Dar es Salaam. Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam imepanga Agosti 29, 2024 kuanza kusikiliza ushahidi katika kesi ya kuchapisha taarifa za uongo kwa lengo la kupotosha umma, inayomkabili Meya wa zamani wa Manispaa ya Ubungo, Boniface Jacob (42) maarufu Boni Yai.
Mbali na Jacob, mshtakiwa wa pili katika kesi hiyo ya jinai namba 11805/2024 ni Godlisten Malisa (38) ambaye ni ofisa afya na mkazi wa Moshi mkoani Kilimanjaro.
Jacob ambaye ni mkazi wa Mbezi Msakuzi na mwenzake Malisa wanakabiliwa na mashtaka matatu, mashtaka mawili kati ya hayo yanamkabili Jacob peke yake.
Washtakiwa hao wameshatakiwa chini ya kifungu cha 16 cha Sheria ya Makosa ya Kimtandao namba 14 ya mwaka 2015.
Uamuzo huo umetolewa leo Jumanne, Julai 30, 2024 na Hakimu Mkazi Mkuu, Ushindi Swallo, baada ya washtakiwa hao kusomewa hoja za awali (PH).
Washtakiwa hao wamesomewa hoja za awali na jopo la mawakili watatu wa Serikali wakiongozwa na Wakili wa Serikali Mwandamizi, Job Mrema akishirikiana na Neema Moshi na Asiat Mzamiru.
Awali, kabla ya kusomewa kwa hoja hizo, Wakili Mrema ameomba mahakama kufanya mabadiliko madogo katika hati ya mashtaka.
“Mheshimiwa hakimu, washtakiwa wapo mbele ya Mahakama na kesi imekuja kwa ajili ya kuwasomea hoja za awali na upande wa mashtaka upo tayari,” amedai Mrema.
“Kabla ya kuwasomea maelezo yao, tunaomba kuwasilisha maombi madogo ya kufanya marekebisho ya hati ya mashtaka chini ya kifungu 234(1) cha Sheria ya Makosaya Jinai (CPA) sura ya 20 iliyofanyiwa marejeo mwaka 2022.”
Mrema baada ya kutoa maelezo hayo, mawakili wa upande wa utetezi wakiongozwa na Peter Kibatala, akishirikiana na Dickon Matata na Josephat Msanga waliomba kupewa nakala ya hati ya mashtaka ambayo imefanyiwa marekebisho.
“Mheshimiwa hakimu, sisi bado hatujapewa hiyo nakala ya hati ya mashtaka wenzetu waliyofanyia marekebisho, ikikupendeza tunaomba watupatia kabla ya hawajaanza kuwasomea mashtaka hayo,” amedai Kibatala.
Kibatala baada ya kueleza hayo, wakili Mrema aliwapatia nakala hiyo kisha upande wa mashtaka kuanza kuwasomea mashtaka.
Wakili Moshi ameanza kwa kuwakumbusha washtakiwa mashtaka kwa kuwasomea upya hati ya mashtaka.
Moshi baada ya kumaliza kuwasomewa mashtaka washtakiwa hao, wakili Mrema aliwasomea hoja za awali.
Mrema amedai katika shtaka la kwanza, Jacob anadaiwa kuchapisha taarifa za uongo mtandaoni kinyume na kifungu cha 16 cha sheria ya mtandao.
Jacob anadaiwa kutenda kosa hilo Aprili 22, 2024 ndani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwa lengo la kupotosha umma, mshtakiwa alichapisha taarifa za uongo katika mfumo wa kompyuta kupitia mtandao wa kijamii wa X (Twitter) wenye jina la Boniface Jocob@ExMayor Ubungo.
Akinukuu taarifa hiyo, Mrema amedai taarifa hizo zilikuwa zinasoma, “Wenye leseni ya kuua wameua tena…kijana wetu Robert Mlanga Mushi maarufu kama Babu G amekutwa hospitali ya kilwa road akiwa ameuawa.
“Imagine tumetoa taarifa Jeshi la Polisi la kupotewa kwa kijana wetu, cha ajabu, Jeshi la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam likawa linatusaidia kumtafuta pia.
“Kila siku Jeshi la Polisi linasema halijapata taarifa wala fununu zozote za kijana wetu na kwamba tuwe wavumilivu, wanapambana kuendelea kumtafuta. Jana machale yakawacheza ndugu wa kijana, baada ya msiri mmoja kuwatonya ndugu nendeni hospitali ya Polisi Kilwa Road mkachungulie vyumba vya kuhifadhia maiti,” inasema taarifa hiyo.
“Ndugu walivyokwenda huko Hospitali ya Polisi Kilwa Road wakamkuta kijana wao akiwa ameuawa, wahusika wa hospitali wanadai maiti ililetwa tangu tarehe 10 Aprili 2024 na askari wa Jeshi la Polisi.”
“Maiti ina siku 12 hospitali ya Polisi Kilwa Road bila Jeshi la Polisi kujua ipo hapo? Polisi waliopeleka maiti ni wa nchi gani? Walipoombwa kujua ni askari wa kituo gani na majina yao ni yapi.
“Wahusika wa hospitali hiyo ya polisi wanadai hawajui na wanaomba wasitajwe….wacha wanyonge tukazike maiti yetu, sitamani kuona hata ndugu wakiomba uchunguzi dhidi ya maiti yao, kwa sababu hata mtoto mdogo anajua hapo Muuaji ni tape.”
Shtaka la pili ni kuchapisha taarifa za uongo mtandaoni kwa lengo la kuipotosha jamii linalomkabili Jacob pekee yake.
Wakili Mrema amedai Jacob anadaiwa kutenda kosa hilo Machi 19, 2024 katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, mshtakiwa alichapisha taarifa za uongo katika mfumo wa kompyuta kupitia mtandao wake wa Kijamii X (Twitter) wenye jina la Boniface Jacob @ExMayor Ubungo kwa kuandika kama ifuatavyo.
“Mauaji Arusha, Mwananchi mwenzetu na aliyekuwa dereva wa magari ya watalii, Omari Msamo ameuawa na askari wa Jeshi la Polisi wilaya ya Karatu mkoani Arusha.
“Omari Msamo ameuawa baada ya kusimamishwa na kushushiwa kipigo kizito kilichotoa uhai wake na Polisi wa usalama barabarani baada kutuhumiwa kuendesha gari akiwa ametumia kilevi, Jeshi la Polisi linatumia kila jitihada kuzuia vyombo vya habari kuripoti tukio hili kama njia ya kuficha na kuwanusuru askari wake dhidi ya mkono wa sheria,” mwisho wa kunukuu.
Mrema ameendelea kudai shtaka la tatu ni kutoa taarifa za uongo, linalomkabili Malisa pekee yake, mshtakiwa huyo anadaiwa kutenda kosa hilo Aprili 22, 2024 katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Malisa anadaiwa siku hiyo ya tukio, kwa nia ovu na kwa lengo la kuupotosha umma na jamii, alichapisha taarifa ya uongo katika mfumo wa kompyuta kupitia mtandao wake wa kijamii wa Instagram wenye jina la Malisa gj, kwa kuandika ujumbe uliosomeka:
“Tarehe 13 Aprili meya mstaafu wa Manispaa ya Ubungo @Exmyor_bonifacejacob alitoa taarifa ya kupotelewa na ndugu yake Bw. Robert Mushi maarufu kama Babu G, ambaye alipotea mapema mwezi April 2024.
“Inadaiwa alikamatwa na watu waliojitambulisha kuwa Polisi maeneo ya Kariakoo na baada ya hapo hawakuonekana tena….leo wakaambiwa nendeni Hospitali ya Polisi Kilwa Road, ndugu yenu amefichwa mochwari pale,” wakaenda.
“La haula! Wakamkuta Robert akiwa kwenye jokofu la baridi. Hakuwa Robert tena bali ni mwili wake ukiwa na majeraha ya kipigo.
“Ni mauaji ya kikatili. Masikini Robert hajawahi kuwa na ugomvi na mtu kwanini utendewe haya,” mwisho wa kunukuu.
Aliendelea kudai kupitia machapisho hayo jamii kwaujumla ilijua ni kweli na baadaye taarifa zililifikia jeshi la polisi na upelelezi ulianza mara moja.
Amedai washtakiwa wote walitakiwa kwenda kuripoti Kituo Kikuu cha Polisi Dar es Salaam (Central).
Aprili 25, 2024 washtakiwa hao walienda kuripoti kituoni hapo na kuhojiwa na kisha kukamatwa.
Amedai Jacob alipopekuliwa alikutwa na simu tatu za mkononi ambazo ni Sumsung Galax nyeusi iliyokuwa na laini kutoka Kampuni ya Tigo: Bontel iliyokuwa na laini mbili za Kampuni ya Vodacom na Samsung Galax Note 20 Ultra Samsung.
Pia, mshtakiwa alikutwa na kompyuta mpakato aina ya HP.
Kwa upande wake Malisa alipopekuliwa alikutwa na simu mbili, aina ya Nokia Samsung Galax A 32.
“Mali zote zilichukuliwa na hati ya kuchukulia mali iliandaliwa na kusainiwa na washtakiwa hao,” alidia wakili Mrema.
Mrema alidai upelelezi ulionyesha kuwa washtakiwa wametenda makosa na kupelekea kufunguliwa kwa kesi hiyo mahakamani hapo na baada ya upelelezi kukamilika walifikishwa mahakamani.
Washtakiwa baada ya kusomewa hoja za awali, walikiri majina na anuani zao huku wakikana mashtaka yote ikiwemo kufikishwa mahakamani hapo.
Baada ya maelezo hayo, upande wa mashtaka waliomba tarahe nyingine kwa ajili ya kuanza kusikiliza mashahidi bila kutaja idadi ya mashahidi wanaotarajia kutoa ushahidi dhidi ya washtakiwa hao.
Kwa mara ya kwanza Jacob na Malisa walifikishwa mahakamani hapo Mei 6, 2024 kujibu mashtaka hayo.