WANAHISA wa Benki ya NMB wameidhinisha gawio la Sh 181 bilioni, sawa na Sh 361 kwa kila hisa moja kwa mwaka unaoishia tarehe 31 Disemba 2023. Anaripoti Mwandishi Wetu … (endelea).
Azimio hilo limepitishwa leo Jumatatu katika Mkutano Mkuu wa 24 wa Wanahisa wa Benki ya NMB.
Afisa Mtendaji Mkuu wa Benki ya NMB, Ruth Zaipuna amesema hilo ni ongezeko la 26% ukilinganisha na gawio la jumla la Sh 143.1 bilioni walilolipa mwaka 2022, na kuandika historia mpya ya kuwa gawio kubwa zaidi kuwahi kutolewa na taasisi ya fedha nchini kwa wanahisa wake.
“Mafanikio haya ni matokeo ya mazingira mazuri ya kibiashara yaliyowekwa na Serikali yetu, imani ya wanahisa na wateja wetu, juhudi za wafanyakazi wetu na ushirikiano mzuri tulionao na wadau wetu wote.
“Tutaendelea kusimamia ahadi yetu ya kudumu katika ukuaji jumuishi na endelevu kwa ustawi wa jamii tunayoihudumia na uchumi wa nchi yetu ya Tanzania kwa ujumla, amesema Zaipuna na kuongeza;
“Tunawashukuru wadau wetu wote kwa kuwa sehemu ya mafanikio haya.”