Mwanza. Mgomo wa wafanyabiashara wa maduka jijini Mwanza umeingia siku ya tatu huku waendesha maguta, madereva wa malori ya mizigo, mama lishe na wabeba mizigo wakihofia ndoa na familia zao kusambaratika kutokana na hali ngumu ya maisha.
Mgomo huo ulianza Dar es Salaam Juni 24, 2024, ambapo wafanyabiashara walifunga maduka yao kushinikiza Serikali kuondoa utitiri wa kodi. Hatua hii iliendelea kuenea hadi Mwanza, Mbeya, Dodoma, Mtwara, Iringa, Arusha na mikoa mingine.
Dereva wa gari dogo la mizigo katika Mtaa wa Liberty, Ndaluka Kamata amesema kabla ya mgomo alikuwa akipata hadi Sh50,000 kwa siku, lakini sasa hali imebadilika kiasi cha kukosa hata Sh5,000 kwa siku.
“Familia yangu inateseka, siku ya tatu sijapewa unyumba na mke wangu anataka kukimbia. Watoto wanateseka na njaa kila siku,” amesema Ndaluka.
Katibu wa Umoja wa Waendesha Maguta mkoa wa Mwanza, Zebedayo Joseph amesema athari za mgomo huo ni kubwa na zinaweza kusambaratisha familia.
“Familia inategemea umeenda kutafuta riziki, lakini unaporudi bila hela, inakuwa vigumu kueleweka nyumbani,” amesema Joseph.
Msukuma mkokoteni, Luhinda Sulle, ameeleza kusikishwa na kutokana na mgomo huo akisema kwa siku tatu hajapata hata Sh1, 000 na sasa anawaza wapi atapata fedha za kununua madaftari ya watoto wake watatu wanaotarajia kufungua shule Jumatatu, Julai 1, 2024.
“Familia yangu inateseka. Kwa kawaida naweza kupata hadi Sh20,000 kwa siku, lakini sasa sijapata hata hela za kuiachia familia yangu,” amesema Sulle.
Mama lishe, Mwamvua Shaban, amesema amelazimika kupunguza kipimo cha mapishi kwa kukosa wateja.
Awali alikuwa anatumia kilo nne za ngano kutengeneza chapati, sasa anapika kilo mbili tu nazo haziishi. Pia alikuwa akipika kilo sita za mchele na kilo 10 za ubnga kwa ajili ya ugali, lakini sasa amelazimika kusitisha biashara hiyo kwa sababu hakuna wateja wa mchana.
Kwa upande mwingine, baadhi ya wafanyabiashara wameamua kufungua maduka yao kwa siri. Muuzaji wa vifaa vya kielektroniki, John Bigangoma amesema mgomo huo umemuathiri kibiashara kwani wateja waliokuwa wameagiza bidhaa hawakuzipata kwa wakati, jambo lililosababisha baadhi yao kusitisha makubaliano.
Hali pia ni ngumu katika manispaa ya Songea, ambapo wananchi na wafanyabiashara kutoka mataifa jirani wameomba mgomo huo kumalizwa haraka.
Agness Joseph, mkazi wa Songea, amesema ameshindwa kununua vifaa vya ujenzi. Dorcas Banda, raia wa Malawi, amesema mgomo huo umewaathiri sana wananchi wa nchi jirani ambao wanafika Ruvuma kununua mahitaji mbalimbali.
Katika manispaa ya Morogoro, mama lishe Mariam Mbuge amesema mgomo huo umesababisha kukosa wateja katika biashara yake.
Awali nilikuwa napata Sh40, 000 kwa siku, lakini sasa sidhani kama naweza kupata Sh20,000. Nina wafanyakazi watatu wanaonisaidia kusambaza chakula kwa wafanyabiashara wa maduka ya bidhaa za jumla,” amesema Mariam.
Mkusanya ushuru wa magari, Asha Bakari, amesema mapato ya ushuru wa maegesho ya magari nayo yamepungua kutokana na mgomo huo.
“Nilikuwa nikikusanya Sh100, 000 hadi Sh120,000 kwa siku, lakini sasa sidhani kama nitafikia lengo hilo,” amesema Asha.
Naye Said Omary, msukuma mkokoteni amesema amekuwa akitegemea kupata fedha kwa kubeba mizigo kutoka Nunge na kupeleka katika magari yanayoenda vijijini.
“Ningeomba Serikali na wafanyabiashara kukaa meza moja ili maisha yaendelee. Mgomo huu hauna faida kwa wananchi,” amesema.
Imeandikwa na Mgongo Kaitira (Mwanza), Juma Mtanda (Morogoro) na Joyce Joliga (Songea).