ARSENAL itatakiwa kutoa Pauni 50 milioni kwa ajili ya kuipata saini ya kiungo wa Aston Villa, Douglas Luiz, katika dirisha hili lakini kwanza itatakiwa kuishinda Juventus ambayo inahitaji huduma yake pia.
Luiz amezivutia timu nyingi barani Ulaya kutokana na kiwango bora alichoonyesha kwa msimu uliopita ambapo alifunga mabao 10 na kutoa asisti 10.
Villa ambayo imefuzu kucheza Ligi ya Mabingwa msimu ujao inahitaji kupata pesa zitakazowawezesha kufanya usajili wa wachezaji wapya watakaoweza kuwafanya wapambane vyema kwenye michuano hiyo.
Mbali ya kutaka kusajili kwa ajili ya kupambana kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa, mabosi wa Villa wanataka kumuuza Luiz ili kujiweka katika mazingira mazuri ya kuepuka rungu la mamlaka za soka nchini England kwa kukiuka sheria za matumizi ya pesa.
Mkataba wa sasa wa Luiz unatarajiwa kumalizika 2026.