Maagizo ya Makamu wa Pili wa Rais akiahirisha Baraza la Wawakilishi

Unguja. Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Hemed Abdulla amesema Serikali inaendelea kuhakikisha inadhibiti bidhaa kupanda bei, ili kuwapunguzia makali ya maisha wananachi.

Akiahirisha Mkutano wa 15 wa Baraza la Wawakilishi leo Alhamisi Juni 27, 2024 amesema uzoefu unaonyesha wafanyabiashara hupandisha bei kiholela.

Ameutaka uongozi wa Wizara ya Biashara na Maendeleo ya Viwanda kufuatilia kwa karibu suala la bei elekezi na kuchukua hatua kali kwa mujibu wa sheria kwa kila atakayebainika kwenda kinyume cha agizo la Serikali.

Amesema Serikali inaendelea kufanya jitihada katika kuwapunguzia gharama za ukali wa maisha wananchi, hususan kwa kuhakikisha bidhaa za chakula, nguo na zote za muhimu zinapatikana kwa bei nafuu.

“Serikali inawataka wafanyabiashara kuwa wazalendo kwa kutopandisha bei kiholela, kwani kunasababisha ugumu wa maisha kwa wananchi,” amesema.

Pia ameuagiza uongozi wa Ofisi ya Rais, Kazi, Uchumi na Uwekezaji kushirikiana na Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi kuhakikisha wananchi wanapata mikopo bila usumbufu wa aina yoyote.

“Nauagiza uongozi wa Wizara ya Maji, Nishati na Madini pamoja na taasisi zake, zikiwemo mamlaka ya maji na Shirika la Umeme kuongeza juhudi za utendaji katika huduma wanazozitoa za upatikanaji wa maji na umeme wa kutosha,” amesema.

Pia ameagiza viongozi wa Wizara ya Afya kuwasimamia watendaji wa wizara, wakiwemo madaktari na wauguzi kufanya kazi na kutoa huduma bora kwa manufaa ya wananchi.

Amesisitiza usimamizi mzuri wa kampuni binafsi zinazotoa huduma katika hospitali za Serikali kuhakikisha huduma bora zinatolewa.

Maagizo mengine ni kwa Mamlaka ya Kuzuia Rushwa na Uhujumu Uchumi Zanzibar (ZAECA) kufuatilia kwa karibu na kuchukua hatua zinazostahili kisheria kwa wazabuni wanaochelewa kukamilisha miradi wanayopewa na Serikali kwa kuzingatia mikataba iliyopo.

Hemed pia ameuagiza ongozi wa Ofisi ya Rais, Fedha pamoja na taasisi zinazohusika na ukusanyaji wa mapato kusimamia ukusanyanyaji wa kodi za Serikali kwa utaratibu wa kisheria.

“Nauagiza uongozi wa Ofisi ya Rais Kazi, Uchumi na Uwekezaji kuwapatia elimu wawekezaji kuhakikisha wanazingatia sheria za nchi, wakati wa utekelezaji wa miradi yao,” ameagiza.

Mbali ya hayo, ameagiza maofisa masuuli wa wizara na taasisi za Serikali kusimamia vyema matumizi ya fedha kwa malengo yaliyokusudiwa, ili kuondoa hoja nyingi za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali katika taasisi.

Wakuu wa mikoa wametakiwa kusimamia amani kwa kuhakikisha wahalifu wanakamatwa na kufikishwa kwenye vyombo vya sheria, wakiwamo wanyang’anyi wanaotumia silaha.

“Jeshi la Polisi na Mamlaka ya Usafiri na Usalama Barabarani waendelee kuwachukulia hatua wale wote wanaovunja sheria na kuhatarisha usalama wa barabarani, kwani Serikali imekuwa ikiendeleza juhudi za kuimarisha miundombinu kupunguza athari zinazotokana na ajali,” amesema.

Amesema Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) zimeandaa mwongozo wa kitaifa wa matumizi ya matokeo ya Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2022.

Kutokana na hilo, amezitaka wizara, taasisi za Serikali na binafsi, na wadau wote wa takwimu kutumia mwongozo huo katika kupanga mipango ya maendeleo na utekelezaji wa shughuli zote za Serikali.

Amesema kwa kipindi cha kuanzia mwaka 2020/2021 hadi Mei, 2024 imeshuhudiwa ongezeko kubwa la ukusanyaji wa mapato kutoka Sh719.33 bilioni hadi Sh1.297 trilioni.

Amesema ongezeko hilo linatokana na juhudi za Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi za kuimarisha mifumo ya usimamizi wa fedha na uendeshaji wa shughuli za Serikali.

“Nitumie fursa hii kutoa wito kwa wananchi kuendelea kutoa risiti na kudai risiti za kielektroniki kwa kila anayepatiwa huduma sambamba na kulipa kodi kwa hiari, ili kuongeza kasi ya ukuaji wa uchumi na Pato la Taifa,” amesema.

Related Posts