Vaibu lamrudisha Aussems | Mwanaspoti

KOCHA wa zamani wa Simba, Mbelgiji Patrick Aussems amekiri kufurahia kurejea tena nchini, huku akiweka wazi vaibu la mashabiki hasa wanaojazana Uwanja wa Benjamin Mkapa ni moja ya sababu iliyomrejesha Tanzania na kujiunga na Singida Black Stars katika mashindano mbalimbali ya msimu ujao.

Akizungumza na Mwanaspoti, Aussems alisema anajisikia furaha kubwa kurudi kwa mara nyingine katika ardhi ya Tanzania, huku jambo ambalo limekuwa likimvutia ni kutokana na jinsi ushindani ulivyo kuanzia kwa mashabiki hadi timu zenyewe.

“Ni furaha kubwa kwangu kupata nafasi hii tena ya kurudi Tanzania, ni nchi yenye wapenza soka bora na kiukweli kipindi chote ambacho nimekuwa hapa nilikuwa nikifurahia kwa sababu ya aina ya mashabiki waliopo na ushindani uliopo,” alisema Aussems.

Aussems mwenye Leseni ya UEFA PRO ni uzoefu wa kufundisha klabu kubwa Afrika, Ulaya na Asia, zikiwemo za Al Hilal (Sudan), Simba (Tanzania), AFC Leaopards (Kenya), Shenzhen Ruby (China), ETG (Evian Thonon Gaillard) FC na Angers SCO FC ya Ufaransa. 

Kocha huyo aliyeiipa Simba ubingwa wa Ligi Kuu Bara mara mbili mfululizo na kuifikisha Robo Fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika 2018-2019, mbali na kuzifundisha klabu ila amewahi pia kufundisha timu za taifa zikiwemo za Nepal na Benin.

Aussems ambaye pia amehudumu kama Mkurugenzi wa Ufundi wa Marbella FC ya Hispania, amesaini mkataba wa mwaka mmoja na timu hiyo utakaoisha mwakani huku Mwanaspoti likifahamu ataongezewa mwingine ikiwa kikosi hicho kitamaliza nafasi nne za juu.