Dar es Salaam. Taasisi ya Chakula na Lishe Tanzania (TFNC), imeanzisha mradi wa kutengeneza vyakula kwa ajili ya kuwasaidia watoto wa shule na kundi rika la vijana balehe nchini kuanzia miaka tisa hadi 19 kukabiliana na upungufu wa damu na madini chuma.
Utafiti wa Afya na uzazi na Mtoto na Viashiria vya Malaria wa 2022 uliotolewa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS), unaonyesha vijana hao wanakabiliwa na upungufu wa damu kwa asilimia 50.
Akizungumza Dar es Salaam Julai 8,2024 kwenye ziara ya wataalamu kutoka chuo cha Afya cha Tsing Hua nchini China ambao ni wafadhili wa mradi huo, Mtafiti Mkuu kutoka TFNC, Dk Anselm Moshi amesema vyakula hivyo vitaenda kujibu changamoto iliyopo.
“Tunafanya hivi kwa sababu kundi hili la vijana limesahaulika kwenye afua nyingi za lishe na kusababisha kukumbwa na matatizo ya upungufu wa damu, vitamini A na madini ya zinki” amesema
Amebainisha kuwa, baada kubuni mradi huo walifanikiwa kupata fedha dola za kimarekani 28,000 kwa wafadhili kutoka nchini China na wameanza kutengeneza vyakula hivyo ambayo utendaji kazi wake utaenda kufanyiwa majaribio kwa wanafunzi wa Wilaya ya Temeke.
“Wanazuoni hawa kutoka China wamekuja kutembelea kuona mradi huu na kuona matokeo yake namna unavyoenda kusaidia kujenga afya za Watanzania,’’ amesema.
Ameongeza: “Tatizo la upungufu wa madini ya chuma kwa kundi hilo la vijana balehe ni zaidi ya asilimia 50.’’
Naye, Mkurugenzi Mtendaji TFNC, Dk Gerama Leyna amesema wataalamu wameanza kutengeneza virutubisho hivyo kwa kutumia maharage yaliochanganywa na madini ya zinki na chuma.
“Vilevile tunatumia mahindi ya njano ili kutengeneza biskuti na tunajitahidi zisiwe na sukari nyingi kuepuka uzito usiozidi,” amesema.
Dk Germana amesema tayari vyakula hivyo wameshaanza kuwapelekea vijana waliopo shule.
“Mipango yetu baada ya kumaliza majaribio madogo kuanzia Julai mwaka huu tutafanya majaribio kwa ukubwa zaidi nchini kuangalia iwapo mtoto akipatiwa asusa hii itakuwa na uwezo wa kutibu tatizo kwa ukubwa,” amesema.
Ameeleza kuwa mipango yao ni kukabiliana na bidhaa zilizopo sokoni na wanatamani kuwe na mchanganyiko wa bidhaa nyingi lakini zenye lishe bora zipatikane kwa wingi na bei nafuu.
Awali, akizungumza kwa niaba ya Wanazuoni hao kutoka chuo cha Afya cha Tsing Hua, Profesa Al Zhao amesema wamechunguza na kuangalia bidhaa zilizotengenezwa na taasisi hiyo kupitia mradi huo zina ubora na zitasaidia kukabiliana na changamoto iliyopo.
“Itasaidia kujenga lishe kwa kundi rika la vijana balehe kwa kuwa ni kundi linaloongoza kwa idadi kubwa lakini ni hazina na tegemeo kwa taifa lolote katika kukuza uchumi,” amesema.