Dar es Salaam. Daladala za ruti zote jijini hapa zimeruhusiwa kupeleka abiria katika Maonyesho ya Biashara ya Kimataifa ya 48 maarufu Sabasaba yanayotarajiwa kuanza Juni 28 mwaka huu.
Hayo yameelezwa kwenye taarifa ya Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri wa Ardhini (Latra) iliyotolewa leo Juni 25, 2024 katika ukurasa wake wa Instagram.
Akizungumza na Mwananchi kuhusu taarifa hiyo, Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano wa Latra, Salum Pazzy, amesema hatua hiyo imekuja kutokana na uhitaji wa abiria na wafanyabiashara wanaotaka kwenda kushiriki maonyesho hayo.
Hata hivyo, Pazzy amesema katika utekelezaji wa ruhusa hiyo wametoa masharti matano ya kuzingatia katika utoaji wa huduma hiyo, ikiwamo ya daladala husika kuwa na leseni hai ya usafirishaji.
Sharti jingine ni utozaji nauli usiozidi viwango vya nauli elekezi iliyoidhinishwa na Latra.
“Pia, safari iwe inaanzia na kuishia katika njia ambayo daladala imesajiliwa na sio vinginevyo.
“Mfano gari la Tegeta Nyuki kwenda Makumbusho kupitia barabara ya Bagamoyo itabeba abiria kutoka Tegeta Nyuki hadi Makumbusho na litaendelea na safari hadi viwanja vya Sabasaba na kurudi tena hadi Makumbusho ili kubeba abiria waliopo Makumbusho wanaoelekea Tegeta Nyuki,” amefafanua Pazzy.
Pia, amesema dereva ahakikishe anafuata sheria zote za usalama barabarani kama vile kutopakia eneo ambalo hakuna kituo na kufuata maelekezo atakayopewa afikapo viwanjani ili kupunguza foleni barabarani.
“Pia, dereva na kondakta wake wanatakiwa wavae sare safi na nadhifu na watumie lugha nzuri kwa abiria,” amesema.
Akitoa maoni kuhusu uamuzi huo, Katibu wa Umoja wa Wamiliki wa Daladala (Darcoboa), Shifwaya Lema amesema ni jambo zuri kwa sababu Latra wameangalia uhitaji kwa wakati huo.
Hata hivyo, Lema ameshauri askari wajipange ili kuepusha foleni ikiwamo suala la malori yanayoingia na kutoka maeneo yale ambayo yamekuwa yakichangia kuwepo kwa foleni eneo hilo mara kwa mara.
Dereva wa daladala inayofanya safari zake Masaki Simu 2000, Omar Msafiri amesema hatua hiyo itawasadia kwa kuwa watakuwa na uwanja mpana wa kupata abiria.
“Kuna wakati abiri njia ya kwetu wanakata, hivyo kama utaona vipi, unalipeleka njia hiyo ya sabasaba kwa kuwa hayo maonyesho huwa watu wengi wanakwenda haswa siku za mwisho wa juma,” amesema.
Jenifer George, mkazi wa Tegeta amesema amefurahishwa na uamuzi huo wa Latra kwa kuwa utawapunguzia usumbufu wanapokuwa wameenda na watoto
“Yaani huwa inafika mahali unataka watoto nao waende kuona maonyesho hayo, lakini ukifikiria usafiri wa kuungaunga, gharama unazoingia, unajikuta mwili unaingia ganzi na kuwaacha, niwapongeze Latra kwa kuja na maamuzi haya,” amesema.
Joackim Maksambo, amesema huwa akifanya kazi katika migahawa iliyopo hotelini hapo, hivyo itamrahishia kupata usafiri mmoja anapotokea na hivyo kumpunguzia gharama.
Rahma Shukuru, mkazi wa Sinza na mfanyabiashara anayeshiriki maonyesho hayo mara kwa mara, amesema sasa ataacha kwenda na gari kwa kuwa ilikuwa inamlazimu kulipia gharama za maegesho katika kipindi chote cha maonyesho kutokana na usafiri wa kumfikisha huko kuwa mgumu.