Mtwara. Wakulima wa zao la ufuta mkoani Mtwara wameeleza kutoridhishwa na uendeshaji wa minada kupitia mfumo wa Mauzo wa Kieleteoniki (TMX) wakihoji uwazi wa nani anayeanzisha na kufunga mnada huo.
Akizungumza jana Jumamosi Juni 22, 2024 baada ya kumalizika kwa mnada wa pili uliofanyika wilayani Masasi ambako zaidi ya tani 8,000 za ufuta zimeuzwa kwa bei ya juu ya Sh3,280 na ya chini Sh3,110 kwa kilo moja, Remijius Dominic, mkulima wa ufuta wilayani Masasi amesema mfumo huo hauwanufaishi wakulima.
“Kusema kweli, sijaridhishwa na mfumo huu. Hatujui nani anayeendesha mnada. Tunafika na kukuta mnada tayari uko kwenye hatua ya tisa. Hatujui nani anafungua na kuufunga mnada,” amesema Dominic.
Amesema bei ya ufuta hairidhishi, akifananisha na mnada wa Songwe mwezi uliopita ambako ufuta uliuzwa Sh4,800 kwa kilo moja, lakini ndani ya mwezi mmoja bei imeshuka hadi kufikia Sh3,000 kwa kilo moja.
“Huu mfumo sio mzuri, mnada unaendelea na wanunuzi ni wawili tu. Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe alisema minada hii ingejumuisha wanunuzi kutoka duniani kote. Dunia nzima ni wanunuzi wawili tu?” amehoji mkulima huyo.
Juma Ibrahimu, mkulima wilayani Masasi, ameunga mkono hoja ya Dominic, akisema uchache wa wanunuzi hauleti tofauti wala ushindani wowote wa bei kwenye mfumo wa TMX.
“Hatuoni ushindani wa mnada sokoni. Wateja ni wachache. Tunaomba Serikali ihakikishe wanunuzi angalau 20 wanasajiliwa, ili kuruhusiwa kununua, kuliko kuruhusu wanunuzi wawili ambao wananyonya wakulima kwa bei ndogo,” amelalamika Ibrahimu.
Mwakilishi wa TMX atoa neno
Hata hivyo, Mwananchi Digital imezungumza na Prince Mng’ong’o, mwakilishi wa TMX kuhusiana na malalamiko hayo na kusema uamuzi wa kuuza ama kutokuuza ni wa mkulima mwenyewe, kulingana na bei anayoona kwenye mnada.
Mng’ong’o amesema mkulima ana mamlaka ya kuuza mzigo wake baada ya kuona bei husika kwenye mnada.
“Hatumshurutishi mtu kuuza mzigo wake (ufuta), akiona bei hajaridhika nayo basi anarudi na mzigo wake maana sisi tunakwenda na bei za soko,” amesema.