Kiongozi Kariakoo awaachia uamuzi wafanyabiashara kufunga, kufungua maduka

Dar es Salaam. Mwenyekiti wa Wafanyabiashara Karikaoo, Martin Mbwana amewaachia uamuzi wafanyabiashara wa kufunga ama kufungua maduka yao, baada ya kuwapatia mrejesho wa kile kilichozungumzwa katika kikao baina ya viongozi hao na Serikali.

Mbwana amesema biashara hizo ni zao na uamuzi wa kufunga au kufungua hayapaswi kuingiliwa na mtu, huku kazi ya Serikali ikiwa ni kuweka mazingira mazuri ili kuchukua kodi.

Ametoa kauli hiyo leo Jumatano, Juni 26, 2024 katika mkutano na wafanyabiashara, ikiwa ni siku ya tatu tangu wagome kufungua maduka, wakieleza kukerwa na usumbufu wanaoupata kutoka Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).

Mbwana amesema hana nguvu ya kuwalazimisha kufungua maduka kama alivyowaambia Jeshi la Polisi kuwa haliwezi kuwa ndani ya mawazo ya mfanyabiashara.

Amesema mfanyabishara kufunga duka lake na kukaa pembeni inamaanisha amevurugwa na kukata tamaa, kwani anategemea duka kuendesha maisha yake, hivyo ni vyema nguvu kutotumika na badala yake kukaa mezani ndiyo suluhisho.

“Haikuwa jambo jepesi, tulionekana kama wahaini, kwamba hawa watu wamefunga mwaka jana na mwaka huu wanafunga msiwasikilize hawa ni wahuni, wanataka kuitisha Serikali washughulikiwe,” amesema Mbwana.

Amesema kama mwenyekiti na viongozi wanzake baada ya mkutano uliofanyika Anatouglou-Ilala, jijini Dar es Salaam, aliitwa polisi mara nne ambapo alihojiwa na alipoonekana hana majibu, aliruhusiwa.

“Mimi ni mwakilishi wenu kwa hiyo yote yanayofanyika Kariakoo, nimebeba dhamana. Mimi mmenituma nyie, nimebeba mawazo yenu kwa uwakilishi wenu, sikuwa mwoga, nilisimama kwenye kile ninachokiamini uwazi na ukweli,” amesema Mbwana.

Pia amesema wakifungua maduka watakuwa wamemuonyesha Rais Samia Suluhu Hassan kuwa walikuwa na shida hiyo iliyoshughulikiwa.

“Siwalazimishi mkiridhia kufunga maduka sina tatizo na mkifungua mtakuwa mmeniheshimisha mwenyekiti na kuonyesha mnaimani na mimi,”amesema Mbwana.

Mjumbe mwingine aliyekuwa mwakilishi Dodoma (hakutaja jina), amesema kuendelea kufunga maduka yao si salama kwa afya zao, biashara na uzima wa nchi.

Amesema kweli wanashida, lakini Serikali imeamua kuwasikiliza, hivyo wafungue maduka na waendelee kufanya shughuli zao na kwa yale ambayo hayajafanyika yatakapoonekana bado kulegalega na mzigo ubaki kwa Serikali.

“Hili ni la mwisho, mkifeli hapa kwa Serikali sisi tusilaumiwe na kweli wametuahidi kutekeleza waliyotuahidi, hivyo nawaomba ndugu zangu hili tulifanye la mwisho tufungue maduka yetu,” amesema mfanyabiashara huyo.

Kutokana na kauli hiyo ya mwenyekiti, baadhi ya wafanyabiashara wameonekana kutoridhishwa na kile kilichozungumzwa, huku wakisema kilichoelezwa ni kimoja wakati wana changamoto zaidi ya hiyo.

Stanley Shayo, amesema walitegemea kiongozi wao atakuja na majibu ya kuwaridhisha, ili wafungue maduka lakini kwa kiasi kikubwa ameongea kisiasa.

“Tulichokuwa tunatarajia ni kuelezwa yale tunayoyalilia, lakini wamekuja na jambo moja ambalo tulishaelezwa muda mrefu. Hili tunaona tumeletewa siasa na viongozi wetu,” amesema.

Mfanyabiashara wa viatu, George Matheo amesema kinachoonekana kwa sasa kama wafanyabiashara kuna watu wanawashinikiza kufunga maduka, jambo ambalo halina ukweli.

“Tumewasikiliza viongozi na wajumbe, lakini kama wamekuja na mamuzi yao na ndiyo maana hawajatupa nafasi ya kuuliza wala kuongea, jambo ambalo linafanyika kihuni kwa upande wetu,” amesema.