Dar es Salaam. Shahidi wa pili katika kesi ya ukahaba inayowakabili washtakiwa watano katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Sokoine Drive, ameileza mahakama hiyo kuwa waliwakamata washtakiwa hao kwa tuhuma za ukahaba kutokana na viashiria vya aina ya mavazi waliyokuwa wameyavaa na muda na mahali walikokutwa na polisi.
Hata hivyo, shahidi huyo ambaye ni askari kutoka Kituo cha Polisi Mburahati, WP Konstebo wa Polisi (PC), Tunusuru Malungula, alijikuta katika wakati mgumu alipotakiwa kueleza maana ya umalaya au ukahaba kutokana na viashiria hivyo alivyovitaja.
Ilikuwa ni wakati wa maswali ya dodoso aliyoulizwa na mawakili wa utetezi katika kesi hiyo, Peter Madeleka, Jebra Kambole na Maria Mushi, leo Alhamisi Juni 27, 2024, mpaka akasema kuwa hajui maana ya ukahaba.
Pia, amesema hajui kama kuna sheria inayobainisha sifa za mavazi yanayoashiria ukahaba wala inayoweka muda ambao mtu akikutwa barabarani anakuwa anajihusisha na ukahaba.
Shahidi huyo pia alitakiwa kueleza kama washtakiwa walikuwa wakiuza miili yao, wao walibaki na nini na wateja walioinunua wako wapi.
Washtakiwa katika kesi hiyo inayosikilizwa na Hakimu Mfawidhi Rachael Kasebele ni Mariam Yusufu Mkinde (25) mkazi wa Magomeni, Mwazani Nassoro (25) mkazi wa Kigogo, Mwanaidi Salum (25) mkazi wa Mabibo, Faudhia Hassan (35) mkazi wa Ubungo na Tatu Omary (40) mkazi wa Ubungo.
Katika kesi hiyo ya jinai namba 17277/2024, washtakiwa hao wanakabiliwa na shtaka moja la kufanya vitendo vya aibu mbele ya hadhara kwa ajili ya kufanya umalaya, kinyume na kifungu cha 176 (a) cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu, Sura ya 16, marejeo ya mwaka 2022.
Wanadaiwa kuwa Juni 17, eneo la Manzese Tip Top, Wilayani Ubungo, Dar es Salaam, walikutwa wakifanya vitendo vya aibu mbele ya hadhara kwa kusimama hadharani, wakiwa wamevaa mavazi yasiyo ya heshima kwa lengo la kufanya umalaya.
Awali, katika ushahidi wake wa msingi akiongozwa na waendesha mashtaka wawili kwa zamu, Mawakili wa Serikali Winfrida Ouko na Tumaini Mafuru, PC Tunusuru alieleza kuwa washtaakiwa polisi liwakamata washtakiwa hao Juni 17, 2024, wakati wakiwa katika doria yeye na wenzake watano.
PC Tunusuru ameieleza mahakama kuwa waliwakamata muda wa saa tisa usiku eneo la Manzese Tip Top, Mtaa wa Midizini, ambapo waliwaona vema kwa kuwa walikuwa wamesimama eneo la biashara palipokuwa na mwanga na kwamba kilichofanya wakawakamata ni viashiria vya ukahaba.
Amevitaja viashiria hivyo kuwa ni aina ya mavazi yasiyo ya heshima waliyokuwa wamevaa, muda na kitendo cha kuanza kukimbia baada ya kuwaona askari.
“Mfano, Mwadhani alikuwa amevaa nguo aina ya tight nyepesi sana ambayo ilikuwa imemchora maumbile,” ameeleza shahidi huyo na kuwa walipowahoji kwa nini wanafanya hivyo, kila mmoja alitoa sababu zake na wengine wakidai hawapendi bali ni kwa sababu wanategemewa.
Shahidi huyo amewatambua mahakamani huku akiieleza mahakama kuwa amefanikiwa kuwatambua kwa kuwa alikutana nao muda mrefu, kwani baada ya kuwakamata waliwapeleka Kituo cha Polisi Mburahati na kuendelea na taratibu nyingine za kuchukua taarifa zao.
Baada ya maelezo hayo, ndipo shahidi huyo akaulizwa maswali kutoka kwa mawakili wa utetezi, kuhusu ushahidi wake.
Wakili Madeleka: Shahidi hebu ikumbushe Mahakama dini yako, umesema ni dini gani?
Wakili: Kwa sababu wewe ni Muislam umeapa kwa Kuran na unaiamini, hebu ieleze Mahakama Surat Yasin (Sura ya Sita) inasemaje?
Wakili: Umesema wewe ni askari polisi, ni sahihi?
Wakili: Askari polisi anatambulika kwa sare na kitambulisho cha kazi ni sahihi?
Wakili: Na kwamba nje ya hizo njia mbili haiwezekani kumtambua askari?
Wakili: Jeshi la Polisi huwa linatoa vitambulisho kwa askari wake, ni sahihi?
Wakili: Wewe hapa umevaa sare za polisi?
Wakili: Umemwonyesha mheshimiwa hakimu kitambulisho?
Wakili: Shahidi, mheshimiwa hakimu mnafahamiana?
Wakili: Kwa hiyo ukimwambia tu kuwa wewe ni polisi kwa hivyo ulivyo, atakuamini?
Wakili: Umemwambia mheshimiwa hakimu kwamba washtakiwa hawa walikamatwa na polisi waliokuwa doria ukiwemo wewe, ni sahihi?
Wakili: Kwa kuwa umesema kwa hivyo ulivyo ni vigumu mheshimiwa hakimu kukuamini kuwa wewe ni askari, je unataka Mahakama isiamini kuwa wewe ulishiriki kuwakamata hawa washtakiwa?
Wakili: Ulisema ulikwenda kuwakamata mkiwa askari sita na umewataja Afande Peter, Jackson Masali na …, ni sahihi kwamba hakuna askari polisi mwenye jina moja, ila mawili au matatu waliyotumia katika kuwaajiri?
Wakili: Ni sahihi kwamba kwenye Jeshi la Polisi kuna askari wengi wanaitwa Peter?
Wakili: Sasa hawa askari wewe uliowataja kwa jina moja ni askari polisi ambao kweli wana majina mawili au matatu kama ulivyosema?
Wakili: Wewe binafsi ulishiriki kumkamata nani kati ya hawa?
Wakili: Unakumbuka hawa wengine waliobaki walikamatwa na nani?
Wakili: Unakubaliana na mimi kwa mujibu wa sheria za Polisi mtuhumiwa mwanamke anapaswa kukamatwa na askari mwanamke?
Wakili: Na mwanamke akikamatwa na askari mwanaume ni udhalilishaji, si ndiyo?
Wakili: Na timu ya ukamataji askari, wanawake walikuwa wawili tu, si ndiyo?
Wakili: Kwa kuwa wewe ulimkamata mmoja tu, Mwazani, mwambie mheshimiwa hakimu, hawa wengine walikamatwa na nani?
Shahidi: Walikamatwa na wale askari wengine akiwemo na Masaji (mwanamke), walikamatwa na Masali
Wakili: Umesema viashiria vya ukahaba ni kwamba baadhi walipowaona walianza kukimbia na umesema wengine wote walikamatwa na Masali, ina maana Masali alikuwa anawakimbiza mmoja mmoja, anamkamata anamleta huku wengine wanaendelea kukimbia, kisha anawakimbilia na kuwakamata?
Wakili: Mlikuwa na warrant of arrest (kibali cha ukamataji)?
Wakili: Wakati ukiongozwa na wakili wa Serikali (kutoa ushahidi) ulimwambia mheshimiwa hakimu kuwa ukamataji huo mlifanya kwa warrant of arrest?
Wakili: Kwa hiyo warrant ilikuwa na majina ya watuhumiwa?
Wakili: Hiyo warrant umeiona hapa mahakamani?
Wakili: Ulimwambia mheshimiwa hakimu kuhusu hiyo RB?
Wakili: Mtuhumiwa akikamatwa akifikishwa Polisi huwa anandika maelezo, na waliomkamata huwa wanashiriki kuandika maelezo yao, uliandika maelezo ya hao watuhumiwa?
Wakili: Wewe uliandika maelezo yako kama mkamataji?
Wakili: Sasa kama hukuandika wewe hujavunja Sheria?
Wakili: Umesema viashiria vya kwamba walikuwa ni makahaba vilikuwa nini na nini?
Wakili: Kwa hiyo viashiria vya umalaya ni mavazi na muda, sawa?
Wakili: Kuhusu kiashiria cha mavazi ulisema ni mmoja tu aliyekuwa amevaa kitopu, kwa hiyo hao wengine uliwaonea (kuwakamata)?
Wakili: Hicho kitop umekiona hapa mahakamani, yaani hapa mahakamani hicho kitopu kipo?
Wakili: Kwa hiyo hilo la kitop ni hadithi zako tu?
Shahidi: Hapana sio hadithi zangu.
Wakili: Umesema moja ya majukumu yako ni kulinda sheria, na bila shaka unazijua hizo sheria?
Wakili: Hebu ieleze mahakama ni sheria gani inasema kuvaa kitop ni umalaya?
Wakili: Umesema vazi lingine ni tight (taiti) nyepesi, umeileta hapa mahakamani?
Wakili: Askari anapotoka kwenda kwenye operesheni huwa anaandika majina yake kwenye OB (kitabu cha matukio), ni sahihi?
Wakili: Wewe uliandika majina yako kwenye OB?
Wakili: OB ni moja ya vitendea kazi vyako muhimu, ni sahihi?
Wakili: Unawezaje kusahau kitendea kazi chako muhimu, ambacho unakitumia kila siku lakini ukakumbuka majina ya washtakiwa na vitopu, huoni wewe ni muongo?
Wakili: Mlipotoka nao huko mlikowakamata na mkawapitisha CRO (chumba cha mashtaka Kituo cha Polisi) mlikowakabidhisha, mliwakabidhisha kwa utaratibu gani?
Wakili: Pia hukumbuki kama waliandikishwa katika OB?
Wakili: Hiyo OB umeileta hapa mahakamani?
Wakili Kambole: Shahidi wewe hukumkamata Mariam (mshtakiwa wa kwanza) ni, sahihi?
Wakili: Kwa hiyo hujui Mariam alivaa nguo gani?
Wakili: Umesema mlikuwa na arrest warrant, ilikuwa na majina haikuwa na majina?
Wakili: Shahidi unaweza kutusaidia hapa mahakamani umalaya maana yake ni nini?
Hakimu: Hujui maana ya umalaya?
Shahidi: Ni kujihusisha na ukahaba
Shahidi: Ni moja ya viashiria vya umalaya.
Wakili: Kwa hiyo ukahaba ni moja ya viashiria vya umalaya na umalaya ni nini?
Shahidi: Ni vitendo vya kujihusisha na ukahaba.
Wakili: Kwa mujibu wa sheria gani?
Wakili: Kwa hiyo wewe ulikuwa unatekeleza sheria ambayo wewe huijui?
Shahidi: Hapana, sababu sheria inakataza vitendo vya umalaya
Wakili: Shahidi, umesema kiashiria kingine cha kuwakamata kwa ukahaba ni muda, kwani ni kuanzia saa ngapi mtu akitembea barabarani anakuwa anafanya umalaya?
Wakili: Kwa kuwa hujui, utakubaliana na mimi kwamba muda si kiashiria cha umalaya?
Shahidi: Sitaweza kukubaliana na wewe
Wakili: Haya mwambie Mheshimiwa ni kuanzia saa ngapi?
Shahidi: Nimeshasema sijui.
Wakili: Hawa washtakiwa walikamatwa saa ngapi?
Wakili: Wewe unajua walikuwa wanakwenda au wanatoka wapi?
Wakili: Utakubaliana na mimi kuwa wakati unaongozwa na wakili wa Serikali hukusema kama walikuwa wamesimama na mwanaume au hawakuwa wamesimama na wanaume?
Shahidi: Sijaulizwa, sikuwaona.
Wakili: Wakati unatoa maelezo yako ulisema baada ya kuwakamata mliwauliza kwa nini wanafanya hivyo, mwingine akasema anategemewa na mwingine kwamba sio kupenda kwake, hayo maelezo kuna sehemu uliyaandika?
Wakili: Kwa hiyo hakuna ushahidi huo?
Wakili: Utakubaliana na mimi kuvaa vitopu si kosa la jinai?
Shahidi: Ni kosa maana si nguo za heshima
Wakili: Kwa mujibu wako nguo za heshima ni zipi?
Shahidi: Zinazofunika maumbile
Wakili: Kuna Sheria inayotoa mwongozo wa mavazi?
Wakili: Hilo unalolisema ni kwa mujibu wa nini?
Wakili: Shahidi, ni sahihi kwamba hawa washtakiwa hata kama uliwakamata ni kwa mara ya kwanza ndio uliwaona ulipowakamata?
Wakili: Utakubaliana na mimi kwamba hujui pale walikuwa wamekaa kwa muda gani?
Wakili: Shahidi kwa mara ya kwanza umesema uliwaona saa tisa na hujui walikuwa wamekaa kwa muda gani, na kama walikuwa wanapita au?
Wakili: Walikaa kwa muda gani pale?
Wakili: Lakini pia wewe hujui ni nini hasa walikuwa wanafanya pale?
Shahidi: Walikuwa wanajihusisha na vitendo vya umalaya.
Wakili: Wakati Wakili wa Serikali anakuongoza ulisema kuwa walimuuzia nani (miili)?
Wakili: Unajua walimuuzia nani?
Wakili: Unajua walimuzia shilingi ngapi?
Wakili: Unajua walikuwa wanauza sehemu gani ya miili yao?
Wakili: Hiyo miili yao walikuwa wanauzia hapo barabarani?
Wakili: Wakati wanauza hiyo miili wewe ulikuwa umekaa sehemu gani?
Wakili: Wao wakiuza miili wanabaki na nini?
Wakili: Umemwambia mheshimiwa hakimu kwamba viashiria ni mavazi kwa kuwa mmojammoja walivaa nguo gani?
Wakili: Umesema walikuwa wanauza miili, wanunuzi wako wapi?
Wakili: Nakuuliza, wanunuzi wako wapi hapa?
Wakili: Hao wanunuzi mliwakamata au hamkuwakamata?
Shahidi: Sijui, sikumbuki
Wakili: Kwa hiyo ni sahihi tukihitimisha kuwa wauzaji walikamatwa na wanunuzi hawakukamatwa?
Wakili: Ni sahihi kwamba hamkuwakamata kwa sababu kununua sio kosa?
Wakili Maria Mushi: Ulisema mliwakamata hawa washtakiwa kwa sababu walikuwa hawajavaa nguo za heshima, kuna sheria gani ambayo inazungumzia kuwa nguo za heshima ni zipi?
Wakili: Kwa hiyo heshima kwa mtu mmoja sio lazima iwe heshima kwa mtu mwingine?
Wakili: Kwa hiyo wewe uliona si nguo za heshima lakini inawezekana mimi ningeweza kuona ni nguo za heshima?
Wakili: Unawafahamu Wamasai?
Wakili: Unajua utamaduni wa mavazi yao?
Wakili: Unajua mavazi yao wengine huwa wanaacha mapaja wazi?
Wakili: Kwa hiyo hayo mavazi yao ni heshima au si heshima?
Shahidi: Sijawahi kuwaona.
Kesi hiyo itaendelea kesho Ijumaa Juni 28, 2024