Mastaa Royal, Pazi wanaotisha BDL

MAMBO ni moto. Wakati timu za kikapu za  wanawake zikichuana katika  Ligi ya Kikapu Mkoa wa Dar es Salaam (BDL), kwa upande wa mastaa wanaocheza nafasi ya kati,  Juliana Sambwe wa Tausi Royals  na Maria Alex kutoka Pazi Queens wamekuwa kivutio katika ligi hiyo.

Kivutio cha wachezaji hao kinatokana na uwezo mkubwa walionao wa uchezaji katika kuunganisha  wachezaji wenzao mpaka timu zao zinapata ushindi, wakimiliki vyema dimba la kati.

Wachezaji hao wote wawili wanacheza nafasi ya kati ‘point gurd.’

Juliana aliyewahi kucheza katika Ligi ya Gradlators ya Burundi, mbali ya kuchezesha timu amekuwa ndiye nyota tegemeo kwa ufungaji upande wa timu yake.

Mchezaji huyo ana uwezo wa kufunga katika maeneo ya mitupo mitatu ‘three pointi’ na pia katika eneo la ndani ya duara la goli ni mjanja wa kufunga  kwa kutumia mkono wa kushoto endapo amebanwa  kulia.

Kwa upande Maria, mbali ya kucheza nafasi ya uchezeshaji amekuwa akicheza pia nafasi ya ulinzi  na upande wa ufungaji pia ni tegemeo akifunga katika maeneo ya mitupo mitatu. 

Mchezaji huyo aliyewahi kuchezea Ukonga Queens kwa misimu minne ameonyesha uzoefu kumbeba katika ligi hiyo.

Denis Lipiki, kocha wa timu ya taifa ya Vijana alisema wachezaji hao wana uwezo mkubwa kuchezesha na kufunga pointi.

“Kwa kweli tumekuwa tukiona  viwango  vizuri vinavyochezwa na wachezaji hao, kwa jinsi wanavyocheza  nawashauri waendelee hivyo,” alisema Lipiki.

Related Posts