Mashindano ya Kombe la Mkuu wa Majeshi, (CDF 2024) yanatarajiwa kuanza Julai 20 na kutamatika Julai 30, 2024 ambapo mechi ya ufunguzi itachezwa kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa.
Akizungumza na waaandishi wa habari Mwenyekiti wa Mashindano, Brigedia Jenerali, Said Hamis Said amesema wamejiandaa vyema na kwamba mashindano hayo yatakuwa ya kuvutia, huku akitaja lengo la mashindano hayo ni kuboresha afya na kujenga umoja na mshikamano wa Wanajeshi wa Jeshi la Wananchi (JWTZ)
“Mashindano ya Kombe la Mkuu wa Majeshi yameanzishwa kwa lengo la kuwakutanisha wanajeshi wote nchini kutoka kila Kamandi ya Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania ambao ni Maafisa, askari pamoja na watumishi wa umma wanaofanya kazi jeshini, ili kuendelea kuboresha afya l na kujenga umoja, ushirikiano na mshikamano katika utendaji wa majukumu ya kila siku,” amesema Said.
Ameongeza kuwa, mashindano hayo yatahusisha timu za michezo mbalimbali kutoka Kamandi zote za jeshi hilo ambazo ni Kamandi ya vikosi vya Chini ya Makao Makuu ya Jeshi, Jeshi la nchi kavu, Kamandi ya Jeshi la Anga, Kamandi ya Jeshi la Wanamaji, Kamandi ya Jeshi la Akiba na Jeshi la Kujenga Taifa.
Timu hizo zitashiriki jumla ya michezo tisa ambayo ni mpira wa miguu kwa wanaume, netiboli kwa wanawake , mpira wa wavu kwa wanaume na wanawake , mpira wa mikono kwa wanaume na wanawake , mpira wa kikapu kwa kwa wanaume na wanawake , ngumi kwa wanaume na wanawake pamoja na mchezo wa kulenga shabaha kwa wanaume na wanawake.
“Timu hizo zitashiriki katika michezo tisa huku zikisindikizwa na kauli mbiu ya mashindano inayosema CDF CUP 2024 Ushindi na Heshima.”
Aidha Mwenyekiti wa Mashindano hayo, amesema licha ya kutimiza amza ya kuwakutanisha wanajeshi na kujenda umoja, washindi watakaopatikana kwenye mashindano hayo watapewa kombe na medali.
Mashindano hayo ya Mkuu wa Majeshi yaani CDF CUP yaliasisiwa na Mkuu wa majeshi Jenerali David Mwamunyange (mstaafu) mwaka 2014, mara ya mwisho kufanyika ilikuwa mwaka 2018 na sasa yamerejea