Dar ea Salaam. Jukwaa la Katiba Tanzania (Jukata), limebainisha kasoro 11 zilizopo katika sheria za uchaguzi za mwaka 2024, likieleza baadhi ya vipengele vinaibua wasiwasi kuhusu uadilifu wa mifumo ya uchaguzi.
Miongoni mwa kasoro hizo ni kuendelea na makamishna wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi katika Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, kutumia watumishi wa umma katika shughuli za uchaguzi na kanuni ya kuamua mshindi wa kura za urais kwa kuangalia kura nyingi.
Miezi michache iliyopita, Rais Samia Suluhu Hassan alisaini sheria hizo ambazo ni Sheria ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani namba 1 ya mwaka 2024, Sheria Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi namba mbili ya mwaka 2024, Sheria ya Marekebisho ya Sheria za Vyama vya Siasa namba tatu ya mwaka 2024.
Akizungumza na wanahabari leo Jumatatu Juni 10, 2024, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Jukata, Dk Ananilea Nkya amesema kitendo cha kuendelea na makamishna waliopo katika Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi hakionyeshi mabadiliko ya kuboresha Tume ya Uchaguzi.
Suala kama hilo, liliwahi kulalamikiwa na chama cha ACT-Wazalendo, kilichotoa wito Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC -ya zamani) ijiuzulu kupisha kuundwa mpya itakayopatikana kwa utaratibu wa ushindani.
Katika maelezo yake, Dk Nkya amewaambia wanahabari:“Kuendelea kutumia watumishi wa umma kwenye shughuli za uchaguzi kunashusha kuhusu uadilifu wa uchaguzi.
“Pia, kanuni ya kuamua mshindi wa matokeo ya urais kwa kuangalia mwenye kura nyingi hata kama kamzidi mwenzake kura moja kutangazwa mshindi wa kiti cha urais, inadhohofisha uhalisia wa uwakilishi wa wananchi,” amesema Dk Nkya.
Mbali na hilo, Dk Nkya amezitaja kasoro nyingine ni kuendelea kuzuia mgombea huru au binafsi kwenye uchaguzi kunanyima au kukiuka haki za watu binafsi ambao hawana nia au hawaridhiki na siasa za vyama vinavyoshindana kusimama kugombea kwenye chaguzi.
Pia, amesema kukosekana kwa sheria maalumu za kusimamia uchaguzi wa Serikali za mitaa kama inavyotakiwa katika kifungu cha 10 (a) cha sheria ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi, kunaibua wasiwasi kuhusu uhalali na uwazi wa mchakato huo.
“Jambo jingine ni kuendelea kuweka marufuku kwa wafungwa na watu walio kizuizini kupiga kura,” amesema Dk Nkya.
Hata hivyo, Kanuni ya Tume ya Huru ya Taifa ya Uchaguzi inaeleza wafungwa na mahabusu waliohukumiwa kifungo chini ya miezi sita ndio watakaopiga kura.
Wiki iliyopita, mkurugenzi wa tume hiyo, Ramadhan Kailima aliwaambia viongozi wa vyama vya siasa 19 kuwa taasisi hiyo imetenga vituo 140 Tanzania Bara na Zanzibar kwa ajili ya kuwaandikisha wafungwa, mahabusu na wanafunzi waliohukumiwa kifungo chini ya miezi, ili kupiga kura.