Nairobi. Waandaaji wa maandamano nchini Kenya wametoa wito wa maandamano mapya ya amani kupinga ongezeko la kodi, huku idadi ya waliofariki dunia kutokana na maandamano ya nchi nzima ikiongezeka hadi 13, ofisa kutoka chama kikuu cha madaktari ameiambia AFP.
Maandamano hayo yanayoongozwa na vijana yalianza kwa amani wiki iliyopita, huku maelfu ya watu wakiandamana kote nchini humo kupinga ongezeko la kodi, lakini hali ya wasiwasi iliongezeka Jumanne Juni 25, 2024, huku polisi wakifyatua risasi kwa waandamanaji waliovamia jengo la Bunge.
Matukio hayo ambayo hayakuwahi kushuhudiwa, yaliacha sehemu za Bunge zikiwaka moto na kuteketea na watu wengi kujeruhiwa, hali iliyowashtua Wakenya na kusababisha Serikali ya Rais William Ruto kupeleka jeshi.
Jana, Juni 25, 2024, Bunge lilipitisha muswada tata ulio na nyongeza ya kodi ambao lazima usainiwe na Rais Ruto, ili kuwa sheria.
Hata hivyo, waandamanaji wameapa kuingia barabarani tena Alhamisi Juni 27, 2024 huku wakitaka muswada huo utupiliwe mbali.
“Kesho tunaandamana kwa amani tena, tutavaa nguo nyeupe kwa ajili ya watu wetu wote waliokufa,” amesema mratibu wa maandamano, Hanifa Adan kwenye ukurasa wake wa X na kuongeza kuwa,“Huwezi kuua sisi sote.”
Waandamanaji wamesambaziana kaulimbiu ya “Tupatane Thursday” (Tukutane Alhamisi), pamoja na hashtag ya #Rejectfinancebill2024 kwenye mitandao ya kijamii.
“Serikali haitujali kwa sababu walitupiga risasi za moto,” Steve (40) aliyekuwa bungeni Jumanne iliyopita, ameiambia AFP.
“Ruto “alidhulumu watu wasio na hatia,” amesema na kuongeza kwamba ataandamana Alhamisi: “Ninatarajia vurugu na machafuko zaidi.”
Simon Kigondu, Rais wa Chama cha Madaktari nchini Kenya, ameiambia AFP: “Hadi sasa tuna watu 13 waliouawa, lakini hii si idadi ya mwisho.”
Ameongeza kuwa hajawahi kuona kiwango kama hicho cha vurugu dhidi ya watu wasio na silaha.
Ofisa katika Hospitali ya Taifa ya Kenyatta jijini Nairobi amesema leo kwamba matabibu walikuwa wakiwatibu watu 160, baadhi yao wakiwa na majeraha madogo, wengine wakiwa na majeraha ya risasi.
Huko mtandaoni, waandaaji wa maandamano hayo wameshiriki jitihada za kuchangisha fedha, ili kuwasaidia waliojeruhiwa kwenye maandamano.
Jana jioni (Jumanne), Ruto alionya kwamba Serikali yake itachukua hatua kali dhidi ya vurugu na machafuko, akiwafananisha baadhi ya waandamanaji na “wahalifu”.
“Siyo utaratibu au hata kufikirika kwamba wahalifu wanaojifanya wanaandamana kwa amani wanaweza kufanya ugaidi dhidi ya wananchi, wawakilishi wao waliowachagua na taasisi zilizoanzishwa kwa mujibu wa Katiba yetu na kutarajia kuachwa huru,” alisema.
Muda mfupi kabla ya hotuba yake, Waziri wa Ulinzi Aden Bare Duale alitangaza kuwa jeshi limeruhusiwa kuingia mtaani, ili kukabiliana na “dharura ya kiusalama” nchini humo.
Polisi wengi wamesambaa kuzunguka Bunge mapema leo Jumatano Juni 26, 2024, kwa mujibu wa ripota wa AFP, huku harufu ya mabomu ya machozi ikiwa bado hewani.
Polisi aliyesimama mbele ya vizuizi vilivyovunjwa kwenye jengo hilo, ameliambia Shirika la Habari la AFP kuwa alikuwa ametazama matukio hayo yakitokea kwenye runinga.
“Ilikuwa ni wazimu, tunatumaini leo itakuwa shwari,” amesema.
Katikati ya jiji la Nairobi ambako maandamano hayo yalikithiri, wafanyabiashara walikuwa wakiangalia uharibifu.
“Hawakuacha chochote, maboksi tu. Sijui itanichukua muda gani kupona,” James Ng’ang’a, ambaye duka lake la vifaa vya kielektroniki liliporwa, ameiambia AFP.
Utawala wa Rais Ruto umeshangazwa na kasi ya upinzani dhidi ya ongezeko la kodi.
Wakati mikutano ya hadhara, inayoongozwa zaidi na vijana, Gen-Z, imekuwa ya amani kwa kiasi kikubwa, hali ya wasiwasi iliongezeka kwa kasi Jumanne alasiri wakati maofisa walipoanza kufyatua risasi kwenye umati wa watu karibu na Bunge.
Waandamanaji walivunja vizuizi vya Bunge na kuvamia jengo hilo ambalo kwa kiasi fulani lilikuwa limewaka moto, huku runinga ikionyesha samani zilizoungua na kuvunja madirisha.
Waandishi wa habari wa AFP waliwaona watu watatu wakivuja damu nyingi na wakiwa wamelala chini bila kutikisika.
Machafuko hayo yameitia wasiwasi jumuiya ya kimataifa, huku zaidi ya mataifa 10 ya Magharibi ikiwemo Marekani yakisema “yameshtushwa hasa na matukio yaliyoshuhudiwa nje ya Bunge la Kenya.”
Waangalizi wa haki pia wameshutumu mamlaka kwa kuwateka nyara waandamanaji.
Malalamiko ya muda mrefu kuhusu kupanda kwa gharama ya maisha yaliongezeka wiki iliyopita wakati wabunge walipoanza kujadili muswada huo wenye nyongeza ya ushuru.

Serikali ya Kenya yenye uhaba wa fedha, inasema ongezeko hilo la kodi zinahitajika, ili kuhudumia deni kubwa la nchi la Ksh10 trilioni (dola bilioni 78), sawa na takriban asilimia 70 ya Pato la Taifa la Kenya.
Hazina hiyo imeonya kuhusu upungufu wa bajeti ya Ksh 200 bilioni, kutokana na uamuzi wa Ruto wiki iliyopita kurudisha nyuma baadhi ya viwango vya kodi vilivyokumbwa na utata.
Wakati Kenya ikiwa miongoni mwa mataifa yenye uchumi unaoendelea zaidi Afrika Mashariki, theluthi moja ya wakazi wake milioni 52 wanaishi katika umaskini.