Mkuu Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila amewataka watendaji wa mkoa huo kufanya kazi kwa uweledi ili watakapoondoka waache heshima kutokana na utendaji wao. Anaripoti Mwandishi Wetu …(endelea).
Pia amewataka kuhakikisha miradi yote ya maendeleo inatekelezwa kwa wakati badala ya kutembea na kamera kila mahali kukagua miradi hiyo kwani anayefanya hivyo ana dalili za tatizo la kuchanganyikiwa.
Chalamila ametoa rai hiyo leo Jumatatu alipofanya ziara ya kushtukiza na kukagua maendeleo ya ujenzi wa barabara ya Mazda Kimanga yenye urefu wa kilomita 3.7 wilaya ya Ilala.
Amefanya ukaguzi huo kufuatia ahadi aliyoitoa kwa wananchi wakati wa mkutano wa hadhara wa kuongea na wananchi wa eneo hilo alioufanya Tabata Kimanga tarehe 30 Mei 2024.
Chalamila amemtaka mkandarasi anayejenga barabara hiyo kuongeza kasi ili mradi ukamilike kwa wakati, wananchi wa maeneo hayo waweze kuitumia katika shughuli zao za kila siku za kujiletea kipato.
Aidha, Chalamila amesema Rais Samia Suluhu Hassan ameelekeza nguvu kubwa katika kuboresha miundombinu ya barabara katika maeneo mbalimbali hapa nchini hususani mkoa huu.
“Niwatake makandarasi waliobahatika kupata kazi kufanya kazi kwa weledi kuzingatia muda na thamani ya pesa,“ amesema Chalamila
Pia ametoa rai kwa wananchi kuendelea kuelimishana juu ya kutoziba mifereji ya maji taka pia kutotupa taka ovyo ambazo huchangia kwa kiasi kikubwa kuziba mifumo ya maji taka
Sanjari na hilo Chalamila amewataka wananchi kutokuwa na shaka kuhusu kusuasua kwa ujenzi wa barabara hiyo ambapo amesema atakuwa anafuatilia kwa karibu maendeleo ya barabara hiyo pale atakapoona kuna shida atachukua hatua stahiki mara mmoja.
Aidha, ametoa rai kwa wananchi kuendelea kulinda amani ya Mkoa wa Dar es Salaam kwa kuwa ndicho kitovu cha uchumi wa nchi, Diplomasia na mambo mengine mengi yenye maslahi mapana kwa nut mmoja mmoja, Taifa la Tanzania, na mataifa mengine duniani.