikwenda hospitalini alikolazwa. Ana hali mbaya, inavyoonekana aliunguzwa baada ya kumwagiwa mafuta ya taa na kuchomwa na kibiriti akiwa amevaa nguo,” amedai.

“Baada ya kuuliza chanzo cha tukio wakaniambia anadaiwa amechukua fedha. Tangu aanze kazi pale alikuwa na siku tatu tu,” amedai.

Mwanyekiti wa Kitongoji cha Isera, Kijiji cha Idetemiha katani Usagara, Elikana Masanja amesema kwa mujibu wa taarifa za majirani binti huyo alikuwa na siku tatu tangu alipoanza kazi.

“Kwa maelezo ya watu alienda kutafuta kazi ndipo alipokutana na mama huyo aliyewahoji majirani iwapo wanamfahamu binti huyo. Mmoja alidai anamfahamu anaishi mtaa wa jirani kwa mama aitwaye Mwanasana,” alisema.

Amesema taarifa alizopewa ni kuwa mama huyo ambaye ni mfanyabiashara alitoka kwenda Sengerema kwenye biashara baada ya kurudi alikuta ndani hapako sawa na fedha hazipo.

Hata hivyo, amesema baada ya tukio hilo hakupewa taarifa hadi alipokuja kusikia kutoka kwa raia wema, ndipo alipokwenda eneo la tukio lakini hakufunguliwa geti.

“Nilipata taarifa kutoka kwa raia wema Juni 4, 2024 nikapiga simu kwa Christina lakini haikupatikana,” amesema.

Amesema Juni 5 akifuatana na mtendaji walikwenda nyumbani kwa mtuhumiwa ambako hawakufunguliwa mlango wa uzio wa nyumba zaidi ya kusikia sauti ya mbwa wakibweka ndani ya uzio.

Anaeleza walienda kwa jirani ambaye naye alieleza hana taarifa kamili za tukio hilo.

Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Wilaya ya Misungwi, Dk Clement Mwarabu,  amesema binti huyo ameungua zaidi ya asilimia 20 ya mwili wake.

Amesema uongozi wa hospitali umetoa msamaha wa matibabu kutokana na hali aliyonayo.

“Tulimpokea mgonjwa, tuliambiwa alipata changamoto ya kuunguzwa moto na alikuwa katika hali mbaya ya kuhitaji huduma ya dharura. Ameungua mikono, tumbo na kwenye mapaja,” amesema.

Akizungumza na Mwananchi Juni 7, 2024 amesema kwa sasa anaendelea kupatiwa matibabu yanayosimamiwa na Serikali.

Mkuu wa Wilaya ya Misungwi, Johari Samizi amewataka wazazi, hususani wanaoishi na wafanyakazi wa nyumbani kuacha kuwafanyia ukatili, badala yake kuwachukulia hatua za kisheria wanapobainika kutenda makosa.

“Kitendo kilichofanyika hakikubaliki kwa sababu alipaswa kuchukua hatua za kisheria kwa kumpeleka kwenye mamlaka husika,” alisema.

Ofisa Ustawi wa Jamii Shirika la Kutetea Haki za Wafanyakazi wa Majumbani la WoteSawa, Renaida Mambo mbali ya kulaani tukio hilo,  amesema kuna wimbi la waajiri kuajiri wafanyakazi walio chini ya miaka 14 linalochochea vitendo vya ukatili.

Amesema mwaka 2023, walipokea kesi 19 za watoto walio chini ya miaka 14 walioajiriwa kazi za nyumbani.

Mambo alisema pia walipokea kesi 67 za wafanyakazi wa nyumbani waliodhulumiwa mishahara yao, vipigo na wengine kubakwa.

Mratibu Kamati ya Amani ya Viongozi wa Dini Mkoa wa Mwanza na Mjumbe wa Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (Bakwata) Mkoa wa Mwanza, Sheikh Twaha Bakari,  amewataka waajiri na wananchi kufuata taratibu na sheria yanapotokea matukio kama hayo.