Ifakara. Serikali kupitia Shirika la umeme nchini Tanesco imetoa Sh400 milioni kwa ajili ya kuondoa adha ya mafuriko yanayowakuta wananchi wa Ifakara kila mwaka.
Fedha hizo zimetolewa kwa ajili ya kuimarisha kingo za mto Lumemo na kujenga tuta kubwa lenye urefu wa kilomita nane ili kuuzuia mto huo kumwaga maji kwenye makazi ya wananchi.
Tuta hilo ambalo pia litakuwa na kimo cha mita moja na nusu kutoka chini kwenda juu ujenzi wake utaanzia katika kata za kibaoni katika eneo lilipo daraja la Machipi ambako ndiko kunapoanzia maji kupasua na kwenda maeneo mengine na kuishia katika kata ya Lipangalala.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa ujenzi wa tuta hilo mwakilishi wa Tanesco, Maulidi Alphonsi ameeleza sababu za shirika hilo kuamua kutoa fedha hizo ni pamoja na umuhimu mkubwa wa mto Lumemo kwenye uzalishaji umeme katika bwawa la Mwalimu Nyerere.
Alphonsi ambaye ni mhandisi wa shirika hilo ameeleza uamuzi huo ni katika kutekeleza jukumu lao la kulinda vyanzo vyote vya maji, huku akieleza mojawapo ya njia za kulinda vyanzo hivyo ni kuimarisha kingo za mito kwa kujenga matuta.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Kilombero, Dunstan Kyobya amemshukuru Rais Samia Suluhu Hassan pamoja na mbunge wa Jimbo la Kilombero, Abubakari Asenga kwa jitihada zake za kuhakikisha fedha zimepatika kwa ajili ya kumaliza adha ya mafuriko kwa Wanakilombero.
“Tunamshukuru Rais kwa kutuletea Sh400 milioni ili ziweze kuboresha kingo za mto Lumemo na kuwaondolea kero ya mafuriko wananchi ndani ya mji wa Ifakara,” amesema Kyobya.
Aidha mkuu huyo wa wilaya amesisitiza kuwa ili kulinda mto Lumemo wasimamizi wa kata zote zinazozunguka mto huo kuhakikisha wanazingatia sheria ya mita 60 kwa kutofanya shughuli zozote za kibinadamu.
Akishukuru kwa niaba ya wananchi wa kata zote sita zilizopata athari za mafuriko, Diwani wa Kata ya Viwanja Sitini, Eric Kulita ameishukuru Serikali kwa hatua hiyo muhimu itakayoleta amani na utulivu kwa wakazi wa maeneo hayo. “Ushauri wangu kwa Serikali ni na kuishauri kuendelea kutoa elimu kwa baadhi ya wananchi wanaofanya shughuli za kuharibu kingo za mito.”
Naye mhandisi wa maji kutoka makao makuu ya Bonde la Rufiji, Geofrey Mkonda ameeleza, “tukumbuke kuwa asilimia 65 ya maji yote yanayoendesha mradi wa Mwalimu Nyerere unaogharimu zaidi ya Sh6 trilioni yanatoka bonde hili la Kilombero hivyo wananchi wa maeneo hayo tuna wajibu wa kutunza vyanzo hivyo,” amesema Mkonda.
Mradi huo wa ujenzi wa tuta unaotekelezwa kwa miezi mitatu unasimamiwa na mamlaka ya maji bonde la Rufiji.