Zungu awatwisha mzigo wabunge bajeti ya kijinsia

Dodoma. Naibu Spika wa Bunge, Mussa Zungu amewataka wabunge kutizama Kanuni za Kudumu za Bunge kama zinakidhi ipasavyo utekelezaji wa dhana bajeti inayozingatia masuala ya kijinsia na iwapo zina kasoro,  ziboreshwe ili ziwawezeshe kuishauri Serikali kwa manufaa ya Taifa.

Zungu ameyasema hayo leo Juni 8, 2024 wakati akifungua mafunzo ya wabunge kuhusu uchambuzi wa bajeti kwa kuzingatia masuala ya kijinsia.

Mafunzo hayo yamefadhiliwa na Shirika la Kimataifa la Maendeleo (UNDP) na Shirika la Umoja wa Kimataifa linaloshughulikia Masuala ya Wanawake (UN Women).

Naibu Spika huyo amesema miongoni mwa jitihada zilizofanywa na Serikali ya awamu ya sita,  ni kupunguza kodi katika majiko ya gesi ambayo ni rafiki na salama.

“Suala la kupunguza kodi katika nishati safi ni muhimu katika kuhakikisha maendeleo endelevu ya dunia yanatimia, pamoja na kupunguza vifo vya wanawake vinayotokana na matumizi yasiyo rafiki ya nishati,” amesema.

Amesema inakadiriwa kuwa Tanzania inapoteza zaidi ya watu 33,000 kutokana na vifo vinavyotokana na matumizi ya nishati isiyo salama.

Amewaomba wabunge watakaporudi majimboni kutoa elimu kwa wananchi,  kwa kuwa bado jamii haina elimu kuhusiana na matumizi ya kuni, gesi na mkaa.

Amesema kilo sita za gesi ni sawa na matumizi ya kilo 30 za mkaa,  huku kilo sita za gesi zikiwa ni sawa na kilo 60 za kuni.

“Utaona jinsi ambavyo miti inakatwa katika mapori yetu, nendeni mkaelimishe umma, tumsaidie na kumshika mkono Rais Samia Suluhu Hassan kuhakikisha kuwa nishati safi inawafikia wananchi,” amesema.

Ametaka wabunge kuhakikisha kuwa bajeti inakuwa ni chombo cha kumkomboa mwanamke na kutoa pongezi kwa Serikali kwa kuwa na miongozo ya bajeti inayozingatia masuala ya kijinsia.

Amesema miongozo ya mwaka 2023/24 na 2024/25,  imetoa maelekezo kwa maofisa wanaoandaa bajeti kuzingatia masuala yanayohusu jinsia katika uwasilishaji, uandaaji, utekelezaji ufuatiliaji, tathimini na utoaji wa taarifa za utekelezaji wa bajeti zao.

Amesema hatua hiyo ni muhimu sana kwa wabunge katika utekelezaji wa majukumu ya msingi hususan katika kupitisha na kusimamia bajeti katika mtizamo wa kijinsia.

“Hivyo ili kwenda sambamba na utekelezaji wa dhana hii yenye mtazamo wa kijinsia,  nadhani tutazame pia kanuni zetu kama zinakidhi ipasavyo utekelezaji wa dhana hiyo na kama zina kasoro ziboreshwe ili ziwezeshwe waheshimiwa wabunge kuweza kushauri kuhusu bajeti kwa minajili ya Taifa letu,” amesema.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Dk Seif Shekalaghe, amesema ujumishaji wa kifedha umeongezeka kutoka asilimia 65 mwaka 2017 hadi asilimia 78 mwaka 2023.

Pia amesema mikopo ya halmashauri kwa vijana wanawake na watu wenye ulemavu imeongezeka kutoka Sh15.6 bilioni mwaka 2017 hadi Sh37.59 bilioni mwaka 2021 na kuanzishwa kwa Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF).

Amesema sera mpya ya 2023 imelenga kukuza haki na usawa wa kijinsia katika nyanja zote za maisha na maendeleo na matarajio,  ni kupungua kwa hali ya utegemezi kwa wanawake na kuwa na mipango jumuishi yenye uwiano sawa wa kijinsia inayogusa mahitaji ya jinsia zote.

Dk Shekilaghe ametumia fursa hiyo kuwaomba wabunge kupitia vikao na mikutano na wananchi kuendelea kufikisha elimu kuhusu sera na umuhimu kwa ustawi wa jamii.

Pia amewataka kuhakikisha masuala ya jinsi yanajumuisha na kupewa kipaumbele.