Bagamoyo. Katika juhudi za kulinda mazingira ya bahari na mazalia ya samaki, vijiji vya Pande na Kaole vilivyo katika kata za Zinga na Dunda mkoani Pwani, vimetengewa zaidi ya Sh85.11 milioni ili kuvisaidia Vikundi vya usimamizi wa rasilimali (BMU) kufaidika na mazao ya bahari.
Akizungumza jana Agosti 2, 2024 katika mkutano wa hadhara katika Kijiji cha Kaole wilayani humo, Mwenyekiti wa Mtandao wa Asasi za Kiraia Bagamoyo (Bangonet), Maria Chigota amesema mradi huo uliofadhiliwa na Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP), umelenga kulinda mazingira ya bahari.
“Miongoni mwa shughuli za mradi huu ni kujenga uhusiano kati ya wavuvi na Serikali kupitia Wizara ya Mifugo na Uvuvi ili kuwezesha kupatikana kwa boti za kisasa nne kwa ajili ya kufanyia doria baharini.
“Tutaendesha mikutano ya hadhara na wananchi katika vijiji vya Pande na Kaole ili waelewe umuhimu wa kuwa na vikundi vya ulinzi wa rasilimali.
“Tutavijengea uwezo vikundi kwa kuvipatia mafunzo ya kilimo cha mwani na ufugaji wa majongoo bahari pamoja na vitendea kazi ili viweze kujiongezea kipato,” amesema.
Akizungumzia mradi huo, Diwani wa Tarafa ya Mwambao wilayani humo, Shumia Ismail amesema utawasaidia wanawake na vijana waliojiajiri kwenye shughuli za uvuvi.
“Kwanza watapata vitendea kazi na vifaa na kujengewa miundombinu katika mradi kufunga majongoo na kilimo cha mwani, kwa hiyo utakuwa na tija zaidi.

Shaaban Mussa mkazi wa Kijiji cha Kaole wilayani Bagamoyo akizungumza katika mdahalo wa kujadili utunzaji rasilimali bahari jana Agosti 2, 2024.
Hata hivyo, ameonya wavuvi wanaotumia njia haramu kwenye uvuvi.
“Tunazidi kupaza sauti kuhusu uvuvi haramu katika maeneo yetu, kwa sababu unapovua mpaka mayai huwezi kupata samaki,” amesema.
Naye Diwani mstaafu wa Kata ya Dunda, Hashim Mwalimu amewataka viongozi wa BMU kulinda bahari kwa kuweka vipindi vya uvuvi ili samaki wazaliane.
“Kuna wakati tulifunga bahari kwa miezi sita hivi, baada ya kufunguliwa pameleta tija sana, hivyo BMU na wananchi mkae na Idara ya Uvuvi ufanyike utaratibu tufunge eneo lile na pakija kufunguliwa tutafaidika. Lakini kwa sasa samaki akizaliwa tu anavuliwa anakwenda kutumika, hiyo sio nzuri,” ameshauri.
Awali akieleza hali ya uvuvi, Ofisa Uvuvi wa Wilaya ya Bagamoyo, Ally Selemani amesema kuna wavuvi zaidi ya 2,000 na vyombo vilvyosajiliwa zaidi ya 500.
Amesema katika kulinda mazingira ya bahari, kuna vikundi vya BMU vinane katika vijiji 11 vilivyo katika kata za Zinga, Kerege, Dunda, Kisutu, Makurunge.
“Changamoto tuliyonayo ni pamoja na watu wanaoendeleza uvuvi haramu ukiwamo uvuvi wa kokoro, wengine wanatumia baruti kuvua samaki. Pia kuna mwitikio mdogo wa wananchi kuhusu sheria zinazowekwa na Serikali kuzisimamia rasilimali za bahari,” amesema.