AKILI ZA KIJIWENI: Kwa Mzamiru, Mwenda Simba imefanya la maana

WIKI hii Simba ilitangaza kuongeza mikataba ya nyota watatu wazawa wanaokichezea kikosi hicho ambao mikataba yao ya awali ilikuwa imefikia tamati mwishoni mwa msimu wa 2023/2024.

Watatu hao ni mshambuliaji Kibu Denis, kiungo mkabaji, Mzamiru Yassin na beki kiraka, Israel Mwenda ambao kila mmoja amesaini mkataba mpya wa kuitumikia Simba kwa miaka miwili zaidi.

Suala la Kibu kutangazwa kuongeza mkataba mpya halikuwa habari mpya kwani kabla ya hapo ilishasambaa taarifa kwa muda mrefu, Simba itabaki na nyota huyo msimu ujao baada ya mshambuliaji huyo kupiga chini ofa kadhaa ambazo zilimfikia kutoka timu nyingine.

Lakini kwa Mzamiru na Mwenda ni jambo ambalo linaweza kuwa mjadala mpya kwa vile kulikuwa na tetesi kuwa wawili hao ni miongoni mwa wachezaji waliokalia kuti kavu katika dirisha hili la usajili.

Kuwabakisha Mwenda, Mzamiru na Kibu ni jambo la maana sana ambalo Simba imelifanya na kama isingefanya hivyo ingejifelisha kwa kiasi kikubwa.

Hao ni wachezaji wazuri wazawa ambao kama wangeondoka, Simba ingepata kazi ngumu katika kuziba mapengo yao maana nchi kwa sasa Ina uhaba wa wachezaji wa nyumbani ambao wana ubora mkubwa wa kuweza kuibeba timu kama Simba.

Lakini wana uzoefu wa maisha katika klabu hiyo na wa kimataifa, kwani wote kwa nyakati tofauti wamecheza timu ya taifa ‘Taifa Stars’ na pia wamecheza mechi nyingi za kimataifa za mashindano ya klabu Afrika.

Katika soka, usajili bora zaidi ni ule wa kubakisha wachezaji wako bora kwenye timu maana sio rahisi kwa kila mchezaji mpya kuweza kuingia kwenye timu na kumudu kwa haraka staili ya kiuchezaji lakini pia hata mazingira yake mapya.

Hivyo Simba wametumia akili kubwa kwa kufanikiwa kuwashawishi watatu hao waongeze  mkataba wa kuendelea kuichezea msimu ujao na utakaofuata baada ya hapo.

Related Posts