Dili la Mpole lakwamia hapa

KILICHOTOKEA kwa mshambuliaji George Mpole, kutojiunga na timu mojawapo alizokuwa anahusishwa nazo,  Kaizer Chiefs, Richards Bay zote za Afrika Kusini na Yanga ya Tanzania ni kuchelewa kupata barua, kutoka FC Lupopo.

Mpole alijiunga na FC Lupopo, baada ya kufanya vizuri akiwa na Geita Gold, alipoibuka mfungaji bora wa mabao 17  msimu 2021/22, hivyo hakutaka kusalia na klabu hiyo ya Kongo,licha ya kuonyesha nia ya kutaka kuendelea naye.

“Hakuna timu  ingenipokea bila barua kutoka FC Lupopo, ndio maana wakati nafuatilia niliamua kukaa kimya, kwani mambo yangeenda sivyo ndivyo ingekuwa ngumu zaidi kwangu. Mkataba wangu na Lupopo aliyekuwa anaujua ni kigogo mmoja wa juu kabisa, ndio maana ilikuwa ngumu wengine kuuelewa, ila jambo la msingi kwa sasa nina barau mkononi nipo huru kwenda timu yoyote,” alisema Mpole.

Straika huyo alisema anauona uwezekano wa kupata timu za daraja la kwanza nje, ikishindikana ataendelea na mazoezi ya kulinda kiwango chake hadi wakati mwingine atakapopata timu ya kuichezea Ligi Kuu.

“Wengi wanajiuliza kipi kilinifanya nisiendelee kusalia FC Lupopo, nilihitaji kupata changamoto mpya, kwa sasa najipanga upya, soka ni kazi yangu nina imani nitafanikiwa tu,” alisema.

Related Posts