Caravans T20… Lions yawaliza Flashnet Strikers

ILIKUWA ni jioni njema kwa Park Mobile Lions baada ya ushindi mnono wa mikimbio 60 dhidi ya Flashnet Strikers katika mduara (oval) wa Leaders Club jijini, Dar es Salaam mwishoni mwa juma.

Mohamed Jawad aliyetengeneza mikimbio 54 na Kashif Ahamed aliyepiga mikimbio 39 ndio walioibeba Lions kuelekea ushindi wao na kuifanya jioni ya Jumamosi kuwa ni burudani tosha kwa timu yao.

Katika mchezo huo, Lions ndio walioshinda kura ya kuanza na wakapendelea kufunga (betting)  na utashi huo uliwapelekea kuvuna mikimbio 150 huku wakitumia wadunguaji sita tu, na alama hizi zilikuwa ngumu sana kuzifikia kwa vijana wa Flashnet Strikers kwani, baada ya mpambano mkubwa waliambulia mikimbio 90 tu huku wakipoteza wiketi tisa.

Mchezo huu ni muendelezo wa michuano ya Ligi ya Kriketi kwa mizunguko 20 (T20) ikiwa chini ya usimamizi wa Chama cha Kriketi nchini (TCA) na kudhaminiwa na kampuni ya Petrofuel.

Kushindwa vibaya kwa Flashnet Strikers si jambo lililotegemewa, kwani wiki iliyopita timu hii ilifanya vizuri ikiifunga Azania Bank Stars uwanjani hapo kwa ushindi mnono wa wiketi saba baada ya wao kuangusha wiketi tatu tu.

Azania ndiyo walioshinda kura ya kuanza na wakafanikiwa kutengeneza mikimbio 121 huku wakiangusha wiketi nane, alama ambayo Flashnet Strikers waliifikia kwa kupata mikimbio 122 huku wakiangiusha wiketi tatu.

Azania iliwategemea kina Muzamil Hassan aliyetengeneza mikimbio 32 na Salfraz Tare aliyeleta mikimbio 29, lakini jitihada zao ziligonga mwamba kwa vijana wa Flashnet Strikers.

Kwa mujibu wa Ateef Salim, Ofisa Habari na Mawasiliano wa TCA, Juni umeng’arishwa sana Ligi ya Caravans na ile ya Vijana ya U17.

Mashindano haya mawili, kwa mujibu wa  Ofisa huyo, yana lengo la kuleta ukomavu kwa wachezaji wa kriketi.

Related Posts