Maandamano yanavyotumika kama silaha ya mabadiliko

Mataifa mbalimbali katika bara la Afrika na kwingineko duniani, yanashuhudia maandamano ya wananchi wanaoshinikiza mambo tofauti wanayotaka serikali katika mataifa yao ziyafanye kwa ajili yao.

Licha ya madhara yanayojitokeza, maandamano hayo yamekuwa yakisababisha mabadiliko katika mfumo wa maisha yao, ikiwemo mabadiliko ya sheria au uamuzi wa viongozi ambao tunazingatia matakwa ya wananchi wanaoandamana.

Mafanikio ya maandamano katika baadhi ya mataifa yanayofanywa zaidi na vijana wanaotambulika kama Gen-Z, yamekuwa yakiwavutia vijana kwenye mataifa mengine wanaokabiliwa na changamoto zinazofanana na wenzao waliofanikiwa kupitia maandamano.

Ingawa sheria na Katiba za nchi nyingi zinaruhusu maandamano, watawala wamekuwa wakipambana kuwadhibiti waandamanaji, jambo ambalo limekuwa likisababisha watu kuuawa na wengine kujeruhiwa katika mapambano hayo.

Tanzania, Kenya na Uganda ni mfano wa nchi za Afrika Mashariki zilizoshuhudia maandamano ya wananchi wanaotaka mabadiliko katika mfumo wa maisha yao.

Maandamano hayo yamekuwa yakisababisha madhara makubwa, lakini yakiambatana na mabadiliko yanayofanywa na viongozi.

Wakenya bado wanatathmini matokeo ya maandamano yaliyofanyika wiki mbili zilizopita kupinga ongezeko la kodi, ambalo lilisababisha watu kupoteza maisha, kujeruhiwa na wengine kukamatwa kwa uharibifu mkubwa wa mali.

Idadi ya waliofariki dunia kutokana na maandamano hayo imefikia 39, huku wengine 361 wakijeruhiwa, kwa mujibu wa Tume ya Kitaifa ya Kutetea Haki za Binadamu Kenya.

Hata hivyo, bado Serikali ya Kenya haijathibitisha takwimu hizo.

Maandamano hayo yalianza kama malalamiko mitandaoni kuhusu nyongeza ya kodi ya karibu dola bilioni 2.7 katika pendekezo kwenye muswada wa fedha wa mwaka 2024, yakageuka vuguvugu la kitaifa la kupinga ufisadi na utawala mbaya.

Rais wa Kenya, William Ruto amejitolea kufanya mazungumzo na vijana na ameahidi kupunguzwa kwa bajeti ya usafiri na katika ofisi yake kulingana na matakwa ya baadhi ya waandamanaji.

Vijana wa Gen-Z wasio na viongozi wamesema hawana imani na Rais Ruto katika kutekeleza mipango yake mipya ya kubana matumizi.

Agosti Mosi, 2024, maelfu ya watu waliandamana nchini Nigeria katika miji mikubwa ya nchi hiyo kudai “hatua za haraka” juu ya matatizo ya kiuchumi ya nchi hiyo, uhaba wa chakula na mfumuko wa bei.

Maandamano hayo yalianza mapema Lagos, kitovu cha kibiashara nchini Nigeria, licha ya hatua ya serikali kuzuia maandamano hayo.

Umati huo, wengi wao wakiwa vijana na wanaharakati wa haki za binadamu, waliandamana hadi katikati mwa jiji na maeneo ya biashara ya Ikeja, Ojota na Ojodu, huku wakiimba:

“Tuna njaa, usituue, njaa na ugumu wa maisha, sera za kupambana na umasikini, maliza ugumu sasa!”

Kwa mujibu wa ripoti ya DW, takriban watu 13 walipoteza maisha siku ya kwanza ya maandamano hayo, huku wengine 300 wakikamatwa na polisi.

Wakati maandamano hayo yakiendelea, imeanza kusambaa video ikionesha kundi kubwa la watu wakiwa wamebeba viroba vya mchele ambao kwa mujibu wa madai yaliyopo ni waandamaji waliopewa chakula ili wasitishe maandamano yao.

Nchini Uganda, wananchi nako wameandamana na takribani watu 45 walizuiliwa na maofisa wa usalama baada ya kukamatwa Julai 23, 2024 wakijaribu kuandamana kwenda bungeni kama ishara ya kupinga ufisadi nchini humo.

Rais wa Uganda, Yoweri Museveni alisema ana maelezo ya kutosha kuthibitisha kuwa waliopanga kufanya maandamano nchini humo, walifadhiliwa na vyanzo vya nje.

Juzi, Waziri Mkuu wa Bangladesh, Sheikh Hasina alijiuzulu na kukimbia nchi kutokana na maandamano yanayoendelea yaliyosababisha vifo vya watu takribani 300.

Tovuti ya Al Jazeera imeripoti kwamba Hasina aliondoka nchini humo Agosti 5, mwaka huu baada ya wananchi kupuuza amri yake ya kutotoka nje na kuvamia Ikulu ya Waziri Mkuu huyo iliyopo jijini Dhaka.

Takribani watu 300 wamefariki tangu kuanza kwa maandamano hayo wiki kadhaa zilizopita nchini humo, huku waandamanaji vijana wakilalamikia hali ngumu ya maisha na ukosefu wa ajira.

Wachambuzi wa masuala ya siasa

Wakizungumzia mwenendo huo wa maandamano, wachambuzi wa siasa wanasema watawala kujigeuza wafalme na kuacha kushughulikia kero za wananchi, ndiyo sababu kubwa inayochochea maandamano hayo katika mataifa mbalimbali.

Mchambuzi wa siasa, Buberwa Kaiza anasema kuongezeka kwa matabaka kati ya walionacho na wasionacho limekuwa likiwahamasisha vijana kuandamana kwa sababu wanaona wachache wanaonufaika na keki ya Taifa kupitia rasilimali za umma.

“Huwezi kuvumilia kuona watumishi wa umma wanajenga majumba makubwa, wanaendesha magari ya gharama wakati wewe huna chakula nyumbani. Lazima waingie barabarani, ninaamini hiyo ni njia pekee iliyobaki kwa kuwa watawala hawataki kuwasikiliza,” anasema Kaiza.

Ameongeza kwamba ili kuondokana na vuguvugu hilo, serikali ihakikishe wananchi wake wanaishi maisha bora, kodi zinatumika vizuri kwa ajili ya maendeleo ya wananchi wao na kuhakikisha vijana wanapata ajira ili waendeshe maisha yao.

Kwa upande wake, Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (Udsm), Dk Richard Mbunda anasema maandamano ya vijana yanachochewa zaidi na ukosefu wa ajira na ugumu wa maisha, hivyo wanaziamsha serikali zao zitatue changamoto hizo.

“Maandamano ya wananchi wenyewe yana nguvu zaidi kuliko yale ya vyama vya siasa. Wananchi wanakuwa na ajenda yao moja wanayoisimamia na wanafanikiwa kwa sababu wanapambana kwa dhati kuleta mabadiliko,” anasema Dk Mbunda.

Related Posts