Hiki hapa kinaweza kuing’oa CCM Ikulu 2025

Miongoni mwa wabunge waliopata umaarufu katika Bunge la mwaka 2015 – 2020, ni Selemani Bungala, maarufu kama Bwege, aliyekuwa mbunge wa Kilwa Kusini kupitia Chama cha Wananchi (CUF) kabla ya kutangaza kuhamia ACT Wazalendo baada ya Bunge kuvunjwa.

Bwege alijipatia umaarufu kupitia mtindo wake wa kuchangia hoja bungeni uliokuwa ukiwachekesha wabunge na watu wengine wanaomsikiliza wakati akizungumza bungeni.

Mwananchi limefanya mahojiano maalumu na mbunge huyu wa zamani ambaye amezungumzia mambo tofauti, ikiwemo siasa za upinzani, maisha yake baada ya kukatwa mguu na mtazamo wake kwenye siasa kuelekea uchaguzi mkuu wa mwaka 2025.

Bwege anasema upinzani hauwezi kukishinda Chama cha Mapinduzi (CCM) bila wao kuungana ili kuwa na nguvu ya kukabiliana na chama hicho tawala ambacho kina nguvu kubwa ya kifedha, mamlaka na mtaji wa watu. Anapendekeza asimamishwe mgombea mmoja atakayeungwa mkono na vyama vyote vya siasa.

Mwanasiasa Selemani Bungala, maarufu kama Bwege akizungumza na mwandishi wa makala hii. Picha na Michael Matemanga

“CCM imetuzidi kila kitu, dola ni yao, pesa wanayo, hadi polisi ni wao, kuna kauli Mwalimu Julius Nyerere aliwahi kusema, kwamba wanyonge wanatengana na wenye nguvu wanaungana, ndicho kinaendelea kati ya upinzani na chama hicho tawala,” anasema Bwege.

Bwege anaamini kwamba wapinzani wakiungana, wakamsimamisha mgombea mmoja, akimpendekeza Tundu Lissu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) na Othman Masoud Othman wa ACT Wazalendo, wana uwezo wa kuwa na marais wa Tanzania na Zanzibar kwenye uchaguzi mkuu wa 2025.

“Hii itawezekana endapo tu vyama vyote vya upinzani vitaamua kuwasapoti hawa wagombea, kinyume na hapo kuing’oa CCM madarakani na upinzani kuikomboa nchi, haitawezekana,” anasema Bwege.

Anasema kwenye upinzani, hasa Tanzania Bara, kinachofanyika hivi sasa, wengi wanaangalia ubunge na ruzuku, lakini si kutaka kuikomboa nchi.

“Wazanzibari wao wana ajenda, kule wanachokitaka ni kuikomboa nchi yao, sisi Bara, upinzani hatujui tunataka nini? Ufisadi tunaoulalamikia, umasikini, maradhi na ujinga, vyote vimekumbatiwa na Serikali ya CCM.

“Hivyo ndiyo vitu upinzani tunavipinga, cha kujiuliza, nini kinatushinda kuungana? Kinachoshangaza zaidi, ACT Wazalendo na CCM wanakutana, Chadema na CCM wanakutana, lakini ACT Wazalendo na Chadema hawakutani. Anayewaonea mnakutana naye, nyinyi mnaoonewa hamkutani, ukiwaambiwa ni chawa wa CCM unasema uongo, ukiambiwa umelamba asali unakataa. Inawezekanaje?” anahoji mwanasiasa huyo.

Anasema kwenye uchaguzi mkuu wa 2025, iko wazi CCM itamsimamisha Rais Samia Suluhu Hassan kuwa mgombea urais wao, hivyo hivyo kwa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi. Hata hivyo, anahoji, wapinzani watamsimamisha nani?

Bwege anasema haoni kinachowazuia Zitto Kabwe (ACT Wazalendo), Ibrahim Lipumba (CUF) na Freeman Mbowe (Chadema) kukutana na kukubaliana kuungana ili kuikomboa nchi.

“Upinzani una nia kweli ya kuwakomboa Watanzania? Chadema na ACT Wazalendo ndiyo vyama vikubwa vya upinzani kwa sasa, vinashindwa nini kuamua kuungana.

“Tanu na ASP viliungana na kuzaa CCM, upinzani tunashindwaje? Tuisapoti Chadema na ACT hata kama siyo Lissu na Othman kwenye urais, basi wagombea watakaosimamishwa na vyama hivyo, Bara na Zanzibar, vyama vyote vya upinzani tuwasapoti, tunashindwaje?” anasema.

Akieleza mikakati ya muungano huo, Bwege anasema baada ya uchaguzi wa Serikali za mitaa baadaye mwaka huu, kila chama cha upinzani kiangalie wapi kina nguvu zaidi na kwenye uchaguzi mkuu, nguvu hiyo iunganishwe kwa kumuunga mkono mgombea mmoja wa urais.

“Bila kufanya hivi ni ngumu kuishinda CCM, mfano ni kule kwetu Kilwa, Chadema huwa hawawezi kusimamisha mawakala, hata sisi ACT kuna sehemu huwa hatuwezi kusimamisha mawakala, sasa tujiulize kuna maeneo upinzani unaweka mawakala na hata ikishinda bado haishindi, itakuwaje kwenye maeneo ambako haiweki mawakala?

“CCM huwa ina mawakala nchi nzima, upinzani utakuta Chadema ina mawakala Arusha, Kilwa hawapo, hivyohivyo vyama vingine, kwa staili hiyo unashindashindaje? Lakini tukiungana tutakuwa na mawakala nchi nzima.”

Anasema hakuna chama cha upinzani ambacho pekee kinaweza kuing’oa CCM madarakani, hicho ndicho kinaendelea kukipa nguvu chama hicho tawala ambacho anasema tatizo lake siyo mtu, ni mifumo.

Anasema hata Katiba ya sasa ambayo wanasema ni mbovu, kama ikifuatwa mambo yanaenda, lakini nayo haifuatwi. Anasema maandamano ya kule Kenya wanayaita fujo, ile siyo fujo, ni kutaka haki. Anabainisha kwamba ipo siku Watanzania nao wataamka, wataunga mkono ukweli.

“Rais akisema ukweli tunamuunga mkono, akisema uongo tumkosoe, tutafika pazuri, siyo sasa Rais akisifiwa penye ukweli tunaona sawa, akikosolewa penye ukweli tunasema uchochezi, hatuwezi kwenda,” anaeleza mbunge huyo wa zamani.

Mpango wa kugombea ubunge 2025

Bwege, aliyeshindwa kwenye uchaguzi wa 2020 baada ya kuwa mbunge vipindi viwili vya miaka mitano mitano kuanzia 2010, anasema hawezi kuacha siasa kwa kuwa ndiyo iliyomtambulisha kwenye jamii.

Hata hivyo, anasema bado hajaamua kama atagombea tena 2025 au la, japo wananchi wa Kilwa wamekuwa wakimfuata mara kwa mara kumtaka agombee. Anasema kwa sasa anasikilizia afya yake, hadi kufikia 2025, akiwa sawa atatangaza nia, kama sivyo atamchagua mrithi wake.

Anasema katika siasa kuna wabunge wa wananchi na wabunge maslahi, yeye ni wa wananchi, na chama chake cha ACT Wazalendo kina taratibu za kugombea.

“Wakati ukifika nitasema, kwa sasa ni mapema kusema, bado najiuguza kwanza, ingawa pamoja na kujiuguza siwezi kuukosa ubunge eti kwa kuwa tu nimekatwa mguu, nitaukosa kwa sababu labda wananchi hawanipendi, jambo ambalo haliwezi kutokea,” anasema Bwege.

Uamuzi mgumu ambao Bwege aliufanya ni alipotaka mguu wake wa kushoto ukatwe, huku akizungumza kwa ujasiri, anasema hakujiuliza mara mbili baada ya daktari kumueleza kuwa baada ya siku saba, mguu wake wote na sehemu ya paja la kushoto vitaoza na kupaswa kukatwa.

“Ili tatizo lisiwe kubwa, nusu ya mguu wangu wa kushoto ulitakiwa kuondolewa, muda uleule nilimwambia daktari ukateni mguu wangu sasa hivi, nipo tayari. Daktari alishtuka, akasema hajawahi kukutana na mgonjwa wa aina yangu,” anasimulia Bwege kwa msisitizo.

Anasema tatizo lililosababisha akatwe mguu ni sukari, na alipooza upande wa kulia, kisha akapata kidonda kwenye mguu wa kushoto.

“Hivi sasa nimepata nafuu sana, ilikuwa siwezi kufanya chochote, baada ya kukatwa mguu, kinachonitesa ni ganzi, sukari imepungua sana, japo presha pia inasumbua,” anasema Bwege.

Anasema siku aliyokatwa mguu, aliamini yote ni mipango ya Mungu, hakuogopa wala kuhuzunika kwa kuwa waliomshauri hivyo ni wataalamu wa afya na waliona ili apone ni lazima mguu wake ukatwe.

“Kama nilivyosema, changamoto hii haijanirudisha nyuma kisiasa, na kama nitagombea tena ubunge, siwezi kuukosa eti kwa sababu sina mguu, labda ni watu tu wanikatae,” anasema huku akitabasamu.

Baadhi ya maneno yake yaliyotikisa na kupendwa ndani na hata nje ya Bunge ni pamoja na “Ulisikia wapi?”, “inawezekanaje?”, “hatutoboi” na mengine mengi, yalimtambulisha kwa kasi mbunge huyo kwa Watanzania kupitia mtindo wake tofauti wa kuzungumza.

Anasema huko Kilwa, utendaji na uwajibikaji wake ndivyo vikimtambulisha zaidi, hasa baada ya kupambana hadi mikoa ya Kusini ikapata hospitali ya kanda ya rufaa.

Bwege, ambaye ni muumini wa uhuru na haki, anasema kama suala la mgombea binafsi lingeruhusiwa, asingetaka kugombea kupitia chama cha siasa. Anasema vyama vina ubinafsi kwa sababu kama lengo lao ni moja, kupambana umasikini, ujinga ufisadi, kwa nini hawaungani.

“Ningekuwa na uwezo ningewaambia Watanzania, upinzani tuutupilie mbali, tuache tu CCM ibaki, kwani hata sasa si ipo peke yake, hawa viongozi wakiitwa na CCM wako mbele, lakini wao wenyewe hawakutani,” anasema.

Akataa kufuata nyayo za baba yake CCM

Bwege amezaliwa kwenye familia ya kada kindakindaki wa CCM, anasema baba yake mzazi alikuwa mbunge wakati wa utawala wa Baba wa Taifa, Mwalimu Nyerere.

“Tangu mwaka 1965, baba yangu alikuwa mbunge, alidumu kwenye nafasi hiyo kwa miaka 15, mazingira ya utendaji kazi wa mzazi wangu huyo ndiyo yalinivutia hadi kujikuta naingia kwenye siasa.

“Baba alikuwa akiwasaidia sana watu, ile tabia nikaichukua mimi, hata hivyo baadaye sikupenda kuwa CCM, maana ubaya wake niliufahamu.

“Kule mtu unaweza kuwa mzuri, lakini kinachoongoza ni mfumo, nilipotaka kuingia kwenye siasa nilimwambia mzee nakwenda upinzani, akanipa baraka zote,” anasema.

Anasema aliingia kwenye chama cha Tadea, wakati huo hakuangalia sera, bali alifuata ukusini kutokana na Kambona (kiongozi wake) wa juu kuwa mtu wa eneo hilo.

“Baada ya muda sikumuelewa Kambona, ndipo nikaenda CUF, wakati huo kulikuwa kuna uchaguzi wa Serikali, NCCR, CUF na Tadea viliungana kuisapoti CUF, hapo ndipo nikajiunga na CUF.

Baadaye Bwege alihamia ACT, ambapo yupo hadi sasa, anasema alitoka CUF baada ya mgogoro na Profesa Lipumba.

“Alipotaka kujiuzulu tulimuomba sana asifanye hivyo, ikashindikana, baadaye akalazimisha awe mwenyekiti na alipewa sapoti na Serikali, sisi wengine tukaona yupo kwa maslahi yake.

“Mtu unasaidiwa na Serikali ya CCM uwe mwenyekiti halafu wewe huyo huyo upambane na CCM, huo ni unafiki, mfano mdogo tu ni huu, Mahakama ilizuia ruzuku kutolewa hadi kesi iishe, yuleyule msajili akachukua hizo pesa na kumpa Lipumba, unasemaje hapo? Si anatumiwa!” alihoji Bwege.

Anachotamani Rais Samia akifanye

Bwege anasema anatamani kuwe na Tume huru kweli ya uchaguzi na nchi ipate Katiba mpya.

“Hivi sasa Bunge linaweza kumuondoa Rais na Rais anaweza kulitoa Bunge, hii si ni kubebana! Unapiga kona mwenyewe unafunga goli mwenyewe, hii si sawa, tukipata katiba mpya mambo yatabadilika.

Anasema Samia Mwenyezi Mungu amemjalia amekuwa Rais, wakati wa mchakato wa mabadiliko ya Katiba yeye ndiye alikuwa Naibu Spika kwenye Bunge la katiba, ana kazi ndogo tu, alilianzisha basi alimalizie.

“Hata Tume Huru ni jina tu limebadilika, ni kama Mariam yuleyule aitwe Ashura.”

Migogoro kwenye vyama vya Siasa

Akizungumzia migogoro kwenye vya ya siasa, Bwege anasema hakuna chama cha siasa ambacho kipo salama.

“CCM bahati yao ni moja tu, wao ndiyo wana Dola, ikitokea chokochoko wanakuonya unarudi nyuma, huku kwingine hakuna, ukishindwa unahama.

Anasema kingine ambacho kinaleta mkanganyiko ni mtu ukitoka kwenye chama, unakosa sifa ya kuwa mbunge, na hapo hapo chama kikikufukuza unaendelea na Ubunge, huu mfumo uangaliwe kwenye haki na demokrasia, kama kungekuwa na mgombea binafsi watu wangekuwa huru,”

Anavyoutazama uchaguzi ujao

Bwege anatamani Bunge liwe na nguvu ili liweze kuidhibiti Serikali.

“Hii itawezekana kama wabunge wa upinzani watakuwa wengi Bungeni, tusiwe na Bunge la ndiyo, natamani uchaguzi ujao Bunge liwe bunge la wananchi kweli,” anasema Bwege, huku akilisifu Bunge lililoongozwa na Samwel Sita kwamba anaona kwake ndilo lilikuwa bunge imara.

Anasema anatamani uchaguzi uwe huru na haki, japo ana wasiwasi na maneno ya aliyekuwa waziri wa habari, Nape Nnauye kwamba kuna ushindi wa batili na halali.

“Hata kama CCM wamekataa, lakini huu ndio mpango wao, yule Nape itakuwa ameropoka tu na kutoa siri, ili kutupumbaza kwenye uchaguzi wa Serikali za mitaa watalegeza kidogo ili tujiamini, lakini kwenye uchaguzi mkuu wanaua, CCM ni wajanja sana.

Related Posts