Teknolojia ilivyosaidia kuongeza idadi ya faru nchini

Dar es Salaam. Wizara ya Maliasili na Utalii imesema idadi ya faru imeongezeka kutoka 161 mwaka 2019 hadi kufikia 253 mwaka jana kutokana na matumizi ya teknolojia ya ulinzi waliyowekewa iitwayo Transmitters.

Hayo yamebainishwa hii leo Jumanne ya Juni 25, 2024 katika warsha iliyoandaliwa na Shirika la Uhifadhi wa Mazingira Duniani (WWF), iliyowakutanisha wataalamu wa wanyamapori pamoja na Serikali jijini Dar es Salaam.

Ofisa Wanyamapori Mkuu kutoka Wizara ya Maliasili na Utalii, Antonia Rafael amesema matumizi ya Transmitters yamesaidia kuhakikisha wanakuwa salama kutokana na changamoto wanazopitia.

“Faru walikuwa 161 mwaka 2019 lakini hadi mwaka jana walikuwa 253, hivyo wameongezeka, juhudi zinahitajika kwa kiasi kikubwa kwa sasa hususuani katika matumizi ya teknolojia,” amesema Antonia ambaye amemuwakilisha Mkurugenzi wa Idara ya Wanyamapori.

“Serikali inatoa wito kwa wadau waweze kushikamana nayo katika kuhakikisha wanyama hawa adimu wanalindwa kwa gharama zote.”

Akizungumzia changamoto za ulinzi wa wanyama hao, Antonia amesema awali faru waliwindwa na majangili kwa sababu ya pembe zake, lakini juhudi za Serikali kwa kushirikiana na wadau wamezuia kwa gharama kubwa.

Amesema faru wana umuhimu katika utalii unaoleta matokeo chanya kiuchumi na katika sekta hiyo nchini hivyo lazima walindwe.

Kwa upande wake, Noah Sitati, mtaalamu wa viumbe hai kutoka WWF, amesema awali waliweka mkakati wa kuongeza idadi ya faru kwa asilimia tano, lakini wamefanikiwa kukua kwa asilimia zaidi ya kumi, hivyo wamevuka malengo.

“Wanaongezeka, lakini bado tuko chini sasa kinachotakiwa ni kuweza kuona namna ya kurudisha maeneo watakayoingizwa kwa kuwa tuna eneo kubwa mfano kama Arusha National Parks,” amebainisha Sitati.

Mratibu wa faru kitaifa, Filbert Ngoti amesema kuna malengo mkakati kumi, ikiwamo elimu na uelewa wa jamii katika ulinzi wa wanyama pori.

“Kwa sasa tunaandaa mpango wa tano wa miaka 10 wenye shabaha ya malengo mkakati katika ulinzi wa wanyama hao. Kila taasisi zinazohifadhi wanyamapori zina kitengo mahususi cha elimu kwa umma juu ya uhifadhi na usimamizi wa faru,” amesema.