Dar es Salaam. Viwanda vya Tanzania sasa vitakuwa na uwezo wa kuongeza uzalishaji katika kiwango wanachokitaka, baada ya fursa ya kupata mikopo wa uwekezaji usiokua na ukomo kupitia taasisi ya viwanda Afrika.
Fursa hii inakuja wakati ambao viwanda vinapewa nafasi kubwa katika kuchochea ukuaji wa uchumi kupitia Dira ya Maendeleo ya miaka 25 inayomalizika na mpya inayoandaliwa, ambapo uongezaji wa thamani ya bidhaa za ndani unapewa kipaumbele.
Fursa ya mikopo kwa viwanda vya Tanzania, inatokana na mkataba uliosainiwa kati ya Shirikisho la wenye Viwanda Tanzania (CTI) na Taasisi ya Manufacturing Afrika kupitia ofisi ya ukaguzi wa hesabu (BDO) East Afrika.
Akizungumza katika mkutano huo, Mkurugenzi Mtendaji wa BDO Afrika Mashariki na mwakilishi wa Manufacturing Afrika, Ali Selemani amesema kupitia mkataba huo sasa, viwanda vitaweza kupata mtaji kuanzia Sh5 bilioni na hakuna ukomo wa fedha zinazoweza kutolewa.
Amesema andiko litakalotolewa na kiwanda likiweza kuendana na fedha inayoombwa, itatolewa baada ya kupitia katika mchakato unaotakiwa.
“Kuna taasisi za kutoa fedha ziko nyuma ya Manufacturing Afrika, ambacho tunasaidia ni kuwaweka sawa ili waweze kupokea fedha hizo kama mkopo au uwekezaji kwenye hisa. Kiwango cha chini ni Sh5.38 bilioni na hakuna kiwango cha juu,” amesema Selemani.
Ametoa mfano wa moja ya maeneo ambayo wanatoa huduma hizo baada ya mchakato kiwanda kilipata kiwango cha Sh134.5 bilioni.
“Kwa upande wa Tanzania kuna mazungumzo yanaendelea na moja ya kiwanda kwa ajili ya kupokea Sh215.2 bilioni. Pindi maafikiano yatakapofikiwa atapewa. Sisi tunachokifanya ni kuangalia mahitaji ya kampuni na kumshauri njia ipi ni nzuri anayopaswa kutumia ikiwa ni kupata mkopo au kukubali uwekezaji,” alisema Selemani.
Hata hivyo, kwa upande wa Tanzania amesema biashara nyingi zinamilikiwa na familia jambo ambalo huweka ugumu kwao kuuza hisa.
“Tulichokibaini ni kuwa uhitaji upo ila kujua ni wapi wanaweza kupata na gharama za kuchakata hadi mtu afikie hizo fedha ni changamoto,” amesema Selemani.
Ili kufikia vigezo vya kupewa mkopo huo miongoni mwa vitu wanavyozingatia ni kuangalia kiwango cha ajira kitakachoongezeka kwa jinsia, uzalishaji na undelevu wa biashara.
Tayari, Manufacturing Afrika inafanya kazi katika nchi za Nigeria, Senegal, Ethiopia na Rwanda na tayari Sh2.259 trilioni zimekwishatolewa.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa CTI, Leodger Tenga amesema Dira ya Maendeleo 2050 inayoandaliwa, inaelekeza viwanda na uzalishaji kuwa sehemu kubwa inayotegemewa kuchangia kufikia malengo ya dira hiyo.
Hali hiyo inafanya kupatikana kwa fursa ya uwekezaji na mitaji kwa viwanda kuwa nyenzo muhimu itakayosaidia kufikia malengo hayo, huku akiweka wazi kuwa Manufacturing Afrika wanao utaalamu na uwezo wa kusaidia upatikanaji wa mitaji kwa ajili ya viwanda.
“Kwetu sisi ni fahari kubwa sana kushirikiana nao ili kusaidia viwanda vyetu. Viwanda vinatakiwa kuchukua nafasi hii muhimu kusukuma maendeleo ya nchi yetu,” amesema Tenga.
Amesema kwa sasa msukumo mkubwa upo katika kutengeneza viwanda vinavyoweza kushindana, na hilo litafanikiwa kwa kuwapo na uongozi bora na mitaji ya kutosha.
Amesema kama nchi bado iko nyuma katika maendeleo ya viwanda kwani wakati Dira ya Maendeleo 2025 inatengenezwa, mpango ulikuwa ni mchango wa sekta hiyo kwenye pato la Taifa kuwa kati ya asilimia 15 hadi 20 ambayo haikufika.
“Mpaka sasa hivi hazijapita asilimia nane, tumekuwa tukiyumba hapo miaka 10 iliyopita. Tulitegemea mchango wake uwe unakua. Ili tupige hatua na kama tunavyoambiwa na ndiyo ukweli wenyewe kama nchi lazima tuwekeze kwenye viwanda, tuna kazi kubwa sana ya kuwekeza huko,” amesema Tenga.
Amesema jukumu hilo linahitaji mchango mkubwa wa mitaji na kuwapo kwa mazingira mazuri ya uwekezaji, ili watakaoweka fedha zao waone wanaweza kupata faida.
“Hili sasa tunatakiwa kujitahidi wenyewe wenye viwanda, tutengeneze miradi yenye uhakika au ambayo ina uwezekano mkubwa wa kufanikiwa, kwani wataalamu wapo wanaweza kuwasaidia kufanya tathmini na kusema unaweza kuleta matokeo,” amesema Tenga.