Na Mwandishi Wetu,Tunduru
 
KATI ya vijana 240  walioteuliwa na Serikali kupitia Halmashauri ya wilaya Tunduru mkoani Ruvuma mwaka 2024  kwenda kujiunga na chuo cha Ufundi Nazareth kilichopo  Mbesa wilayani humo ni vijana 6 tu ndiyo walioripoti  hadi kufikia tarehe  31 Julai na kati ya hao mmoja amekimbia na hivyo kuwa na vijana 5.
 
Aidha,walioteuliwa  kwa mwaka wa masomo uliopita 2023  walikuwa 114, lakini wanaoendelea  hadi sasa na mafunzo ya ufundi ni 8 huku wengine 106 wameingia mitini hawajulikana walipo na  hivyo kushindwa kutumia vema fursa ya uwepo wa Chuo hicho kwenye wilaya hiyo.
 
Serikali kupitia Halmashauri ya wilaya Tunduru iliteua wanafunzi  waliohitimu darasa la saba na kidato cha nne mwaka 2023 na 2024 ili kujiunga kwenye mafunzo ya ufundi ili waweze kupata ujuzi katika fani mbalimbali zitakazo wawezesha kupata ujuzi  ambao utawasaidia katika maisha yao.
 
Hayo yamesemwa jana na Mkuu  wa chuo hicho Ezekiel  Mapunda,wakati akizungumza na Waandishi wa Habari mara baada ya kumalizika kwa Maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 50 ya chuo cha Nazareth Mbesa kinachomilikiwa na Wamisionari wa Kanisa la Bibilia Duniani.
 
Mapunda alisema,chuo cha Ufundi Nazareth Mbesa  kilianzishwa kwa lengo la kuwapa vijana wa Kitanzania elimu ya ufundi ili waweze kujitegemea katika maisha yao na wakati kinaanzishwa mwaka 1974 walianza na  fani ya Useremala na ilipofika mwaka 1976 waliongeza fani ya magari na mwaka 1994 walianzisha fani nyingine ya uchongaji na ukelezaji vyuma na uchomeaji.
 
Kwa mujibu wa Mapunda,ilipofika mwaka 2017 fani mbili mpya za umeme wa majumbani,ushonaji nguo na mapambo zilisajiriwa ili kupanua wigo zaidi kwa watoto wa kike kujiunga na chuo ili  nao waweze kujitegemea mara watakapomaliza mafunzo na kozi hizo zinatolewa kwa muda wa miaka mitatu.
 
Alisema, mwaka 1974 wakati chuo kinaanzishwa walianza na wanafunzi 8,lakini kwa sasa kuna  wanafunzi 150 kati yao 110 wanaishi bweni na 40 wanatoka nyumbani.
 
Alisema,walifundisha kwenye mazingira magumu kwa kutumia chaki kwa sababu walimu wengi walikuwa Wazungu,hivyo suala la mawasiliano la lugha lilikuwa gumu kwa wanafunzi waliokuwepo wakati huo.
 
Hata hivyo,kwa sasa wamepiga hatua kubwa katika suala la ufundishaji  kwani wanafundisha kwa kutumia projekta na wamefunga mtandao wa Internet wenye kasi unaowawezesha kupata vifaa vya kufundishia kwa ajili ya kuongeza uelewa kwa wanafunzi badala ya kufundisha kwa chaki.
 
“uelewa wa mtu unapanuka zaidi anapoona  na kusikia,kwa hiyo utaratibu wa uwasilishaji wa mada nyakati hizi ni bora na nzuri sana kuliko mwanzoni kulingana na mazingira ya sasa hivi na upatikanaji wa vifaa vya kufundishia na kujifunzia”alisema Mapunda.
 
Kwa upande wake Katibu Mkuu  wa pili wa Shirika la misaada la Makanisa ya Bibilia Dunian Klaus Brinkmann,amewataka Wanafunzi wa chuo  hicho kutumia ujuzi na elimu wanayoipata kufikiria kwenda kujitegemea kwa  kujiajiri badala ya kuwaza kuajiriwa Serikalini.
 
Brinkmann alisema,zaidi ya wanafunzi 1000 wamehitimu mafunzo ya fani mbalimbali tangu chuo kilipoanzishwa mwaka 1974,ambapo wengi wa vijana waliohitmu wamepata kazi kwenye taasisi na idara za Serikali na wengine kujiajiri.
 
Alisema,mafanikio hayo yametokana na  malengo waliyokuwa nayo na kutumia vizuri elimu  waliyopata wakiwa katika chuo hicho ambacho ni mojawapo ya vyuo vikongwe hapa nchini.
 
Pia amewataka kwenda kufanya kazi kwa weledi,kuwa wabunifu,waaminifu na kutengeneza bidhaa bora pindi watakapomaliza mafunzo yao ili kujenga imani kwa wateja kwenye maeneo yao iwapo wanataka  mafanikio.
 
Akitoa salamu za Mkuu wa tatu wa Misheni  Mbesa Karl Warth,Mkuu wa sita wa Misheni hiyo Helga Armbruster alisema,wakati wanaadhimisha miaka 50 ya chuo hicho baadhi ya watu wametoa fedha na michango yao ili kufanikisha malengo ya kuwawezesha vijana wa Tunduru kupata ujuzi utakao wasaidia katika maisha yao.
 
Karl Warth,amewapongeza wafanyakazi wa chuo kwa kazi nzuri wanazozifanya katika kuimarisha na kuboresha elimu ya ufundi ambayo imewasaidia baadhi ya vijana wa Kitanzania hususani wanatoka wilaya ya Tunduru kujitegemea.
 
Kwa upande wa wahitimu wa chuo hicho mwaka 1993  walisema,chuo cha Ufundi Nazareth Mbesa kimewapa mafanikio makubwa na wamekuwa tegemeo kwa familia,jamii na Taifa ikiwemo kuwapa ufundi vijana wenzao wa Kitanzania katika fani mbalimbali.
 
Hata hivyo katika risala yao iliyosomwa na Selestine Kalo,wameshauri chuo kuleta vifaa vya kisasa kwa ajili ya kufundishia na kujifunzia kutokana na kukua kwa teknolojia hasa uwepo wa magri yanayotumia gesi.
 
Vile vile,wameiomba jamii,kukiamini na kutumia fursa ya uwepo wa chuo cha Ufundi Misheni Mbesa kupeleka watoto wao kupata ujuzi utakaowasaidia  kufanya kazi za kujiletea maendeleo na kujikwamua na umaskini.