Tanzania majanga, yaikosa Riadha Afrika

HUWEZI kuamini, lakini ndo ukweli ulivyo, kwa mara ya kwanza Tanzania haitashiriki mashindano ya Riadha Afrika (African Athletics Championship) tangu yalipoanzishwa mwaka 1979 baada ya wanariadha waliotarajiwa kubeba bendera kukosa vigezo vya ushiriki.

Mashindano hayo ya 23 kwa mbio za viwanjani yafanyika kati ya Juni 21- 26, jijini Douala huko Cameroon, ikitazamiwa kushirikisha wanariadha zaidi ya 3500 kutoka nchi 50.

Katika mashindano hayo, Tanzania ilikuwa iwakilishwe na Hamida Nassoro aliyefuzu kupitia mashindano ya All African Games yaliyofanyika Machi mwaka huu, huko Accra, Ghana, lakini mwanariadha huyo anasumbuliwa na majeruhi na kumzuia asishiriki mashindano hayo.

Mjumbe wa Shirikisho la Riadha Tanzania (RT), Alfredo Shahanga ameithibitishia Mwanaspoti, Tanzania kwa mwaka huu hitashiriki mashindano hayo yanayofanyika kila baada ya miaka miwili kutokana na kukosa wanariadha wa kuiwakilisha.

Shahanga alisema walifanya mashindano ya mbio za wazi kwa ajili ya kutafuta vijana watakaofikia viwango kwa ajili ya kwenda kushiriki, lakini mambo yalienda sivyo.

Amesema mashindano hayo ya msako yalifanyika Mei 27 mwaka huu kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid, jijini Arusha kwa kushirikisha zaidi ya wanariadha 100 kutoka Arusha, Manyara, Pwani, Shinyanga na Tabora ikuhusisha wanaume na wanawake zikihusisha mbio za mita 100, 200, 400, 400, 1500 na 5000, lakini hakuna aliyefikia kiwango kinachotakiwa na Shirikisho la Riadha Afrika (CAA) hili kuweza kushiriki.

“Hatukuweza kumpata mchezaji yeyote aliyeweza kufikia viwango vinavyotakiwa na CAA ili kwenda kushiriki hivyo ieleweke tu mwaka huu hatutashiriki,” amesema Shahanga.