Majibu ya CCM kwa ACT-Wazalendo kuhusu mikopo ya Serikali

Unguja. Baada ya Chama cha ACT-Wazalendo kusema Serikali imejikita kukopa badala ya kubuni vyanzo vya mapato na hivyo kuliweka Taifa katika hatari ya madeni, Chama cha Mapinduzi (CCM) kimesema Serikali inakopa kwa masilahi ya wote na lazima ifanye hivyo ili kutekeleza miradi ya maendeleo.

Juni 23, 2024 akihutubia mkutano wa hadhara katika uwanja wa Kwa Mwarabu Magogoni, Mwenyekiti wa ACT-Wazalendo Taifa, Othman Masoud alisema Zanzibar inakopa kwa sababu ya kukosa maono ya viongozi, lakini kwa rasilimali ilizonazo haistahili kuingia kwenye madeni.

Kwa sasa deni la Taifa ni Sh1 trilioni. Hata hivyo, akiwasilisha bajeti ya Serikali hivi karibuni, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Fedha na Mipango, Dk Saada Mkuya alisema bado deni hilo ni himilivu na hakuna nchi inaweza kuendelea kwa kutegemea fedha zake za ndani.

Akizunguza akiwa ziarani katika Tawi la CCM Mafufuni Bumbwini, Juni 26, 2024 Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar, Dk Mohamed Said Dimwa amesema kauli za wanasiasa wa upinzani kuilaumu Serikali kuhusu mikopo inatakiwa kupuuzwa.

“Fedha hizo ni kwa ajili ya kuimarisha miradi ya maendeleo ikiwamo ujenzi wa miundombinu ya barabara za lami, majisafi na salama, ujenzi wa shule za kisasa, hospitali, viwanja vya ndege vya kisasa, na bandari za kisasa,” amesema Dk Dimwa.

Amesema katika bajeti ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) ya mwaka 2024/25 iliyopitishwa hivi karibuni, zaidi ya asilimia 63 ya fedha za bajeti hiyo zimeelekezwa kuimarisha miradi ya maendeleo kwa ajili ya kukabili changamoto za wananchi wote wa mijini na vijijini.

“Suala la kukopa fedha kwa ajili ya maendeleo si la Zanzibar tu, wala Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, bali nchi mbalimbali duniani zinakopa na kwa mujibu wa takwimu kutoka Shirika la Fedha Duniani (IMF) nchi zilizoendelea kiuchumi mfano Marekani, Urusi (Russia), Ufaransa na zingine ndiyo zenye madeni makubwa,” amesema.

Amesema, “Hivyo, hao wanasiasa nawashauri wajiongeze kwa kufanya utafiti kujua mwenendo wa uchumi wa dunia unaendaje.”

Amewataka wanachama wa CCM na Jumuiya zake kwa ngazi za mashina na matawi kufanya vikao vya mara kwa mara kujadili maendeleo, changamoto na mikakati ya pamoja ya kuimarisha taasisi hiyo.

Dk Dimwa amewasihi viongozi, watendaji na wanachama kwa ujumla kuhamasisha wananchi na wafuasi wa vyama vya upinzani kujiunga na CCM ili kuongeza idadi ya wapigakura wa chama hicho.

Katibu wa Kamati Maalumu ya NEC, Idara ya Oganazesheni CCM Zanzibar, Omar Ibrahim Kilupi amewasisitiza wanachama hao kuhakikisha wanapata kadi za mpigakura wawe na uhalali wa kukipigia kura nyingi chama hicho.